Said Mussa Chanda Chema Jangwani

Ni kijana mdogo mwenye uwezo mzuri uwanjani kama winga na kiungo mchezeshaji. Wengi walianza kutambua uwezo wake akiwa na kikosi cha Serengeti Boys hali iliyowafanya mabosi wa Jangwani kwenye benchi la ufundi kutosita kumpandisha timu ya wakubwa.

Katika michuano ya Sportpesa alionesha uwezo mzuri na wengi kumtabiria makubwa endapo benchi la ufundi la Yanga SC chini ya kocha mkuu George Lwandamina hawatasita kumpa nafasi kwenye kikosi chao. Hali ambayo imekwenda kinyume kidogo, maana katika mechi 11 walizocheza wanajangwani hao kinda Saidi Mussa alibahatika kupangwa mechi moja tu dhidi ya Stand United akitokea benchi katika ushindi wa 4-0.

Licha ya kukosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza , kinda huyo ni aina ya wale wachezaji wenye imani pana ‘ ipo siku nitatoka’ hali ambayo inamfanya kuwa na morali , ari na nguvu ya kufanya mazoezi muda wote akiamini ipo siku mwalimu atamwamini na yeye kuonesha kile alichonacho.

Mechi ya jumapili ( jana ) kombe la ASFC dhidi ya Reha FC , Yanga SC walibanwa mbavu na timu hiyo ya ligi daraja la pili kwa takribani ya dakika 84! lakini mabadiliko ya kumtoa Emanuel Martin na kumpa nafasi kinda huyu yalizaa matunda . Yanga ilihitaji mchezaji wa pembeni mwenye kasi, nguvu na uwezo wa kumiliki mpira kitu ambacho kingewafanya Reha FC kutanuka kwenye muhimili wao wa ulinzi uliokuwa imara na ukitunzwa kwa nidhamu ya hali ya juu.

Tayari Reha walishamfanyia hesabu Yusufu Muhilu ambaye licha yakuwa na kasi lakini kila mara walifanikiwa kumtoa relini. Rafael Daudi hakuwa imara sana hali iliyomfanya Tambwe muda mwingi kuwa kama hayupo uwanjani, muunganiko kimbinu ulikataa. Martin alikosa kasi kama tegemeo pembeni, kuingia kwa Saidi Mussa kulileta uhai kwa Yanga na kuwafanya wachezaji kama Tambwe , Buswita , Tshishimbi kuwa vyema kwenye muhimili wa ushambuliaji.

Zilimchukua sekunde 23 tu kuonesha nini Yanga walikuwa wanakikosa alipoingia pale alipokamata mpira na kufanya driving nzuri pembeni iliyozaa kona .

Saidi Mussa almaarufu ‘ Ronaldo ‘ kiasilia ni winga wa kulia mwenye kasi, nguvu na uwezo wa kutoa pasi zenye macho licha ya umri wake mdogo wa miaka 18. Ni wakati wa benchi la ufundi la Yanga SC kumpa nafasi kijana huyu ili aisaidie timu yake yenye tatizo kubwa la wachezaji wenye kasi pembeni ( agility).

Azam FC pia walipandisha takribani wachezaji watano toka timu B akiwemo mshambuliaji Yahya Zayd. Azam wanampa nafasi Zayd na amekuwa bira hali iliyomfanya kuitwa timu ya Kilimanjaro Stars. Ni wakati wa Yanga kutoa fursa kwa akina Saidi Mussa , Maka Edward na golikipa kinda Ramadhani Kabwili.

Uwekezaji katika soka la vijana ndio chachu ya maendeleo ya soka letu ngazi ya vilabu na timu ya taifa. Nchi ina akina Zaydi na Mussa wengu sana tatizo ni mfumo mzuri wa kuwapata , kuwatunza na kuendeleza vipaji vyao.

Njia pekee ya kumwendeleza mchezaji kinda ni kumpa nafasi ya kuonesha kile anachokifanyia mazoezi . Si mbaya vijana hawa kuanza kupewa dakika 25 mpaka 45 ili kupata match fitness and confidence.

Yanga kwa Saidi Mussa ama kwa hakika ni dodo chini ya mpera. Ni wakati muafaka kuanzia mechi 4 zilizobaki za mzunguko wa kwanza ligi kuu na kombe la Mapinduzi kumtumia kinda huyu. Daima chnda chema huvikwa pete !

Merry Christmas and Happy New Year 2018
By Samuel Samuel

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *