Yote kuhusu miaka tisa ya Simba Day haya hapa

Klabu ya Simba, leo Jumanne itatimiza mwaka wa tisa wa tamasha lake  lililobatizwa jina la ‘Simba Day’ kwa kucheza na Rayon Sport  kutoka nchini Rwanda.
Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa klabu hiyo kucheza mechi ya  tamasha lake na timu kutoka Rwanda, kwani miaka yote mitane  imecheza na timu za nchi tatu ambazo ni Kenya, Uganda na Zambia.

Historia ya Simba Day

Kwa ufupi tu ni kwamba Simba Day ilianzishwa mwaka 2009 chini  ya uongozi wa mwenyekiti wa wakati huo Hassan Dalali pamoja na  Katibu wake mkuu Mwina Kaduguda.
Hutumia siku hiyo walioichagua ambayo ni Agosti 8 ya kila mwaka  kutambulisha kikosi chao chote cha msimu unaofuata wa ligi na  hata mechi za kimataifa.
Hufanya hivyo kwa kutambulisha mchezaji mmoja mmoja na namba  atakayoivaa kwa msimu husika, pamoja na kuonyesha jezi mpya za  msimu watakazotumia.
Msimu huu itawatambulisha wachezaji wapya wanaotarajiwa kuwa  kivutio kikubwa, wakiwemo Emmanuel Okwi anayerejea kwa mara  ya tatu, pia Haruna Niyonzima kutoka Yanga, Aishi Manula na John  Bocco kutoka Azam FC.
Sambamba na hilo, siku ya Simba Day, uwanjani hapo hutawaliwa  pia na burudani kadha wa kadha kutoka kwa bendi na wasanii  mbalimbali maarufu ambao wanakuwa wapo kwenye chati wakati  huo.
Tamasha hilo la Simba kuwa ni hitimisho la wiki nzima kwa  viongozi wa klabu hiyo, wanachama, mashabiki na wachezaji  kutembelea na kutoa misaada sehemu mbalimbali za kijamii kama  vile kwenye vituo vya watoto yatima, hospitalini na hata kufungua  matawi.
Yafuatayo ni matokeo ya mechi zote za tamasha la Simba Day tangu  ianzishwe.

1. Simba 1-0  SC Villa (2009)

Hii ndiyo mechi ya kwanza kabisa ya Simba Day ilipoanzishwa na  timu ya SC Villa kutoka nchini Uganda kualikwa.
Katika mechi hiyo Simba iliifunga SC Villa bao 1-0. Bao hilo  lilifungwa katika dakika ya nane tu ya mchezo na kiungo Hilary  Echessa, akiwa ndiyo kwanza amesajiliwa kutoka timu hiyo hiyo  aliyoifunga.
Mechi hii ilichezwa kwenye uwanja wa Uhuru kwa sasa lakini  zamani ukiitwa wa Taifa.
Ulikuwa msimu wa kwanza wa wacheza Emmanuel Okwi na Joseph  Owino kusajiliwa Simba ambao nao walicheza kwa mara ya kwanza  mechi hiyo wakiwa na timu yao mpya.

2. Simba 0-0 Express (2010)

Simba iliadhimisha mwaka wake wa pili wa Simba Day kwa  kulazimishwa sare ya bila kufungana na wageni waalikwa timu ya  Express kutoka nchini Uganda kwenye uwanja wa Uhuru.

3. Simba 0-1 Victors (2011)

Mwaka wa tatu Simba iliadhimisha siku yake,  kwa kupokea kipigo  cha bao 1-0 kutoka kwa timu ya Victors nayo pia kutoka nchini  Uganda.
Mechi hii ilichezwa kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini  Arusha na kuweka rekodi ya mechi pekee ya Simba Day kuchezwa  nje ya Dar es Salaam.
Bao la washindi lilifungwa dakika ya 70 kwa njia ya penati  na  Patric Sembuya.

4. Simba 1-3 Nairobi City Stars (2012)

Simba ilipokea kipigo kikali cha mabao 3-1 toka kwa Nairobi City  Stars kutoka nchini Kenya, mechi iliyochezwa kwenye uwanja mkuu  wa Taifa. Huo ni mwaka wa nne wa Simba Day.
Mabao ya washindi walifunga na Duncan Owiti, Bruno Okullu  na  Boniphace Onyango.
Bao pekee la Simba lilifungwa na Felix Sunzu kwenye dakika ya 15.

5. Simba 4-1 SC Villa (2013)

Simba ilifanya kufuru kwa kuisasambua bila huruma SC Villa ya  Uganda mabao 4-1 kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Magoli ya Simba kwenye mechi hiyo ya tamasha yalifungwa na  Jonas Mkude, William Lucian ‘Gallas’, na Betram Mombeki  aliyefunga magoli mawili katika dakika ya 70 na 72.

6. Simba 0-3 Zesco (2014)

Kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya Zesco kilikuwa ni cha tatu kwa  Simba kwenye mechi zake za tamasha la Simba Day mwaka 2014.
Yalikuwa ni mabao ya Jackson Mwanza kwenye dakika ya 14,  Clatos Chane dakika ya 64 kwa penalti na Mayban Mwamba  dakika ya 90.

7. Simba 1-0 SC Villa-2015

Kiungo Awadh Juma aliwainua vitini mashabiki wa Simba kwa  kufunga bao pekee dakika ya 89 na kuifanya timu hiyo kuibuka na  ushindi wa bao 1-0 dhidi ya SC Villa.
Tayari baadhi ya mashabiki wa timu hiyo walikuwa wameshatoka  uwanjani, wakiamini kuwa mechi hiyo ingetoka sare.

8. Simba 4-0 AFC Leopards-2016

Ibrahim Ajib ambaye kwa sasa yupo Yanga aliifungia Simba magoli  mawili kwenye mechi hiyo ya nane ya tamasha hilo.
Straika Mrundi, Laudit Mavugo akiwa ndiyo kwanza anajiunga  kutoka Vital’O ya Burundi alifunga bao moja, huku Shiza Kichuya  ambaye naye alikuwa akiichezea Simba kwa mara ya kwanza  akitokea Mtibwa Sugar, akifunga bao moja.
Kwa matokeo hayo kabla ya mechi ya kesho, Simba imeshinda  mechi nne kwenye tamasha lake hilo, sare moja na kufungwa mechi  tatu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *