Usajili Yanga msimu wa 2017-18

Kikosi cha Yanga

Kabla ya kuangazia usajili wa Yanga SC kwa msimu ujao wa ligi kuu Tanzania bara na michuano ya klabu Bingwa Afrika mwakani, kwanza tukitazame kikosi cha msimu uliopita kupitia hilo ndio tutajua mahitaji ya timu kwa msimu ujao.

Msimu wa 2016-17 Yanga hawakuwa vyema sana kama misimu miwili iliyopita licha ya kuibuka mabingwa wa ligi kuu kwa tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa dhidi ya Simba SC walioishia nafasi ya pili.

Kwa sehemu kubwa kikosi cha wachezaji 27 kilitawaliwa na majeruhi, kushuka viwango vya baadhi ya wachezaji na kwa zaidi ya asilimia 30 wakiwa ni averaged players ambao hawapo katika viwango vikubwa kulingana na mahitaji ya timu hususani katika michuano ya kimataifa.

Lakini pia sababu nyingine ni kukosa motisha na morali ya kazi kutokana na klabu kukumbwa na tatizo la kiuchumi. Yanga walipoweza kuikamata Simba waliokuwa mbele kwa alama 8 zaidi yao , basi klabu ilitakiwa kuongeza hamasa, ari na motisha kwa wachezaji lakini ndio kwanza posho zikaanza kusumbua na mishahara hali iliyopelekea timu kupoteza baadhi ya mechi sare , kutolewa klabu bingwa na kushindwa kabisa kuvuka hatua ya makundi kombe la Shirikisho Africa.

Kimbinu na kiufundi kwa msimu wa 2016-17

Kongole nitoe kwa George Lwandamina ambaye baada ya kuipokea timu tu alijua sehemu kubwa ya wachezaji vipaji vimedumaa, majeruhi na timu nzima kwa ujumla kuwa katika fatigue kutokana na kucheza mfululizo kwa misimu miwili hivyo alianzisha programu yake maalumu ya kuwatumia wachezaji wote kikosini kwa short term plan na long term plans kwa wale ambao wangeweza ku ‘ adopt ‘ mfumo na mbinu zake ili kila nafasi katika timu iwe na back up ya mchezaji ambaye anaweza kucheza angalau kwa asilimia 50 katika kiwango cha mchezaji wa kudumu.

Mfano alimpa Geofrey Mwashuiya wing ya kushoto ambayo mara nyingi ilikuwa ikishikiliwa na Deusi Kaseke au Haruna Niyonzima. Kaseke alianza kuonesha kuchoka na mara nyingi kucheza chini ya kiwango . GM aliweza kuimudu vyema nafasi hiyo na kuingia kikosi cha kwanza hata kucheza mechi ya klabu bingwa Afrika marudiano na Zanaco kule Zambia.

Eneo la kati licha ya ujio wa Zulu lakini Lwandamina alijaribu mara kadhaa kumpa nafasi Juma Makapu ili kupata back up ya Kamusoko na Justine Zulu. Baadhi ya mechi Makapu alizumudu vyema na watu kumsifu kocha kurudisha kipaji cha mchezaji huyo ingawa bado anaingia katika kundi la averaged players ambao wanakosa mwendelezo mzuri wa vipaji vyao . Wanapanda na kushuka .

Safu ya kiungo ; Juma Mahadhi alikosa nafasi katika kikosi cha Hans Van Pluijm ambaye alimsajili kama mbadala wa Saimoni Msuva wing ya kulia au kusaidia wing ya kushoto au kumpanga kama central winger lakini mdachi katika mechi zake 15 alimpa mechi mbili tu za ligi kuu na mbili za kombe la Shirikisho dhidi ya TP Mazembe na Medeama mechi alizoonesha kipaji kizuri . Lwandamina aliamua kumpa nafasi kama ” false 10 ” akicheza kama playmaker wa juu aidha na Haruna Niyonzima au Obrey Chirwa ikiwa ni fursa mpya kwa kinda huyo kuonesha kipaji chake . Hakuwa na mafaniko mazuri sana kiufundi.

Beki ya kulia tumeona Lwandamina alivyoleta upinzani mkali kati ya Hassani Kessy na Juma Abdul pia changamoto kwa wakongwe Nadir na Yondani kwa kijana Vicent Andrew ambaye alipata mechi nyingi ingawa mwishoni alisugua benchi kutokana na makosa ya hapa na pale .

Hii ni mifano michache ya jinsi Lwandamina alivyojaribu kuokoa jahazi la Yanga SC kutetea mataji yake ligi kuu, ASFC na ushiriki kimataifa . Mafanikio hayakuwa makubwa lakini aliweza kutetea kombe la ligi kuu.

Nini kifanyike msimu wa 2017-18?

Kwanza kabisa ukiondoa masuala yote ya kimbinu na kiufundi yaliyowasumbua , tatizo kubwa ambalo liliwatesa Yanga SC ni fedha . Hivyo kama klabu katika usajili wa msimu huu lazima iangalie wachezaji wenye gharama nafuu lakini wana uwezo mkubwa kuitumikia klabu hiyo ili klabu isijekuwa na shida ya kulipa posho na mishahara kama msimu huu.

Wapo wachezaji ambao wana uwezo mkubwa na wenye gharama nafuu na pia nidhamu zao nzuri ndani ya uwanja na nje ya uwanja . Ni kiasi cha scouting team ya Yanga na bechi la ufundi kuwatafuta wachezaji hao . Mfano uwezo wa Yusufu Ndikumana wa Mbao FC ni mkubwa lakini klabu yenye misuli midogo ya kiuchumi kama Mbao imeweza kumhudumia mchezaji huyo.

Tukiachana na hilo la kifedha sasa niangazie kiundani mustakabali wa timu kimbinu na kiufundi.

Nafasi ya walinda milango ..

Klabu ina walinda milango watatu wenye uwezo mzuri Deogratius Munishi , Beno Kakolanya na Ali Mustafa. Hapa kocha anatakiwa kumwachia golikipa mmoja na kumpandisha golikipa mmoja wa timu B. Ali Mustafa ambaye hapati nafasi ya kucheza amwachie aidha kwa mkopo au kuvunja mkataba na kuacha ushindani kwa Deogratius Munishi na Beno Kakolanya huku wawili hawa wakitoa changamoto ya kujifunza kwa yule golikipa wa timu B. Ana uwezo mzuri na itakuwa exposure kubwa kwake .

Msimu wa 2015-16 lango la Yanga SC lilikamatwa na magolikipa wawili tu Deo na Ali huku Tinocco akikosa kudaka hata mechi moja hivyo klabu inaweza kuwa na magolikipa wawili wazuri na msaidizi wao toka timu B ambaye baada ya muda atakuwa katika kiwango kizuri kwa kujifunza kwa wenzake . Hapo kwanza klabu itakuwa imepunguza gharama kwa Batezi na kuingia mkataba mwepesi na golikipa wa timu B pia kiwango chake cha mshahara kitakuwa kidogo.

Beki ya kulia hakuna haja ya kutafuta mtu . Juma Abdul na Hassani Kessy bado wapo vizuri kuimudu vyema nafasi hiyo . Kikubwa ni mwalimu katika kipindi cha preseason kumjenga vizuri Kessy katika hali ya kucheza kama modern fullback right ambaye ana uiwiano mzuri katika kulinda na kusaidia mashambulizi.

Upande wa kushoto ni dhahiri kaka yangu Oscar Joshua umri umemtupa mkono kisoka pia ameshindwa kumpa changamoto chanya Haji Mwinyi . Huyu anahitaji apewe mechi ya heshima kumuaga na kuleta mbadala mzuri wa Haji Mwinyi . Gadiel Michael wa Azam FC angefaa sana nafasi hiyo .

Walinzi wa kati; Heshima tu kuendelea na Nadir Haroub kwa msimu ujao licha ya ufanisi wake kupungua lakini aendelee kubaki kama nembo ya klabu . Vincent Bossou mkataba umekwenda ukingoni , huyu ni moja ya walinzi wa kati wazuri sana lakini klabu itazame gharama zake na nidhamu yake kama itapata mbadala wake basi hakuja haja ya kuongeza mkataba wenye gharama kubwa na kugeuka mzigo kwa klabu .

Narudia kumtolea mfano Yusufu Ndikumana wa Mbao FC katika nafasi hii . Ni mlinzi mzuri pia ana uwezo mzuri kucheza kama kiungo wa kati nafasi ambayo imekuwa ikiitesa sana Yanga mpaka Lwandamina kuanza kumtumia Yondani kwenye baadhi ya mechi.

Kiungo cha kati hakuna mjadala si Zullu wala Makapu ambaye anaweza kuikoa Yanga SC kwa msimu ujao hususani mechi za klabu bingwa Afrika. Hapa klabu ivunje kibubu chake kwa kusajili mchezaji mzuri toka nje au ndani ili kupata muunganiko mzuri kimbinu tokea kati . Chaila wa Zesco United ni chaguo sahihi au kupata mzawa juu ya Jonasi Mkude ili kuiweka sawa nafasi hiyo .

Saimoni Msuva ana mkataba mpaka mwakani lakini mawakala mbalimbali kumtaka akacheze nje tayari kunaifanya saikolojia yake kujipanga na soka la nje hivyo kumng’ang’ania si jambo jema sana . Hapa kuna vitu viwili ; kwanza kabisa klabu inaweza kufanya biashara nzuri ya kumuuza na kutafuta mbadala wake lakini siafiki kwa Juma Mahadhi kuuzwa au kutolewa kwa mkopo . Kiasilia Mahadhi ni kiungo wa pembeni ubaya ni waalimu wote wawili yaani Lwandamina na mtangulizi wake Hans Van Pluijm wamekuwa wakimtumia kati nafasi ambayo ameishindwa kabisa na kila mara kutupiwa lawama . Mahadhi apewe nafasi wing ya kulia aidha akiwa na Msuva au yoyote atakayekuja.

Kushoto Mwashuiya amekuwa na mwendelezo mzuri sema anahitaji vitu vidogo tu apunguze dribbling zisizo na faida kwa timu na kucheza kwa faida ya timu .

Nikiingia eneo la kati wachezaji kama Mateo na Busungu ni kazi moja tu kuwatoa kwenye timu kwa msimu ujao wa ligi . Busungu nidhamu mbovu na kwa upande wa Mateo kipaji kimegoma kupanda hivyo anaweza kupelekwa kwa mkopo au kumvunjia mkataba kama bado upo au kumwacha aende. Nafasi zao lete vijana wenye uchu wa kuchora ramani zao kisoka kama Waziri Jr wa Toto Africa, Mbaraka Yusufu toka Kagera Sugar na Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting. Lakini pia eneo hili la kati kama mlivyofanya msimu unaokwisha kwa Yusufu Mhilu pia Maka Edward wa kikosi B aliyeshika dimba mechi na AFC mpeni nafasi. Ni kijana mzuri na ana kipaji kizuri.

Haruna Niyonzima hakuna mjadala ongeza mkataba bado ana uwezo mkubwa kuichezea Yanga SC sambamba na pacha wake Thabani Kamusoko. Wakati huo mnatakiwa kumpandisha Samwel Greyson mfungaji wa goli la tatu mechi na AFC Arusha. Ana uwezo wa kucheza vyema kama mshambuliaji wa kati na kiungo mshambuliaji.

Tambwe ooops! kama Lwandamina atapewa fungu la maana kwa usajili mzuri wa maandalizi ya mechi za klabu bingwa Afrika hana budi kutafuta mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa mechi za kimataifa. Tambwe ni mzuri sana ndani ya ligi lakini amekuwa hana msaada mzuri mechi za kimataifa hivyo GL msimu huu nafasi za kimataifa ni lazima aziangalie kwa jicho la tatu.

Donald Ngoma bado ni mchezaji mzuri sana kubaki Yanga lakini linapokuja suala la gharama, nidhamu na mchezaji binafsi kukosa passion ya kuitumikia klabu kutokana na vurugu za hapa na pale, mwalimu hana budi kumwachia na kutafuta mtu mwingine mwenye uwezo zaidi yake na gharama nafuu tukilenga mgawanyo wa milioni 900 za Sportspesa ambazo zinatoka milioni 77 kwa mwezi hivyo matumizi makubwa au gharama kubwa za uendeshaji klabu zinaweza kuwafanya Yanga kukwama.

Mwisho…

Katika kumalizia naweza kuwaangazia wachezaji wazawa ambao wanaweza kuichezea timu hiyo kwa mafanikio mazuri endapo watapewa nafasi.

Zahoro Pazzi – Mbeya City

Huyu bado ni mchezaji mzuri sana na gharama zake ni nafuu . Anakupa vitu viwili kwa wakati mmoja katika eneo la ushambuliaji.

Zahoro anaweza kucheza kama mshambuliaji kiongozi kati lakini pia kutokana na uwezo wake wa kukaa na mpira , kukokota na kutoa pasi nzuri za mwisho , anaweza kutumika kama mshambuliaji namba mbili ( false 9/playmaker ).

Ni rahisi sana kimbinu kutengeneza kombinesheni ya Zahoro na Niyonzima kati kuliko Mahadhi na Niyonzima lakini utakuwa na faida pia ukimtoa Mahadhi wing ya kulia , Haruna akisimama nane na Zahoro 10 !.

Mrudishe Mrisho Ngasa ukikosa fedha za kusajili ‘ pro ‘ mwenye uwezo mkubwa nje . Ningependa zaidi kuona nafasi ya ushambuliaji Yanga wanapata mtu kama Kipre Tcheche lakini kama unakosa fedha basi mrudishe nyumbani Ngasa bado ana uwezo kukuchukulia kombe la ligi ukiwa na mechi 4 mkononi .

Himidi Mao Mkami kiungo wa Azam FC . Mkataba wake na Azam unakwisha mwezi wa kumi , ni mchezaji sahihi mzawa kukamata dimba la kati au Babu Ali wa Kagera Sugar ambaye hakupata sana nafasi msimu huu kutokana na rotation za Mexime lakini bado ni bora kuliko Makapu.

Asanteni sana
Wenu katika soka
Samuel Samuel
0624006257

 

One Comment

  1. Shomari o w missima

    June 26, 2017 at 7:59 pm

    Mimi ni Shomari khalfan umri wangu miaka 10 naipenda sana Timu yangu ya Yang Africa ingawa Baba yangu ni mpinzani. Maoni yangu ni kwamba viongozi wetu muwe makini katika usajili wa msimu huu ili kuwaonesha hao masimba kwamba tunaweza h
    ata bila nguvu kubwa ya manji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *