Wanawake, umaarufu na ulevi sababu ya Waafrika kushindwa kucheza nje

Rais wa FIFA ,Gian Infantino akimkabidhi Mohamed Salah tuzo ya mchezaji bora wa Dunia kwa nchi za kiarabu 2016

Rais wa FIFA , Gianni Infantino akimkabidhi Mohamed Salah tuzo ya mchezaji bora wa Dunia kwa nchi za kiarabu 2016

Kila mchezaji anayecheza mpira wa miguu ndani ya bara la Afrika, ndoto zake ni siku moja kupata nafasi ya kucheza soka la kulipwa ughaibuni ( Ulaya) ambako kumekua na mvuto mkubwa wa malipo mazuri, matangazo na miundombinu.

Lakini ukiwauliza wachezaji hao, ni vipi utaweza kufika Ulaya kucheza mpira kwenye miundombinu mizuri, maslahi na matangazo wanakosa majibu, zaidi utasikia nikipata nafasi….

Mohamed Salah mchezaji bora wa Dunia 2016 kutoka nchi za Kiarabu, ameelezea kipi kinachowakwamisha wachezaji wengi wa  Afrika kuweza kusakata kandanda barani Ulaya.

Salah mchezaji wa timu ya Taifa ya Misri (Pharaos) na AS Roma ya Italia ambaye pia amewahi kuvichezea vilabu vya FC Basel, Chelsea, Fiorentina (mkopo) , amesema wanawake, umaarufu na ulevi (starehe) kwa kifupi ndio imekua kikwazo kwa wachezaji wengi.

Akitolea mfano nchi yake ya Misri, Salah amesema wachezaji wengi kutoka nchini Misri wamekua wakipata nafasi ya kusajiliwa na vilabu vya Ulaya, lakini mwisho wa siku wanaamua kurejea nyumbani sababu ya kuyakosa maisha waliyoyazoea kuishi nyumbani.

Mchezaji akiona haongelewi kwenye vyombo vya habari, hapati nafasi ya kufanya starehe ikiwemo wanawake na ulevi, anaona bora arejee kucheza ligi ya nyumbani ambapo vitu hivyo vyote atavipata. “Alisema Salah”

Ameendelea kusema Ulaya ili uwe maarufu inabidi ufanye kazi ya ziada, upiganie namba katika kikosi chako cha kwanza na kutoa msaada mkubwa kwa timu yako, kitu ambacho kila mchezaji  anakua na malengo yake, hivyo hana budi kukubaliana na hali halisi na kusahau starehe za nyumbani.

Mwisho Salah amesema ndio maana wachezaji wengi wa Misri wamekua wakienda Ulaya na kukaa miezi 6, mwaka 1 na kushindwa kuvumilia na kuamua kurejea kucheza nyumbani katika vilabu vya Al Ahly, Zamalek, nk.

Baada ya kusoma mahojiano hayo ya Salah na kituo kimoja nchini Misri, nikagundua tatizo hili pia limekuwepo Tanzania, kila mchezaji ukiongea nae ana ndoto za kucheza soka ulaya, swali Je amejipangaje kuzikabili changamoto hizo?

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *