Unamuelewa Saimon Msuva?

Saimoni Msuva ni mmoja wa wachezaji ambao kabla ya kufanikiwa kutoka nje ya mipaka ya nchi hii, wengi walimpigia kelele kuwa anachelewa kuianza safari ya soka lake ngazi ya kimataifa. Ubora wake kama winga na mshambuliaji wa pembeni uliwafanya wadau wengi wa soka nchini kuamini muda wa mchezaji huyo kutoka nje ya nchi umefika.

Kila safari ina mengi ya kupitia yenye kukutia moyo kwenda mbele au kukatisha tamaa kuifikia tamati kikubwa ni uwezo binafsi wa kupambana na mazingira yanayokuzunguka ili kutimiza lengo.

Safari ya Msuva kuivuka mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenda nje haikuwa rahisi. Ilikuwa safari ya kadhia na udhia. Kuna wakati alionekana si chochote si lolote mbele ya umma wa wadau wa soka nchini hususani wapenzi wa Yanga SC klabu aliyojiunga nayo mwaka 2012 akitokea Moro United na hii ilitokana na nyakati ngumu kwake za kutimiza majukumu yake uwanjani na ukinzani wa wadau wenye nyoyo nyepesi. Imani ya kufanikiwa, nidhamu ya asili, usikivu, juhudi na tamaa ya kujifunza ili kuitengeneza kesho yenye amani , furaha na maendeleo katika soka lake ndizo zilikuwa silaha zake kukinzana na umma huo.

Dhima yangu kuu si kuielezea safari ya kiungo huyu toka Yanga hadi alipotua Difaa Al Jadida nchini Morocco bali ni kile anachokifanya sasa ambacho kwa namna moja ama nyingine kina akisi ukomavu wake kisoka na kutoa somo kubwa kwa wadau wa soka nchini, vijana wanaochupikia katika soka, wachezaji waliopo sasa ndani na nje ya nchi .

Saimoni Msuva baada ya dili lake la kuuzwa na Yanga SC kwenda Al Jadida kufanikiwa mapema mwanzoni mwa msimu huu kisoka 2017-18, alijongea mazoezini kuwaaga wachezaji wenzake wa Yanga SC waliokuwa wakifanya mazoezi uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam. Hapa Msuva alikwenda kufanya vitu vitatu kwa wakati mmoja . Kwanza kabisa ni kutambua mchango wa wenzake uliomwezesha yeye kufanikiwa kuwa bora katika kipaji chake mpaka timu hiyo kumuona na kukubali kumnunua. Pili ni kuwapa ujumbe wenzake jitihada na nidhamu ndani ya uwanja na nje ya uwanja ndio silaha ya kukinzana na mashabiki wenye nyoyo nyepesi kurusha lawama kwa wachezaji. Wamtazame yeye kama kioo cha wao kutimiza malengo yao . Mwisho ni kutimiza nguzo ya upendo kwa wengine.

Tukio la pili kwa Saimoni Msuva ni kutambua kila jitihada za mwanadamu katika jambo lolote alifanyalo ni lazima kujiweka sawa na masuala ya kiimani ili mwenyezi Mungu aweze kubariki kazi yako au jitihada zako. Msuva alikwenda kanisani na kutoa shukrani kwa mchungaji wake ambaye binafsi alikiri amekuwa msaada mkubwa kwake kiroho kumjenga katika imani ya kupambana , imani ya kutokata tamaa katika lolote alitendalo kwa haki na lenye kibali mbele za Mungu. Hapa anatoa somo kwa wenzake kwa imani zao wasiache kumtegemea Mungu.

Tumeziona jitihada za kiungo huyu akiwa na klabu yake mpya nchini Morocco. Baada ya mwezi mmoja tu yaani kutoka mwezi wa nane mpaka mwezi wa tisa, alifanikiwa kuwa mchezaji bora wa mwezi katika klabu mpya tena akiwa ugenini Afrika kaskazini. Hii ni kwa sababu aliondoka nchini kwa baraka pande zote kwa wapenzi wa soka na Mungu wake lakini pia akiweka jitihada ili kusimamia lengo la ubora .

Msuva kabla ya kutejea nchini kwa mapumziko mafupi aliibuka kama kinara wa kutupia magoli katika klabu yake jambo ambalo lilizidi kumfanya kuwa bora na tegemeo katika kikosi cha Al Jadida.

Baraka Kizuguto aliyewahi kuwa afisa habari wa Yanga SC na baadae TMS meneja TFF ni mmoja wa washauri wakubwa wa mchezaji huyu ambaye hakuwahi kujiweka hadharani kwa namna yoyote lakini Saimoni Msuva baada ya kutua nchini aliamua kuujuza umma kuwa nyuma ya pazia lake la mafanikio kiasi aliyopata mpaka sasa kuna watu ambao walimwezesha kusogea hatua moja mbele. Wapo wengi sana lakini Kizuguto alivaa jezi ya mchezaji huyo kuwakilisha mamia ambao kwa namna moja ama nyingine walichangia na wanachangia kumwezesha kuwa bora katika kazi yake .

Kubwa kuliko yote ambalo limenivutia kuandika waraka huu , ni tukio alilolifanya jumatano tarehe 10, Januari 2018 katika kituo cha Wakati Ujao Youth Academy. Ni kituo cha watoto Yatima ambao mbali na malezi mengine lakini pia wanafundishwa soka kama kipaji cha kuwakomboa baadae ( wakati ujao ) .

Saimoni Msuva mbali na zawadi zingine alizotoa kituoni hapo kama msaada kupunguza makali ya gharama za kuendesha kituo hiko, alitoa jezi za timu yake ya Difaa Al jadida kwa timu ya kituo hicho kama zawadi na hamasa kwao ili wacheze kwa moyo wakiwa na imani ya kufanikiwa kisoka hapo baadae.

Naitazama zawadi ya jezi hizo kama mbegu ya mafanikio kwa watoto hao na vijana wanaochipukia katika soka nchini. Wakati wowote watoto hao watakapokuwa wanavaa jezi hizo nyoyoni mwao watajipa tumaini la kufanikiwa kucheza mpira katika kiwango kizuri na mwisho wa siku kwenda mbali katika uga wa soka la kulipwa . Hapo Msuva atakuwa kwa namna moja ama nyingine ameshiriki kujenga kizazi bora kijao cha soka nchini.

Si kwamba Msuva anapenda sifa au ana uwezo mkubwa kifedha kwa haya anayofanya . Ni moyo na uzalendo kwanza katika tasnia ya soka pili kwa nchi yake na mwisho ni moyo mpana wa shukrani kwa kila hatua .

Dini zote zinahubiri katika upendo na kujaliana kama ndugu . Msuva anatimiza hili kwa vitendo. Upendo kwa soka letu , nchi na jamii zenye mahitaji maalumu. Ni jambo ambalo kwa kila public figure ambaye kwa namna moja ama nyingine amepiga hatua moja mbele ageuke nyuma kuwatizama wengine.

Si lazima utoe fedha zako mfukoni lakini unaweza kutumia ushawishi wako katika jamiii kusaidia wengine na mwisho wa siku Mungu kukuzidishia baraka.

Tumtizame Saimoni Msuva kama kioo cha uzalendo, upendo na moyo wa shukrani kwa wengine .

By Samuel Samuel

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *