Obrey chirwa, simama wima niyaone matone ya jasho lako

Obrey Chirwa akiwania mpira na William Gallas

Matone ya jasho la mwanaume yana thamani kubwa sana chini ya jua! Siku zote mwili wa mwanaume hauvuji jasho pasipo na kitu cha thamani pia. Hio ndio sababu kubwa ya tone moja la  jasho lichuruzikalo juu ya ngozi ya mwanaume mpambanaji kuwa na thamani kubwa mithili ya kitu kipambaniwacho.

Nina kila sababu ya kumtaka Obrey Chirwa asimame! Asimame kwa miguu yake miwili, kikakamavu na kishupavu pia. Sina haja ya kutaka kumsumbua, najua atakuwa amechoka sana na majukumu ya kuisaidia timu yake kwenye ratiba ngumu saa chache tu zilizopita, hata zile kumbukumbu mbaya za mchezo wenyewe bado hazijafutika. Chirwa simama tafadhali!

Chirwa simama wima nataka nikuone kuanzia miguuni mwako hadi kwenye utosi ili niyaone pia kwa uzuri hayo matone ya jasho lako yalivyoulowanisha mwili wako. Hakika kuna kitu kikubwa cha kujifunza kutoka kwenye mwili wa Chirwa.

Chirwa si mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kuukokota mpira kwa madaha, si mchezaji aliyezaliwa na uwezo wa kuufanya mpira umuheshimu, sijui kumpindua kwa maudhi mpinzani wake au kumdhalilisha kwa chenga zitakazorudiwa mara kwa mara kwenye runinga, hapana, huyu si mchezaji wa aina hio na kwa umri wake hawezi tena kuwa mcheza wa aina hio kamwe!

Chirwa ni aina ya wachezaji wenye shughuli maalum uwanjani, kazi zao huwa hazifanywi sana na wachezaji wenye vitu vingi uwanjani, si kwamba hawapo au hawawezi, hapana! Wapo na wanaweza kuifanya shughuli anayofanya Obrey Chirwa lakini si kiuadilifu kama anavyoifanya mwenyewe na si kiukamilifu kama anavyoipigia hesabu kichwani mwake.

Mwenyewe anaujua fika udhaifu huu, anafahamu fika kuwa hajazaliwa na uwezo wa kuupaka rangi kwa miguu mpira uwanjani sasa afanye nini ili na yeye achomoze mbele ya wachezaji wenye uwezo wa kuufanya watakavyo mpira na kuibua shangwe kila sekunde kwenye majukwaa?

Kabla mpira haujamfikia kwenye miguu yake, akilini mwake huanza kupanga mikakati mujarabu juu ya sehemu sahihi anapotakiwa kuupeleka huo mpira, changamoto kubwa anayokumbana nayo ni pale njiani anapopaswa kupita kuzuiwa na mpinzani wake huku jukumu pekee lililosalia likawa ni kupambana nae ana kwa ana kwenye hali ya mmoja dhidi ya mmoja.

Hiki huwa ni kibarua kigumu mno kuliko vyote kwa Chirwa, atafanya nini na ameshazaliwa mwanaume? Huwa hana namna zaidi ya kutumia siraha yake moja kubwa sana ambayo kwenye mpira wa Tanzania inasamsaidia sana na hata Afrika bado inahitajika kwa ukubwa wake.

Ikifikia hali kama hiyo, hutumia nguvu zake alizojaaliwa, Chirwa ana nguvu sana uwanjani zinazomwezesha kupambana vizuri tu kwenye hali ya mmoja dhidi ya mmoja. Kwenye mchezo dhidi ya Simba, alikuwaakioneshana uwezo na matumizi mazuri ya nguvu dhidi ya Jjuuko Murshid.

Ni ngumu sana kumuona Chirwa akianguka anguka hovyo uwanjani, ni mfupi na mwenye misuli iliyojengeka sana. Kiafrika tunasema dona limeujenga vizuri tu mwili wake na hii ni moja kati siraha muhimu sana kwenye vita ya mpira.

Lakini Chirwa ni mchezaji mwenye maamuzi sahihi sana, kutokuwa na vitu vingi mguuni kunampunguzia uwezo wa kucheza kwa kipaji cha juu kwenye nafasi ya pembeni, kule kunahitaji kasi, kumshinda mpinzani wako kwenye vita dhidi yake na kujipambanua kwa stadi ya kuuchezea walau kiasi mpira.

Ni rahisi sana kumuona kwenye uwezo wake pindi anapocheza kwenye eneo la katikati mwa uwanja pale kwenye matumizi ya nguvu, matumizi ya akili na matumizi sahihi ya maamuzi sahihi. Hapa ataruka vichwa kwenye mipira ya kona, ataruka juu kuishinda mipira ya krosi na atakimbia kuwasumbua walinzi wa kati.

Unaweza kusema kwamba kutokuwa na vitu vingi ndio ubora wake kwani anatumia nguvu nyingi na juhudi nyingi sana kuendelea kubaki kwenye ubora, safari yake kuingia kwenye kikosi cha Yanga ilikumbwa na misukosuko mingi sana, alikutana na kila aina ya masahibu yanayokatisha tamaa.

Aliitwa mtalii, alitukanwa sana, aliitwa mchezaji wa kawaida sana na aliitwa mchezaji asiye na uwezo hata robo tatu ya kukichezea kikosi cha Yanga na soka la Tanzania kwa ujumla. Maneno aliyokutana nayo kwenye soka la Tanzania huenda yalikuwa yakimtoa machozi kila ilipoitwa leo.

Machozi haya hayakuwa ni kwa sababu ya kutokomezwa maneno ya kukatisha tamaa bali yalikuwa ni ya kujipiga kifua kama mwanaume na kujisemea moyoni kwamba, waache tu wakinipa nafasi tu nitawaonesha kitu ambacho hakijawahi kushuhudiwa na mboni zao tangu wazaliwe.

Kila alipoiangalia leo yake wakati huo alitamani sana kuingia kwenye kikosi cha Yanga lakini atacheza nafasi ya nani wakati Amissi Tambwe tayari alishajenga ikulu yake na Donald Ngoma? Hakuwa na mawazo sana kwani alijiamini na aliwekeza imani yake kwenye juhudi na nidhamu yake ya kupambana kwenye mazingira magumu.

Alijaribu kuzifanya changamoto kuwa fursa na sasa ni mshindi! Hakuzaliwa na mbawa ambazo pengine zingemfanya kuchomoza juu ya wote na kuwafunika kisha kuonekana yeye tu, lakini alizaliwa na miguu miwili ya kusimama wima, ngangari na kishupavu kisha akaonekana mbele ya wote.

Ni kama vile alianguka, akasimama, akaanguka tena na akasimama tena huku akijiapiza kutoanguka tena hata kamna kutatokea lolote lile, tunavyozungumza amefanikiwa kufunga mabao matatu kwenye michezo mitatu mfululizo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ameifunga Stand United na amefunga kwenye ratiba dhidi ya simba ambayo itamfanya kuonekana kwa thamani ya jasho lake uwanjani, Chirwa endelea kusimama wima si mimi tu kila mmoja anatamani kuona thamani ya jasho lako uwanjani. Halidi Abdulrahman.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *