Yanga haijui biashara na biashara haiwajui Yanga

Viwanja vya soka hutumika kama jukwaa la biashara. Jukwaa hili hutumika na makampuni mbalimbali kuweka matangazo yao ili kuwafikia watumiaji wa mwisho wa bidhaa zao, hawa tunawaita walaji wa bidhaa za makampuni hayo.

Jezi za timu mbalimbali ni jukwaa jingine kwa timu hizo kufanya biashara kubwa na makampuni yanayohitaji kuwafikia walaji wa mwisho wa bidhaa zao. Achana na idadi ndogo ya mashabiki wanaohudhuria kwenye viwanja vya soka nchini.

Matangazo ya kwenye jezi huweza kuwafikia walaji kwa picha za video kwenye makundi mbalimbali ya mitandao ya kijamii, picha za mnato zinazosambaa kwa njia ya mitandao ya kijamii na magazeti ambazo zinauwezo wa kudumu kwa muda mrefu zaidi.

Pia, kuna zile kamera za Azamtv zinazowafikia hata wasiokuwepo uwanjani, huyu ni mtu wa kati kati ya walaji na timu husika.

Kwenye michezo miwili ya kirafiki ambayo timu ya Yanga imecheza ndani ya wiki mbili hizi baada ya kuanza kwa Ligi Kuu Bara, ukiwemo mchezo dhidi ya KMC na ule dhidi ya Rhino Rangers, Yanga ilitumia jezi za wadhamini wa Ligi hiyo, ambao ni Kampuni ya Mawasiliano ya Simu za Mkononi, Vodacom.

Ikumbukwe kwamba michezo hiyo miwili haikuwa ya Ligi Kuu Bara, bali ilikuwa ni michezo ya kirafiki tu. Zile jezi za Vodacom hazikupaswa kuvaliwa kwenye michezo ile.

Vodacom ilipewa matangazo ya bure siku ile, hawakuhitaji kuwaomba Yanga wala kuwalipa walau thumni ili wavae jezi zao, hapa Yanga haikujua maana ya biashara kwa kutumia jezi zao, siku ile wangeweza kuingiza kitita kikubwa cha fedha kupitia matangazo ya kwenye jezi zao tu.

Pia Yanga kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya KMC hawakuweka tangazo la uwanjani la wadhamini wao wakuu, yaani Kampuni ya Michezo ya Kubashiri, Sportipesa, hii ni kudumaza biashara yako, kutoonesha thamani halisi ya mdhamini wako.

Kwa upande wa Azam, waliweka matangazo tu ya Makampuni ya Azam, Benki ya NMB inayoidhamini Azam ambayo haikucheza siku hiyo. Hii ilisababishwa na aidha, Azam ambao ni wamiliki wa Azam Complex kutopokea maombi ya Yanga kuhitaji kuweka matangazo yake au Yanga kutoijua biashara.

Kuhusu sakata la jezi unaweza kujiuliza Yanga haina jezi zingine? Kwanini inatumia jezi za Vodacom kwenye michezo isiyo ya Ligi Kuu? Jibu jepesi ni kwamba, Yanga haijui biashara na hata biashara haitaki kuwajua Yanga. Rafiki mfanye rafiki na mnafki achana nae!

Ni hivi juzi tu, kwenye mchezo wa mpira wa kikapu nchini Marekani ilipanga mpango mkakati maalum wa kuzitumia vizuri jezi zao kujiiingizia mkwanja mrefu. Yanga imesalia kwenye eneo ililopo na haitaki kusogea.

Mchakato huanzia kwenye takwimu halisi za watu wanaohudhulia kuushuhudia mchezo wenyewe na wale wanaoutazama kupitia televisheni, mchakato huu ni lazima usimamiwe na meneja masoko wa klabu husika, huyu huhusika na kuwaambia watu wanaohitaji kuweka matangazo yao takwimu halisi na vipi matangazo hayo yatawafikia walaji wa mwisho.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *