Yanga yajipanga kumaliza kwa kicheko

Kindumbwendumbwe cha ligi kuu Tanzania bara mzunguko wa pili msimu wa 2017-18 kuanza tena leo jumamosi tarehe 3, Februari 2018.

Ni takribani mechi 240 zinatarajiwa kurindima katika viwanja mbalimbali mpaka hapo tamati ya ligi itakapofikiwa na kumtoa bingwa wa msimu atakaeiwakilisha nchi katika michuano ya klabu bingwa Afrika msimu wa 2019.

Mzunguko wa kwanza ulitamatika mwishoni mwa mwezi Januari na mnyama Simba SC kumaliza mzunguko huo wakiwa kileleni mwa ligi wakionesha dhamira ya kulitwaa taji hilo kubwa kabisa kisoka Tanzania ambalo ni takribani misimu sita! sasa wameshindwa kulinyakuwa wakifanya hivyo mara 18 tu toka kuanzishwa kwa ligi hii mwezi Januari 19, 1965.

Yanga SC mabingwa watetezi wa ligi hii, leo watakuwa mkoani Iringa kuwakabili Lipuli FC katika ufunguzi wa duru hili la pili la ligi. Mechi ya mzunguko wa kwanza jijini Dar es salaam timu hizo zilikwenda sare ya 1-1.

Wengi wanaitazama kama mechi ya kukamiana pande zote. Lipuli wakidhamiria kumuonesha bingwa mtetezi hawakubahatisha mechi ya awali kumnyima alama tatu! na tayari wameanza tambo za kutoka na ushindi nyumbani leo ili kuanza vyema mzunguko huu.

Yanga SC kupitia afisa habari wao Dismasi Teni wamesema wanauanza msimu huu kwa hesabu za mbali sana lengo kuu likiwa ni kutetea ubingwa wao.

“ tumejipanga vyema mzunguko huu. Tunaheshimu uwezo wa timu zote 15 tutakazokutana nazo lakini lengo letu ni kushinda kila mchezo ili hesabu za ubingwa zikipigwa mwisho wa ligi ziwe vyema upande wetu. Lipuli ni timu nzuri na sisi tumejipanga vyema kuwa bora uwanjani ili kuondoka na alama tatu” Alisema Dismas Teni.

Mashabiki na wanachama wandamizi wa klabu hiyo kwa nyakati tofauti wamekaririwa kujinadi kutetea taji lao licha ya hasimu wao mkubwa Simba SC kuwatangulia mbele kwa alama nyingi. Simba wapo kileleni wakiwa na alama 35 ilihali Yanga wanashika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi kwa alama 28 wakitanguliwa na Azam FC wenye alama 30 nafasi ya pili.

Yanga wanaikabili Lipuli FC bila kiungo mshambuliaji wao Ibrahim Ajibu ambaye amekuwa msaada mkubwa kwa timu hiyo katika mechi mbalimbali . Ajibu anaikosa mechi ya leo kwa ugonjwa sambamba na Mwinyi Haji ambaye pia ni mgonjwa.

By Samuel Samuel

One Comment

  1. Pingback: Yanga yajipanga kumaliza kwa kicheko

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *