Nani mbabe mechi ya 84, Simba na Yanga

Donald Ngoma akijiandaa kupiga shuti mbele ya mlinzi wa Simba, Mohamed Hussein

MAHASIMU wa jadi katika soka la Tanzania, Simba na Yanga  zinatarajia kukutana Jumamosi ijayo ama kwenye Uwanja wa  Uhuru jijini Dar es Salaam au Uwanja wa Taifa.
Kama itachezwa Uwanja wa Uhuru itakuwa ni mara ya kwanza  baada ya miaka 11.
Mara ya mwisho timu hizo kupambana kwenye uwanja huo ilikuwa  ni Oktoba 29, 2006 kwenye mechi ya Ligi Daraja la Kwanza  Tanzania Bara (sasa Ligi Kuu).
Timu hizo zilitoka suluhu bila kufungana. Mechi hiyo itakayochezwa  Oktoba 28 ambayo Yanga itakuwa wenyeji itakuwa ni ya raundi ya  nane ya Ligi Kuu Tanzania Bara inayoendelea kutimua vumbi  nchini.
Rekodi zinaonyesha kuwa baada ya mechi hiyo, timu hizo  hazijawahi kucheza tena uwanja huo, kwani mechi iliyofuata Julai 8,  2007 ilichezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro.
Ikumbukwe ilikuwa ni mechi ya Ligi Ndogo kutafutwa bingwa,  kabla ya kuanza kwa mfumo mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara  ulioanza kuchezwa mwezi Agosti na Septemba kama ilivyo nchi  nyingi barani Ulaya.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwa dakika 120 baada ya timu hizo  kuigia fainali katika mtindo wa mtoano, zilitoka sare ya bila  kufungana na Simba kufanikiwa kutwaa ubingwa kwa mikwaju ya  penalti 5-4.
Mechi ya kwanza Simba na Yanga kuchezwa kwenye uwanja mkuu  wa Taifa ilikuwa ni Oktoba 26, 2008 iliyoisha kwa Yanga kuibuka  na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Ben Mwalala dakika ya 15 ya  mchezo.

Mechi ya 84

Itakuwa ni mechi ya 84 timu hizo kukutana kwa michezo ya ligi tu,  tangu ilipoanzishwa mwaka 1965 wakati huo ikiitwa Ligi ya Taifa.
Mpaka sasa watani hao wameshapambana mara 83 kwenye mechi  za Ligi Kuu peke yake.

Yanga bado vinara kwa Simba

Kati ya mara 83 ambazo timu hizo zimekutana, Yanga inaongoza  kwa kuifunga Simba mara nyingi zaidi.
Yanga imeifunga Simba mara 31, huku Simba yenyewe ikiwa  imeichapa Yanga mara 24 na kutoka sare mara 28.

Simba mbabe wa Yanga karne ya 21

Tangu kuanza kwa karne mpya ya 21, Simba imeifunga Yanga mara  nyingi zaidi.
Kwa mujibu wa rekodi zilizopo ni kwamba, Simba imefunga Yanga  mara 11 kuanzia mwaka 2000 ikiwa ni mwanzo wa karne ya 21.
Simba na Yanga zimecheza mara 33 kwenye Milenia, Yanga  ikishinda mara saba na timu hizo zimetoka sare mara 15.

Kichuya kuweka rekodi ya Tambwe?

Winga wa Simba Shiza Kichuya, iwapo atafunga kwa upande wa  Simba basi atakuwa akiifunga Yanga kwa mara ya tatu mfululizo na  kujitengenezea rekodi kwenye mechi hizo za watani.
Alifunga goli Oktoba Mosi 2016, Simba ikitoka sare ya bao 1-1  dhidi ya Yanga mechi ya kwanza msimu uliopita, huku akifunga bao  mechi ya mzunguko wa pili wa ligi hiyo, Februari 25 mwaka huu,  Simba ikishinda mabao 2-1.
Straika wa Yanga, Amissi Tambwe ana rekodi ya kuifunga Simba  mara tatu mfululizo.
Alifanya hivyo, Septemba 26, 2015, alipofunga goli moja, Yanga  ikishinda mabao 2-0, lakini pia goli lingine alilifunga Februari 20  mwaka jana akifunga bao, Simba ikilala tena kwa mabao 2-0.  Oktoba Mosi mwaka jana alifunga bao moja, timu hizo zikitoka  sare bao 1-1, lakini alishindwa kuendeleza rekodi ya kufunga  mfululizo, aliposhindwa kufanya hivyo, Yanga ilipolala mabao 2-1  Februari 25 mwaka huu, mechi ya mzunguko wa pili msimu uliopita.

Ajibu kufunga kwa mara ya kwanza?

Straika wa Yanga, Ibrahim Ajibu kama akifunga bao, ataweka  rekodi ya kufunga goli kwa mara ya kwanza kwenye historia yake  ya soka nchini.
Tangu apandishwe kikosi cha kwanza cha Simba mwaka 2013,  hajawahi kuifungia Simba goli lolote kwenye mechi za watani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *