Tathimini ya mchezo kati ya Yanga dhidi ya St Louis

Michuano ya klabu bingwa Afrika imeanza kutimua vumbi barani Afrika kwa michezo mbalimbali kupigwa katika viwanja mbalimbali. Tanzania bara walikuwa wenyeji kwa mchezo kati ya mabingwa wa Tanzania Yanga SC dhidi ya mabingwa wa visiwa vya Ushelisheli mchezo uliomalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi mwepesi wa 1-0.

Goli la Yanga lilifungwa dakika ya 67 ya mchezo na winga wake Juma Mahadhi dakika moja baada ya kuingia uwanjani akitokea benchi.

Tuitazame Yanga kwa uchache katika mchezo wa leo na mustakabali wake katika michuano hii mikubwa kabisa barani Afrika. Hii ni tathimini fupi ya ushiriki wa kila mchezaji katika mchezo wa leo na timu kwa ujumla wake.

1. Ramadhani Kabwili

Ameingia kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga kama golikipa namba moja baada ya Youthe Rostand kukosa leseni ya ushiriki katika mashindano huku Beno Kakolanya akiwa na majeruhi kidogo aliyoyapata mazoezini mkoani Iringa ingawa alipangwa kama kipa wa akiba.

Michezo miwili ya ligi aliyopata kucheza Kabwili dhidi ya Lipuli na Njombe mji alionesha kiwango kizuri na kuwavutia wengi kitu ambacho kimechangia kwa kiasi kikubwa kuaminiwa leo langoni.

Leo Ramadhani Kabwili aliweza kuonesha kiwango chake lakini kiuhalisia michuano hii imeonesha ni mikubwa kwake na anahitajika kuwa chini ya mtu ili ajifunze zaidi. Ameonesha kukosa umakini hususani kwenye mashambulizi ya kushitukiza na uwezo wa kupangua mipira nje ya 18.

Kama St. Loius wangekuwa makini makosa yake mawili yangeigharimu timu. Majeruhi ya Beno na kukosa leseni kwa Youthe kunalilazimisha benchi la ufundi kuendelea kumtumia kinda huyu. Kwenye mechi ya marudiano anahitaji umakini mkubwa kwa akili yake kuwa mchezoni . Walinzi wa Yanga wanahitajika kumlinda vyema kufuta makosa yake .

2. Hassani Kessy

St. Loius waliingia na mfumo wa 4-5-1 wakitumia muda mwingi kujilinda hali ambayo iliwafanya walinzi wa pembeni wa Yanga kupanda juu kusaidia mashambulizi kwa kutengeneza krosi za pembi ili kutoa msaada kwa viungo wa kati kufumua ngome ya washelisheli hao.

Kessy alikuwa bora kwenye marking licha ya kukosa pressure kubwa lakini alionesha uwezo mzuri kwenye kupandisha timu. Uwezo binafsi dakika ya 37 uliwawezesha Yanga kupata penati baada ya kuamua kuipasua ngome ya St. Loius kwa chenga zake baada ya kuona krosi zote hazizai matunda.

Tatizo kubwa la Kessy ni kutoa krosi ambazo hazina macho kwa maana ya kumfikia mtu husika . Nyingi zinapita juu sana zikiwa sharp. Anahitajika kutengeneza krosi ( volleys ) ambazo zinawafikia wahusika au kuweka mpira chini kwenye edge kutafuta ‘ V’ pasi kwa washambuliaji wa kati. St. Loius wana makosa mengi kwenye marking endapo walinzi na mawinga wa pembeni wakiongeza kasi ya mashambulizi wataobgeza idadi ya wao kufanya makosa na wao kujipatia nafasi ya kuwaadhibu.

3. Gadiel Michael

Tofauti na mechi kadhaa za ligi kuu ambazo alisimama kama msaada mkubwa kwenye kusaidia mashambulizi, leo Gadiel hakuwa vyema sana kwenye kuipasua ngome ya St. Louis kwa pembeni.

Muda mwingi alikuwa akipiga back passes au kupiga krosi zisizo na macho au kukaa muda mrefu na mpira na mwisho wa siku kushindwa kuachia mpira katika mwendelezo wa kujenga mashambulizi. Ukiondoa hilo bado ni mchezaji sahihi kama beki wa kushoto kwa majukumu ya awali ya ulinzi.

4. Juma Saidi ‘ Makapu ‘

Anaendelea kuonesha ubora wake katika nafasi hii mpya kama mlinzi wa kati. Kiasilia Makapu ni kiungo mkabaji lakini benchi la ufundi la Yanga kuanzia katika michuano ya kombe la Mapinduzi wamekuwa wakimtumia katika nafasi hii kutokana majeruhi ya Shahibu na Andrew Vincent pia Nadir umri ukianza kumtupa mkono. Makapu leo kwa kiasi fulani walikuwa na kombinesheni nzuri na mwenzake Kelvin Yondani kama walinzi wa kati.

Aliweza kuwazuia vyema St. Loius kwenye direct play kwa kutumia viungo na washambuliaji wa kati, kuanzisha mashambulizi hususani katika kupiga mipira pembeni au long balls. Bado ana tatizo kubwa la kushindwa kuondoa mipira nyuma kwa wakati ( clearance ) na hii inatokana na mentality ya kucheza kama kiungo nafasi hiyo. St. loius si wazuri sana kwenye pressing lakini Yanga ikikutana na timu nyingine ni hatari.

5. Kelvin Yondani

Naweza sema ni kama ajuza anazeeka na uzuri wake. Yondani ni mmoja kati ya wachezaji wa Yanga ambao wamegusa sana mpira leo licha ya kucheza kama ‘ centre half ‘. Kupwaya kwa viungo Ibrahim Ajibu na Rafael Daudi kuliwapa nafasi St. Loius ambao walikuwa wanatumia viungo watano mpaka sita eneo la kati kumiliki mpira pia kuizuia Yanga kwenda mbele kasi katika njia ya kati.

Yondani mara kadhaa alikuwa akipanda juu kusaidia kusukuma timu mbele kwa mashuti yake na pasi ndefu. Almanusura dakika ya 49 Yanga wapate goli alipoachia mkwaju mrefu na kumkuta kipa wa St. loius mikononi mwake. Upande wa ulinzi yakiwa majukumu yake ya awali aliweza vyema kuyatekeleza pia kufuta makosa Makapu kam Ribelo.

6. Paapy Tshishimbi

Ameibuka kama ‘ man of the match ‘ . Amestahili kuibuka bora kutokana na kazi kubwa aliyoifanya uwanjani leo. Yanga wameingia uwanjani kwa mfumo wa 4-2-1-3. Tshishimbi na Rafael Daudi ndio waliopangwa kucheza kati na juu yao asimame Ibrahimu Ajibu huku kulia akiwepo Pius Buswita na kushoto Emanuel Martin.

Mechi ilipoanza mfumo mzima uliharibika na kujikuta timu ikicheza bila patterns za maana za mashambulizi zaidi ya wachezaji kucheza wanavyojua wao na hii ilitokana na Ibrahimu Ajibu na Rafael Daudi kuvuruga pattern nzima kwa jinsi walivyoanza kucheza nje ya mfumo. Ajibu aliondoka juu na kucheza sana chini hali iliyovunja muunganiko wao wa kati ba Tshishimbi pia Rafael Daudi kitu ambacho kilimfanya Chirwa juu kukosa mipira mizuri ya mwisho.

Daudi yeye alikosa kasi na muda mwingi kujikuta katikati ya viungo wa St. loius. Hii ilimfanya Tshishimbi sasa kucheza ‘ double pivot ‘ kwa maana ya kusimamia ulinzi wa timu, kuvunja mipango ya wapinzani wao pia kusaidia mashambulizi kwa kukataa Chirwa kushuka sana chini na ndio maana hata goli lilitokana na pressure yake kabla ya Mahadhi kufunga .

7. Piusi Buswita

Licha ya kukosa kasi kama winga wa pembeni lakini ameonesha mchezo mzuri kama kiungo wa pembeni. Ni mechi ya kwanza klabu bingwa Afrika hivyo mchezo wa marudiano akipata nafasi anaweza kuwa bora hususani katika kuongeza kasi ya mashambulizi ya pembeni.

8. Rafael Daudi Loth

Ni mchezo wa kwanza klabu bingwa Afrika akipangwa kama kiungo mchezeshaji acheze pacha na Tshishimbi. Rafael mchezo umemkataa kuanzia dakika ya kwanza hadi ya mwisho kwa maana nzima ya kuisadia timu kujenga mashambulizi mazuri kuanzia kati. Muda mwingi alikuwa akikubali kukabika pia akiwa na mpira hakuwa na madhara kwa maana ya kucheza taratibu sana hali ambayo ilivunja tempo na chemistry ya timu.

9. Obrey Chirwa

Ni kama bahati haikuwa upande wake. Alipangwa kama mshambuliaji wa kati akicheza na Ibrahimu Ajibu lakini muda mwingi alionesha pressure ya kutafuta goli hali iliyomnyima umakini kwenye finishing. Pressure hiyo ilimfanya kukosa penati dakika ya 37 ya mchezo baada ya Hassani Kessy kufanyiwa madhambi.

Bado ni mchezaji mzuri endapo anakuwa na utulivu pia timu ikiwa katika tempo nzuri. Bado ni tishio kwa St. Loius kutokana na uwezo wake wa kufunga kwa maana ya kumalizia pasi za mwisho pia kujitengenezea nafasi ya kufunga kwa maarifa na nguvu zake .

10. Ibrahim Ajibu

Alipangwa kama mshambuliaji namba mbili kwa Obrey Chirwa lakini kutokana na kutokuwa vyema kiafya kwa kutoka katika majeruhi ya kuuguza goti lake aliondoka nafasi hiyo na kucheza chini zaidi ili kuepuka pressure ya viungo na walinzi hali ambayo ingweza kumtonesha.

Kosa lililofanyika ni wakati yeye anafanya switching ya position ilimpasa Rafael Daudi kupanda juu nafasi yake na yeye kusimama na Tshishimbi akicheza kama kiungo huru ili kuisaidia timu kwenye umiliki wa mpira hususani katika mipango ya kuanzisha mashambulizi tokea chini. Rafael hakung’amua mipango ya Ajibu pia benchi la ufundi na kuifanya timu kukatika kati.

Mabadiliko ya kumtoa Ajibu nje kumwingiza Mahadhi na Mwashiuya kuliirudisha timu kwenye game plan hii licha ya mabadiliko hayo kuchelewa kufanyika .

11. Emanuel Martin

Dakika 20 za mwanzo alikuwa vyema kama winga wa kushoto lakini baadae alipotea hususani St. Loius walipoamua kuua forwad line yao na kujaa nyuma wakiufinya uwanja mbele ya lango lao. Ni kama ana tatizo pa pumzi kubaki katika kasi yake dakika zote 90.

Akiongeza kasi na kucheza kama kiungo mshambuliaji wa pembeni anaevunjikia kati anaweza kuipa Yanga magoli au kuwatengenezea wenzake mipira mizuri.

WALIOINGIA

1. Juma Mahadhi

Ameendelea kuonesha ubora wa kiwango chake kama kiungo na winga wa pembeni. Zilimchukua sekunde 60 kusahihisha makosa ya wenzake katika kutumia nafasi walizokuwa wakizitengeneza kwa kufunga goli pekee.

Aliongeza kasi ya mashambulizi lakini ana tatizo la kukaa na mpira muda mrefu ( too much dribbling ) pia bado krosi zake hazina macho. Akirekebisha makosa yake mazoezini Lwandamina hana budi mechi ijayo kumwazisha ili Buswita acheze kati na Chirwa kama Ajibu atakuwa bado hajapona kwa asilimia 100 na Rafael Daudi kuanzia nje.

2. Yusufu Mhilu

Licha ya kuingia lakini hakuwa na impact kubwa kimbinu. Anahitaji muda zaidi kudhihirisha ubora wake katika kikosi cha Yanga . Hana kasi kama kiungo.

3. Mwashiuya

Kuingia kwake kulileta uhai kwenye wing ya kushoto. Kasi na krosi zake ziliwarudisha nyuma St. loius ambao mwishoni walionesha nia ya kutafuta goli.

By Samuel Samuel

One Comment

  1. Pingback: Tathimini ya mchezo kati ya Yanga dhidi ya St Louis

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *