Serikali ya Magufuli, sakata la kodi TFF na TRA

image

Kikosi cha timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 21

Wazee wetu walikita mizizi ya hekima na kustawisha matawi ya busara na kuwa moja kati ya vielelezo vilivyowafanya kuwa kizazi cha dhahabu kwa kizazi cha sasa.

Hekima na busara zao ziliwahi kuzaa usemi unenao “Ukimuona mwenzako ananyolewa, wewe tia maji”.

Tangu serikali mpya ya awamu ya tano, serikali ya Dr. John Pombe Magufuli ichukue madaraka, kina mambo kadha wa kadha yameshika hatamu. Ziara za kushitukiza kwenye sekta mbalimbali, watu kunyolewa kama si kutumbuliwa majipu.

Kashikashi hii, imehamia kwenye sekta ya kabumbu kama si kandanda au soka.

Kimbunga cha serikali ya Mheshimiwa Rais kimevitembelea viunga vya michezo.

Wakati sekta nyingine zikinyolewa, huku kwetu tulihisi tuna nywele za shaba zilizojiotesha kwenye kichwa cha chuma kiasi kwamba hata wembe wa mheshimiwa rais, uliotengenezwa kwa madini ya platinums usingeweza kufua dafu.

La hasha! Tulisahau kwamba mwenzako akinyolewa wewe tia maji.

Licha ya kunyolewa vichwa  vikiwa vikavu, lakini mtego huu wa Dr. Magufuli, utawanasa panya wanaohusika na hata wasiohusika.

Tukumbuke, timu yetu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka kumi na tano(U15), walianza ziara maalum kwa kucheza michezo mbalimbali ya kirafiki ndani na nje ya Tanzania. Yaani Kenya, Uganda na Burundi.

Ziara hii sasa, imeota mbawa, kutokana na kudaiwa kodi ya bilioni 1.6 na mamlaka ya ukusanyaji wa kodi Tanzania(TRA).

Wadau wa soka wanakumbuka wakati serikali hii ikiingia madarakani kilio chetu kilikuwa ni kupunguziwa kodi kwa vifaa vya michezo vinavyotolewa na shirikisho la kandanda ulimwenguni (FIFA), ili vije kutumika kwa maendeleo ya mchezo husika. Taratibu ndoto hizo zinaanza kufifia.

Jamani, maendeleo ya soka hapa Tanzania hayawezi kuja kwa kuwa na TFF pekee, lazima mkono wa serikali uingie kwenye bakuri letu.

Lazima serikali iwe na sura ya michezo, vinginevyo tutaendelea kumlaumu Jamal Malinzi na sekretarieti yake bila kujua kuna kivuli kimewafunika.

Tukiizungumzia, Uganda, michezo imevaa sura ya kitaifa, Tanzania soka limevaa sura ya Jamal Malinzi.

Serikali ya mheshimiwa rais, Magufuli iangalie upya juu ya mustakabali wa kodi kwenye sekta ya michezo. Inawaumiza wengi, wanaohusika na wasio husika.

Vijana wenye ndoto watakuwa wapi kesho muda kama huu? Nakupenda Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *