Singano kulikoni? mbona kimyakimya?

Singano_01

Tulidhani amepotea. Tulidhani amekosea njia. Tulikuwa sahihi ingawa haikuwa kweli. Tulikuwa sahihi kwa maana ya uhalisia wa soka la Azam FC linaloongozwa na mfumo wa 3-5-2 usiopendwa na wengi. Usahihi wetu ulitokana na namna alivyo Ramadhan Singano ‘Messi’ kwa maana ya mchezaji anayecheza pembeni.

Hakuwa na uwezo wa kukaba, akili yake iliathiriwa na ushambuliaji pekee na hakukuwa na njia ya kuyaruhusu mawazo ya kwamba huenda angeweza siku moja kupenya kirahisi.

Si nyinyi tu mliodhani ilikuwa hivyo, hata baadhi ya nyota waliopita waliwahi kuwaza kitu kama hicho. Wakati kila mmoja akiwaza hivyo, Stewart Hall alikuwa akikuna kichwa chake kuangalia njia sahihi ya kumfanya aingie kwenye mfumo wake. Naanza kumuelewa kidogo kidogo Stewart Hall lugha anayoizungumza.

Singano_02

Fikiria namna Singano alivyo na miguu myembamba iliyoundwa na chembechembe ngumu zenye kipaji cha hali ya juu kwenye kuuchezea mpira. Ndivyo ilivyokuwa kwenye mchezo wa Jana dhidi ya Esperance. Mbali na kucheza mpira wa ‘kideo’ kuna namna nyingine ambayo amezidi kuongezeka ubora kwenye kiwango chake. Wasiwasi wangu ulikuwa kazi bure. Kocha wake anajua jinsi anavyofanya kazi aliyomtuma dimbani.

Ni nadra sana kwenye kipindi kama hiki kumuona mchezaji akipotea na kurudi kama awali. Sote ni mashahidi juu ya uwezo wa kupachika mabao aliozaliwa nao Malimi Busungu na Paul Nonga. Sote mashahidi juu ya kipaji cha Joseph Kimwaga na Peter Mwalyanzi. Lakini upepo umebadili uwezo wao. Sijui ni bahati au ni nini lakini siamini katika bahati. Ninaamini kwenye ubora na ndiyo unaompambanua Singano kutoka kwenye kundi la kina Simon Msuva.

 

Niazime macho ya akili yako uweze kuona ukweli huu usioonekana kwa mboni za kawaida. Kuna namna ambayo wanandinga wetu wanakosa kujifunza. Ajabu unatumia muda mwingi kubuni mtindo wa nywele ili uishi kwa vituko kuliko kutumia muda vizuri kuwaza kwanini Nwankwo Kanu pamoja na kusahaulika kwa siku nyingi dimbani amekuwa balozi wa Startimes Afrika. Dunia inamtambua Mario Balottelli kwa vituko zaidi licha ya kuwa na kipaji kisicholandana hata kidogo na Marcus Rashford. Singano amekuja kimyakimya mpaka najiuliza kulikoni imekuwa hivyo.

Nakiri moyo usiokata tamaa hauwezi kuishiwa na mbinu za kujifunza. Heko Ramadhan Singano. Mapambano bado yanaendelea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *