Tathmini: Mwadui v Azam

Mwadui watawakuwa wenyeji wa Azam kwenye pambano la mzunguko wa tatu wa Ligi Kuu Vodacom Tanzania Bara litakalochezwa siku ya Jumapili kwenye uwanja wa Mwadui.


Pambano hili ni mtihani kwa timu zote mbili. Kocha Julio Kihwelo anapaswa kushinda mechi hii kudhihirisha maneno yake mengi kwenye vyombo vya habari si kelele za bure.

Kikosi cha Mwadui kimesheheni wachezaji wengi wazoefu wanaoijua vyema ligi Kuu Vodacom Tanzania, Bara jambo linalomfanya kocha Julio Kihwelo atambe kuwa watafanya vizuri na kuwa moja ya timu zinazowania ubingwa msimu huu.

Sare ya mabao 1-1 kwenye mchezo wa kirafiki mwezi uliopita ni sababu nyingine inayoongeza mvuto kwenye pambano hili.

Katika mechi ya ufunguzi Mwadui walilizwa na Toto Africans 1-0 kabla ya kuwazibua kwa mabao 2-0 wageni wenzao wa Ligi Kuu, African Sports siku ya Jumatano na kujiandikishia alama zao tatu za kwanza.

Mshambuliaji wa Taifa Stars aliyesajiliwa kutoka Kagera Sugar, Rashid Mandawa pamoja na mfungaji bora wa msimu uliopita wa Ligi Daraja la Kwanza, Kelvin Sabato wanatarajiwa kuongoza safu ya ushambuliaji ya Mwadui.

Kwa upande wa Azam, alama tatu ni muhimu hasa ukizingatia ushindani baina yao na Yanga na Simba unaonekana kuwa mkali Zaidi msimu huu. Japo msimu bado ni mchanga lakini Azam wanajua mbio za ubingwa zishaanza, kutetereka kokote kule ni kutoa mwanya kwa wapinzani wao.

Bila shaka kipa wa Coastal union, Shaban Kado, atakuwa anajiandaa kukabiliana na heka heka za Kipre Tchetche au John Bocco. Mkenya Allan Wanga aliyefungua kitabu chake cha mabao anaweza kuendelea kuaminiwa na kocha Stewart Hall.

Kikosi cha Azam kilichoinyuka Stand United mabao 2-0 : Aishi Manula, Aggrey Morris, Pascal Wawa, David Mwantika, Erasto Nyoni, Abubakar Salum, Farid Mussa ( Gadiel Mbaga 60’) , Jean Mugiraneza, Frank Domayo, John Bocco (Nahodha), Allan Wanga ( Kipre Tchetche 60’).

Mechi Za Ligi kuu ya Vodacom Jumapili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *