Real Madrid na Getafe, mpira unaelea angani

Ligi Kuu nchini Hispania, imejaaliwa kuwa na ubora wa kiwango cha dunia. 

 Real Madrid, chini ya Rafael Benitez imekuwa si ya kufurahisha kama ilivyokuwa chini ya utawala wa Carlo Ancelotti. Haichezi tena mpira unaosisimua mzunguko wa damu bali mara kadhaa huchafua mzunguko mzima wa damu.

Sina maana kwamba haichezi vizuri, la hasha. Bali huwezi kuiweka kikaango kimoja na ile ya Carlo Ancelotti.

Wanakutana na Getafe ambayo imekuwa na homa za vipindi. Wamekuwa hawana muendelezo wa matokeo bora.

Sijui, wataingia na mawazo yapi ila kimwenendo wao ndani ya La Liga hawana meno makali ya kuweza kumtisha Rafael Benitez.

Huku kwake, wanaonekana kuhangaika wanapokutana na timu za kariba yake kuliko timu za katikati mwa msimamo wa La Liga.

Bado sidhani kama mfupa wa Getafe utayashinda meno ya Real Madrid.

Ingawa ndani ya dakika tisini kuna matendo mawili ambayo kila timu huyaishi.

Matendo hayo ni kushambulia na kushambuliwa. Hivyo basi, mwendo wa kinyonga wa Rafael Benitez na homa ya vipindi kwa Getafe, itatengeneza mchezo usiotabirika kirahisi.

Huu ni mchezo unaoweza kuufananisha na mpira wa hewani, yeyote anaweza kuuwania na kuugeuza awezavyo.

Mchezo upo wazi, nadhani utaamuliwa na stadi binafsi za mchezaji na nidhamu ya ufundi wakati matendo mawili yanapochomoza.

Getafe wanahitajika kukaba kwa nafasi wakiwa na maarifa ya kuwatoa washambuliaji wa Real Madrid kwenye reli. Hii ni njia rahisi zaidi kwao hasa linapokuja tendo la kushambuliwa.

Real Madrid hawahitaji njonjo nyingi, njia nzuri kwao kufika kileleni ni kuchimbia mizizi kwenye idara ya kiungo na kuchanua matawi kwenye safu ya ushambuliaji.

Cristiano Ronaldo, James Rodriguez, Karim Benzema, Gareth Bale, Isco, hawa ndio wanandinga wa kuhofiwa sana na Getafe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *