Uchambuzi wa kikosi cha Yanga dhidi ya Stand United

Kikosi cha Yanga kinatarajiwa kushuka dimbani muda mchache ujao kuwania pointi tatu dhidi ya Stand United kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Kikosi cha kocha George Lwandamina hii leo kimeonekana kuwa na mabadiliko kwenye eneo lake la ulinzi kwa kuwaanzisha Hassan Kessy kwenye eneo la ulinzi wa kulia akichukua nafasi ya Juma Abdul.

Katika eneo la ulinzi wa kati, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ atacheza na Andrew Vincent, Cannavaro amechukua nafasi ya Kelvin Yondani aliyekuwa mhimili mkubwa wa Yanga kwenye eneo hilo tangu kuanza kwa msimu huu.

Mabadiliko hayo yametokana na ukweli kwamba, Lwandamina ameamua kuwapumzisha wachezaji hao kwa ajili ya pambano la watani wa jadi wikiendi ijayo, hii ni kufuatia kwamba nyota hao kila mmoja ameoneshwa kadi mbili za njano hivyo kwenye mchezo wa leo wameepushwa kupata kadi za tatu endapo ingetokea kuoneshwa ambazo zingewaondoa moja kwa moja kwenye mchezo dhidi ya Simba.

Youthe Rostand anaendelea kusimama kwenye lango la Yanga, Pato Ngonyani, Pius Buswita na Papy Kabamba wanatarajiwa kusimama kama viungo watatu kwenye eneo la katikati mwa uwanja wenye majukumu ya kuhakikisha timu inatengeneza mashambulizi na kulinda kwa ujumla.

Obrey Chirwa, Ibrahim Ajib na Godfrey Mwashiuya ndio watakaokamilisha idadi ya washambuliaji watatu wengine kwenye mfumo wa 4-3-3 atakaoingia nao Lwandamina kwenye mchezo huo.

Lakini Obrey Chirwa anatarajiwa kuwa ndie mshambuliaji wa kati mwenye majukumu ya kufunga kutokea kati huku Ajib na Mwashiuya wakitokea pembeni.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *