Said Ndemla, sikiliza sauti inayotoka ndani ya moyo wako

Kiungo wa Simba, Saidi Ndemla. [Picha/Azamtv]

Moyoni mwa mwanadamu yeyote yule kuna sauti hutoka. Sauti hii humtaka mhusika kuifuata kwa kuwa huwa inabeba muongozo wa safari ya mtu katika maisha. Kama kuna kosa kubwa ambalo mtu hulifanya mbele ya sauti hio ni kuiwekea vikwazo, oh! haiwezekani, lakini sijachelewa! Hili ni kosa kubwa, kamwe usiiwekee vikwazo sauti inayotoka ndani ya moyo wako.

Said Ndemla kuna sauti inatoka ndani ya moyo wako, umeisikia? Sauti yenyewe inakutaka kutogeuka nyuma kwani kuzisikiliza sauti zinazosikika zikikupigia kelele. Ni sauti moja tu ambayo tu ambayo kwa sasa unatakiwa kuifuata, nayo ni ile inayotoka ndani ya moyo wako na si ile inayosikika nje ya masikio yako.

Ni moja kati ya vipaji vikubwa sana. Amekuwa sasa hivi na anatosha kucheza soka nje ya Tanzania au mahali popote ambapo atapata nafasi ya kucheza na kukionesha zaidi kipaji chake kuliko kaa kwenye benchi na kutumika kama mpango wa pili kwa kocha, Joseph Omog.

Ndemla yule yule mwenye uwezo wa kuingia na kuonesha uwezo ule ule wa tangu tumeanza kumfahamu akiibukia kwenye kikosi cha Simba cha vijana chini ya umri wa miaka 20, ndie yule yule mwenye uwezo wa kuufanya mpira ugeuke burudani hata mbele ya watu wasioupenda mpira.

Ndemla anakipaji cha kucheza soka nje ya nchi, umri wenyewe ndio huu, kuendelea kukaa benchi kwenye kikosi cha Simba kunapunguza uwezekano wa kuwa bora na tofauti maradufu. Kuendelea kuiwaza Simba kwa sasa hautakua wakati sahihi, kuendelea kutumika kama njia mbadala ya Simba si afya kwa kipaji chake.

Wakati wenyewe ndio huu na hakuna wakati mwingine! Kikosi cha Simba kwa wakati huu licha tu ya presha ya kuhitaji matokeo kinakabiliwa na ushindani mkubwa wa namba. Nafasi anayocheza Said Ndemla inaushindani mkubwa sana kiasi kwamba kocha Joseph Omog akimuangalia usoni Ndemla lazima atakua anawaza tu matokeo na kisha kujisemea moyoni mwake subiri kwanza hapa natafua matokeo ili nilinde ajira yangu.

Hakuna kocha asietamani kuwa na mchezaji mwenye nidhamu kubwa kama Ndemla, hebu angalia muda ambao ameutumia kwenye benchi la Simba, ni muda mrefu sana kiasi kwamba angekua na nidhamu hafifu tusingemuona tena kwenye ulimwengu huu wa mpira wa miguu.

Lakini kila anapoingia kwenye mechi, kitu cha kwanza mchezo wote utafuata mapigo ya miguu yake na kasi ya ajabu ya mwili wake. Eneo lote la kiungo la Simba hubadilika na kuwa la kibunifu zaidi ya awali, mpira hufuata ubunifu wa miguu yake namna ambavyo hujiandaa kupokea mpira, kuupokea na kuanza kuukokota kuelekea kwenye eneo la robo tatu ya mwisho ya uwanja kutokea kwenye lango la timu yake.

Akili nyingi, ubunifu, kasi na nidhamu lakini bado utaendelea kutamani kumuona Said Ndemla kwa jinsi mwili wake mwembamba ulivyojaaliwa kuwa na nguvu miguuni na kuzitumia kupiga mashuti makali ya nje ya boksi. Mashuti yake yamekosa tu ile kitu inaitwa shabaha, mara chache hulenga lango lakini mara nyingi huishia kupaa au kutoka sentimita chache tu langoni mwa mpinzani.

Hakuna shaka kwamba hio husababishwa na namna anavyoendelea kukaa benchi, kuna vitu hupungua kwa mchezaji asipopata mechi nyingi ndani ya msimu. Ndemla ni mchezaji na silahayake ni miguu hivyo kutoitumia ipasavyo hukosa au hupungua uwezo wake wa kawaida.

Kwanini Ndemla anatakiwa kufanya kadri awezavyo kuhakikisha kuwa anafuzu majaribio yake hayo? Kiukweli AFS ESkistuna si sehemu sahihi kwa sasa lakini Simba si sehemu sahihi zaidi kwa afya ya kipaji chake. Kama atafanikiwa kupata nafasi AFC ni bora akaenda huko. Si sehemu sahihi kwa kua si tu timu hio inashuka daraja msimu huu bali nchini Sweden si sehemu inayozalisha wachezaji wengi wanaokwenda kwenye Ligi Kubwa Duniani.

Sharti moja ambalo Ndemla anatakiwa kulifuata kwenye klabu hio endapo atafuzu majaribio yake ni kusaini mkataba wa muda mfupi mno, usiozidi misimu mmoja. Kisha kuhakikisha anavuja jasho mithili ya mlevi anaeipambania pombe yake inayotaka kumwaga.

Said Juma ‘ Makapu’ akikabwa na Said Ndemla

Baada ya mkataba huo kufikia ukingoni, anatakiwa kuhakikisha amepata nafasi kwenda kucheza soka eidha nchini Hispania, Italia, Ubelgiji, auUfaransa. Huku si lazima akaanzia kwenye ngazi kubwa, huko si lazima akacheze kwenye Ligi Daraja Kwanza tu bali hata Daraja la Pili itakua ni sahihi.

Nchini Sweden si mahali ambapo fedha nyingi ataipata, asitegemee hilo. Ni vema kujiandaa kisaikolojia kisha akaitumia AFC kama daraja la kumvusha na kufikia mahali ambapo sauti ya moyoni mwake inahitaji kwenda. Hii si sehemu ambayo Michael Olunga, yule Mkenya msomi alipokaa sana, alichukua muda mfupi tu kisha akaondoka zake na sasa yupo nchini Hispania.

Said Ndemla, usiangalie nyuma, kuondoka ni sahihi zaidi kwa sasa kuliko kuendelea kubaki sehemu ambayo hupati nafasi ya kucheza kwa muda wote, hupati nafasi ya kucheza kwa michezo mingi, naamini Simba watalia sana kupoteza kipaji chenye uwezo wa ajabu lakini ifuate sauti ya moyoni mwako, kamwe usiiwekee vikwazo.

Imeandikwa na Halidi Abdulrahman [Twitter @Halidi97]

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *