Nendeni tu! Ronaldo aigomea Serikali ya Hispania

Mshambuliaji wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo amegoma kukaa chini kumalizana na Mamlaka ya Mapato nchini Hispania juu ya madai ya ukwepaji wake wa kodi.

Ronaldo ambaye baada ya tuhuma hizo kuibuka alitishia kuondoka nchini Hispania na Real Madrid amepewa muda wa kuyazungumza ili wayamalize, amlipe mfalme chake na maisha mengine yaendelee lakini nyota huyo amekomaa kwamba hajakwepa kodi.

Ronaldo anatuhumiwa kukwepa kodi ya pauni zisizopungua milioni 13.1 na waendesha mashitaka wameamua kumfikisha mahakamani ambapo ikithibitika, atalazimika kulipa kodi hio, faini na huenda akapata adhabu ya kwenda jela, japokuwa si rahisi sana kuingia humo endapo atalipa kodi hio.

Ronaldo kupitia kwa wawakilishi wake anadai kwamba alilipa kodi kubwa kuliko hata aliyokuwa anastahili kuilipa, hajawahi kujaribu kukwepa wala kuvificha vyanzo vyake vya mapato, hivyo haoni sababu ya yeye kuambiwa akae chini na wahusika ili wamalizane.

Ronaldo amesema endapo bwana kodi ameamua kumfikisha mahakamani watamalizana huko huko kwa mwenye ushahidi kuutoa kwa sababu baada ya kutafakari kwa kina na upekuzi, wanasheria wake wanadai, madai ya Serikali ya Hispania hayana msingi wowote.

Nyota huyo ana dili za kibiashara na kampuni kubwa za kimataifa kama vile Nike, Coca Cola, Emirates, Castrol, Herbalife na Tag Heuer.

Jopo la wanasheria wake limeitaka Serikali ya Hispania kuhakikisha haki inatendeka kwa mateja wao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *