Namhurumia sana Benitez, ila simuelewi Perez

Kuna wakati mgonjwa anaweza kushauriwa na daktari ale matunda na mbogamboga ili aishi lakini anaweza kuamua kuacha ili afe. Unaweza kushangazwa na hili lakini hapa ulimwenguni kuna mambo yanastaajabisha kiasi kwamba sintofahamu huwa huwa jibu sahihi.

 

Ballon d'rFedha inaendelea kuifanya Real Madrid iishi kwa presha muda wote, majanga yanaongezeka, kufukuzana kunashika hatamu na mataji yanazidi kukauka. Ni kama vile natembea juu ya mawazo yangu, sikupata muda wa kutafakari kwa kina juu ya mustakabari wa Carlo Ancelloti na maisha sahihi ya Cristiano Ronaldo mbele ya Rafael Benitez. Wakati Florentino Perez akiwaza juu ya juu ya Carlo Ancelloti kupoteza muelekeo na kuamini Rafael Benitez atawarudisha kwenye mstari, kumbe yeye ndiye aliyepoteza muelekeo alistahili kwanza kurudi mstarini. Muda huo huo Rayo Vallecano wasingeweza kusahau fedheha iliyowakuta, mabao 10-2? Getafe na Granada nao wangetelezea huko. Lakini Florentino Perez hakuyaona yaliyoushangaza ulimwengu, alifumba macho kabla ya mlango wa kuingilia Santiago Bernabeu haujapisha sura mbili, moja ikiwa na furaha huku nyingine ikiwa na majonzi.

Rafael Benitez aliingia huku akiwaza ataendesha vipi maisha yake ya udikteta mbele ya mastaa wa Carlo Ancelloti, hapa ndipo Casemiro, Mateo Kovacic, winga Lucas Vazquez na yule Danilo walipoanzisha maisha mapya. Walikula na kunywa kwenye kumbi za starehe wakijua fika kwamba wapo salama, lakini akilini walifikiria sana namna ambayo wataweza kuyatekeleza majukumu mapya, kucheza kwa kujilinda zaidi kuliko kushambulia. Na hapo hapo BBC ikawa si furaha tena mbele ya macho ya Cristiano Ronaldo. Kila akitazama pembeni alitamani kulia ila alipata hafueni baada ya mshikaji wake Messi kuingia kwenye chumba cha upasuaji.

Kuanzia hapo nilianza kumhurumia sana Benitez, kwani kadiri siku zilivyosonga mbele, like kilichomuondoa Carlo Ancelloti kilionekana kumnyemelea kwa karibu mno. Real Madrid imekuwa timu inayoweza kupata matokeo dhidi ya timu ndogo ilhali huku kwa kina Barcelona, PSG na Atletico Madrid kunaonekana kuwa maji ya shingo. Yote haya ameyataka Perez.

Namheshimu sana Rafael Benitez, kuifanya Liverpool iwe timu yenye hadhi ya juu si jambo la kawaida ila kuifanya Real Madrid kuwa timu yenye kariba ya Liverpool si jambo la kawaida zaidi. Nashangaa kisha nastaajabika kabla sijamuonea huruma Benitez kwa kushikilia misimamo isiyowanufaisha mastaa wa timu, Ronaldo amebeba ujumbe kwenye paji lake la uso, Benzema na Bale wanamfikiria Carlo Ancelloti na maisha yake mapya kule Bayern Munichen huku mimi sintofahamu likiwa jibu langu sahihi juu ya Florentino Perez. Simuelewi kabisa. Huyu ni rais anayefanya anachokiamini na anayeamua anachokiwaza. Ni rais mwenye msimamo. Kwake aheri afe kwa kuacha matunda na mbogamboga kuliko kuishi kwa kufuata ishauri wa daktari usioendana na msimamo wake. Tukutane Real Madrid ikifanikiwa kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa, La Liga na Copa del Rey mfululizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *