Ni Yanga huru dhidi ya Azam yatima inayosaka matokeo

Kiungo mkabaji wa Azam, Himid Mao akiambaa na mpira huku akichungwa na Thaban Kamusoko wa Yanga katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Kiungo mkabaji wa Azam, Himid Mao akiambaa na mpira huku akichungwa na Thaban Kamusoko wa Yanga katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Mabao nane ya kufunga, hawajaruhusu bao kwenye michezo miwili waliyocheza kwenye Kombe la Mapinduzi, Yanga inashuka dimbani usiku wa Jumamosi hii kuwania pointi tatu  dhidi ya Azam isiyo na kocha wa kudumu kias cha kufananishwa na yatima.

Ni pambano litalopigwa kwenye dimba la uwanja wa Amaan, Zanzibar ikiwa ni muendelezo wa mechi za kombe la Mapinduzi.

Yanga ndiyo vinara wa msimamo wa kundi B kwa pointi sita huku Azam, ikiwa kwenye nafasi ya pili ikiwa imejikusanyia alama nne hivyo huufanya mchezo wenyewe kuwa mgumu uwanjani.

                          FALSAFA YA YANGA NA WACHEZAJI WA KUCHUNGWA.

Kocha wa Yanga, George Lwandamina anatafuta kilicho bora kutoka kwa wachezaji wake. Mara nyingi huwajaribu wachezaji kutokana na mchezo husika. Lwandamina, hutumia mfumo zaidi ya mmoja uwanjani, huweza kucheza 3-5-1-1 ambao umetokana na mfumo wa 3-5-2 au 4-4-2 ndani ya mchezo mmoja. Anawatumia Juma Abdul, Andrew Vincent, Kelvin Yondan na Mwinyi Haji kama walinzi wanne kwenye 4-4-2. Anapobadili mbinu uwanjani kwenda kwenye 3-5-1-1 huwaacha nyuma Andrew Vincent, Yondani na Justice Zulu huku majukumu ya Juma Abdul na Mwinyi Haji huwa ni kushuka kwenye mstari wa idara ya ulinzi pale timu inapopoteza mpira na hufanya mijongea ya kuisaidia timu kushambulia pindi inapopoteza mpira. Idara ya kiungo ni moja kati ya sehemu yenye ubora mno kwenye falsafa ya Lwandamina anaonekana kumuamini sana, Said Juma Makapu au Justice Zulu na Haruna Niyonzima au Thabani Kamusoko kuiendesha timu kupata matokeo. Licha ya ubora aliourithi kutoka kwa Hans van Pluijm, kwa kipindi hiki kifupi tayari ameanza kupandikiza mbegu za aina ya soka analotaka timu yake icheze, alimpumzisha Donald Ngoma kwenye mchezo dhidi ya Zimamoto hivyo Ngoma anatarajia kurejea kwenye kikosi cha kwanza. Wachezaji watakaoamua matokeo kwa upande wa Yanga na wale wa kuchungwa na Azam, hakuna shaka Simon Msuva aliyekuwa na muendelezo wa uchezaji bora uwanjani na ufungaji ameonekana kufanya mijongeo ya hatari sana pembezoni mwa uwanja kwenda mbele hasa anapokuwa huru yaani bila kughasiwa na walinzi wa timu pinzani uwanjani, ni lazima Azam wamchunge sana! Donald Ngoma, Juma Abdul, Haruna Niyonzima ambaye amekuwa akiubeba mpira kuanzia katikati mwa uwanja kuelekea kwenye robo tatu yao ya mwisho na kupiga pasi sahihi, amekuwa msaada sana kwa Yanga. Mchezaji mwingine wa kuchungwa ni Emmanuel Martin kwa kuwa anahitaji kumhakikishia Lwandamina kwamba anastahili kuwepo kwenye kikosi cha kwanza.

FALSAFA YA AZAM NA WACHEZAJI WA KUCHUNGWA.

Chini ya Idd Cheche, Azam ni dhaifu mno kimbinu uwanjani. Haina muunganiko mzuri uwanjani, haina uwiano mzuri uwanjani, ni ngumu mno kueleweka inacheza soka la aina gani kwa sasa. Ubora wa utimamu wa kimwili kwa Azam upo chini mno, mipango, uhakika wa pasi zenye uhakika hauna uhakika kwa Azam licha ya kushinda mchezo wao wa kwanza na kulazimishwa sare kwenye mchezo uliofuata.

Bado kuna matatizo ya maelewano hafifu baina ya wachezaji wa Azam, hata hivyo mchezaji ambaye anaweza kuamua matokeo kwa Azam ni chipukizi Shaaban Idd ambaye ameonekana kufanya safari za hatari sana pindi anapokuwa na mpira mguuni.

Mchezaji wa kutumainiwa kwa upande wa Azam ni mlinda mlango, Aishi Manula ambaye huwa bora sana anapocheza dhidi ya timu kubwa.

DAKIKA TISINI.

Eneo la kiungo ndilo litakaloamua nani atashinda kwenye mchezo wenyewe. Licha ya mbinu hafifu za Azam, hautarajiwi kuwa mchezo rahisi kwa kuwa historia baina ya wawili hao haioneshi namna ambavyo mmoja wao hupata urahisi.

Upande wa kulia na kushoto kwa Yanga ni hatari sana hivyo Azam, ni lazima wacheze kwa kukaba maeneo kuhakikisha Simon Msuva, Emmanuel Martin, Mwinyi Haji na Juma Abdul hawatembei na mpira wakiwa huru kuelekea kwenye robo tatu yao ya mwisho na kusababisha madhara,.

kwa Yanga wanahitaji kufanya kinyume chake. Hakuna anayejua lakini mara nyingi huwa si mchezo wenye mbinu nyingi bali vurugu na vitendo visivyo vya kiungwana hutawala kwa timu zote.

Saikolojia ya Yanga ipo huru kwa kuwa hata wasipoibuka na ushindi au kupata sare hawana cha kupoteza, hii ni faida kwao kwani watakuwa na muda mwingi wa kutumia ufundi wao kupata matokeo tofauti na Azam wanaokwenda kutafuta ushindi kwenye mchezo huo. Dakika tisini zitaamua!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *