Simba na Yanga nje ya Ligi Kuu

Timu ya Simba imeweka historia nyingine, ilipowachapa mahasimu wao wa jadi Yanga kwa mikwaju ya penalti 4-2 kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi katika pambano lililochezwa Jumanne usiku kwenye Uwanja wa Amaan.

Hiyo inakuwa ni mechi ya 23 kwa timu hizo kukutana nje ya Ligi Kuu Tanzania Bara. Hizi ni baadhi ya mechi ambazo Simba na Yanga zimekutana kwenye michuano mbalimbali nje ya Ligi Kuu au ya Muungano, bali makombe mengine, ikiwemo mechi ya kirafiki.

Kombe la Mapinduzi

1 Simba 2-0 Yanga (2011)

Ilikuwa ni mechi nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi kama ilivyokuwa mechi ya jana. Mechi hiyo ilichezwa Januari 12, 2011. Simba ilishinda mabao 2-0, yaliyofungwa na Mussa Hassan Mgosi dakika ya 33, na Shija Mkina dakika ya 71.

2. Simba 4-2 Yanga (2017)


Method Mwanjali na Amissi Tambwe wakiwania mpira ulio juu

Method Mwanjali na Amissi Tambwe wakiwania mpira ulio juu


Hii ni mechi iliyochezwa Jumanne usiku kwenye Uwanja wa Amaan mjini Zanzibar, Januari 10, na Simba kuifunga Yanga kwa penalti 4-2, baada ya kutoka sare ya bila kufungana kwa dakika 90.

Jonas Mkude, Daniel Agyei, Mzamiru Yassin na Janvier Bokungu, wakifunga penalti zao, Methold Mwanjale akikosa, huku upande wa Yanga, Simon Msuva na Thabani Kamusoko wakipata penalti zao, lakini Haji Mwinyi na Deogratius Munishi Dida wakikosa.

Kombe la Kagame

3. Yanga 2-0 Simba (1975)

Ilikuwa ni mwaka 1995, Yanga ilipotwaa Kombe la Kagame kwa kuifunga Simba mabao 2-0, kwenye Uwanja wa Amaan mjini Zanzibar wakati huo likiitwa Kombe la Afrika Mashariki na Kati.
Katika mechi hiyo ya fainali, magoli yalifungwa na marehemu Gibson Sembuli na Sunday Manara.

4. Simba 5-4 Yanga (1992)

Simba ilifanikiwa kutwaa Kombe la Afrika Mashariki na Kati au Kagame Cup linavyojulikana kwa sasa, ilipoifunga Yanga kwa mikwaju ya penalti 5-4. Ni baada ya sare ya bao 1-1.

Mechi ilichezwa pale pale, Zanzibar, Uwanja wa Amaan.

5. Simba ilipata ushindi wa chee (2008)

Simba ilipata ushindi wa chee kwenye Kombe la Kagame mwaka 2008, baada ya Yanga kushindwa kutokea kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Simba ilipewa ushindi wa tatu wa michuano hiyo, Julai 27 baada ya wapinzani wao kushindwa kufika.

6. Yanga 1-0 Simba (2011)

Ilikuwa ni Julai 10, Yanga ilipoichapa Simba bao 1-0 kwenye mechi ya fainali Kombe la Kagame mwaka 2011. Lilikuwa ni bao pekee la Mghana Kenneth Asamoah, dakika ya 108, Uwanja wa Taifa.

Kombe la Hedex

7. Yanga 2-0 Simba (1996)

Mechi ilichezwa CCM Kirumba, Mwanza, Yanga ikishinda mabao 2-0, ikiwa ni Kombe la Hedex iliyochezwa Juni 30, 1996. Ni mabao ya Bakari Malima na Edibily Lunyamila.

8. Simba 1-1 Yanga (1996)

Mechi nyingine ya kombe hilo iklichezwa jijini Dar es Salaam, ikiwa ni ya marudiano. Ilikuwa ni Julai 13 kwenye Uwanja wa Uhuru. Bakari Malima aliifungia Yanga, Hussein Masha akiifungia Simba.

Kombe la Tusker

9. Simba 5-4 Yanga (2001)

Simba iliifunga Yanga kwenye michuano ya Kombe la Tusker kwa mikwaju ya penalti 5-4 kwenye Uwanja wa Uhuru, baada ya kutoka sare ya bila kufungana, Februari 10, 2001.

10. Simba 4-1 Yanga (2002)

Machi 31, 2002, Simba iliichakaza Yanga mabao 4-1 kwenye michuano hiyo, iliyofanyoka Uwanja wa Uhuru.
Mark Sirengo, na Emmanuel Gabriel wakiifungia Simba, Madaraka Selemeni akifunga magoli mawili. Sekilojo Chambua aliifungia Yanga goli la kufutia machozi.

 

11. Simba 2-0 Yanga (2005)

Simba iliendelea kuitesa Yanga kwenye michuano hiyo, baada ya kuichapa mabao 2-0 kwenye mechi ya fainali Julai 2, 2005, Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza. Ni magoli ya Emmanuel Gabriel na Mussa Hassan Mgosi.

 

12. Simba 7-6 Yanga (2006)

Hapa Simba na Yanga zilikutana kwenye hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo ya Tusker. Simba ilifanikiwa kutinga fainali kwa kuifunga Yanga kwa mikwaju ya penalti 7-6, baada ya sare ya bao 1-1 kwa dakika 120.
Emmanuel Gabriel akiifungia Simba, Credo Mwaipopo akiifungia Yanga, Agosti 15, 2006.

13. Yanga 2-1 Simba (2009)

Ilikuwa ni nusu fainali nyingine iliochezwa Desemba 25, Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Yanga ilifanikiwa kushinda mabao 2-1, yaliyofungwa na Jerry Tegete na Shamte Ally, Hillary Echessa akiifungia Simba.

Kombe la AICC

14. Yanga 1-0 Simba (1989)

Kombe la AICC ni moja kati ya michuano iliyovuma sana miaka ya ’80. Simba na Yanga zilikutana Juni, 1989 na Yanga kushinda bao 1-0, lililofungwa na Joseph Machela.

Mechi ya kirafiki

15. Yanga 3-0 Simba (2003)

Yanga iliichakaza Simba mabao 3-0, Aprili 20, 2003 kwenye mechi pekee ya kirafiki ya watani wa jadi. Wafungaji walikuwa ni Kudra Omari, Heri Morris na Salum Athumani. Mechi ilichezwa CCM Kirumba, Mwanza.

Kombe la CCM

16. Simba 1-1 Yanga (2003)

Kombe la CCM nalo lilikuwa moja kati ya michuano maarufu sana miaka ya ’80 hadi mwanzoni mwa 2000.
Simba na Yanga zilikutana kwenye michuano hii, Januari 19, 2003 na kutoka sare ya bao 1-1.
Shengo Tondolo aliifungia Simba, huku Rajab Mwinyi akiifungia Yanga.

Ngao ya Jamii

17. Yanga 2-1 Simba (2001)

Hii ni michuano ambayo huchezwa kwa ajili ya kuashiria kuanza kwa msimu mpya ya ligi.
Februari 17, 2001, Yanga iliichapa Simba mabao 2-1, yaliyofungwa na Edibily Lunyamila na Ally Yusuph ‘Tigana’, huku Steven Mapunda ‘Garincha’ akiifungia Simba.

18. Yanga 3-1 Simba (2010)

Yanga iliichapa Simba kwa mikwaju ya penalti 3-1, Agosti 18, 2010 baada ya kutoka sare bila kufungana na kutwaa Ngao ya Jamii kwa mara nyingine.
Penalti za Yanga zilifungwa na Geofrey Bonny, Stefano Mwasika na Issac Boakye, ile ya Simba ikifungwa na Mohamed Banka.

19. Simba 2-0 Yanga (2011)

Ilikuwa Agosti 17, 2011, Simba nayo ikafanikiwa kutwaa Ngao ya Jamii mbele ya Yanga kwa kuichapa mabao 2-0.
Haruna Moshi ‘Boban’ aliifungia Simba bao pamoja na Felix Sunzu.

Kombe la FAT

20. Simba 1-0 Yanga (2000)
Kombe la FAT kwa sasa ndilo linajulikana kama Kombe la FA. Simba iliifunga Yanga bao 1-0 Novemba 12, 2000 kwa bao la marehemu Ben Luoga.

21. Yanga 2-1 Simba (2000)

Novemba 15, 2000 timu hizo zilikutana kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha kwenye mechi ya marududiano na Yanga kushinda mabao 2-1.
Magoli ya washindi yalifungwa na Aziz Hunter na Vicent Tendwa, Ally Yusph ‘Tigana’ akiifungia Simba goli la kufutia machozi.
Matokeo hayo yakafanya matokeo ya jumla kuwa mabao 2-2 na kulazimika kupigiana penalti, Simba ikatwaa kombe la ushindi wa penalti 5-4.

Mtani Jembe

22. Simba 3-1 Yanga (2013)

Ni michuano iliyodumu kwa miaka miwili tu. Ilikuwa inazikutanisha timu hizo tu. Mwaka 2013, Simba iliichapa Yanga mabao 3-1, yaliyofungwa na Amissi Tambwe magoli mawili na Awadh Juma goli moja, huku la kufutia machozi likifungwa na Emmanuel Okwi.

23. Simba 2-0 Yanga (2014)


Juma Awadh akimfunga bao Juma Kaseja

Juma Awadh akimfunga bao Juma Kaseja


Mwaka uliofuata timu hizo zilikutana tena Uwanja wa Taifa na Simba kushinda kwa mara nyingine magoli 2-0 yaliyofungwa na Awadh Juma na Elius Maguri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *