Mtazamo wa Usajili Ligi Kuu Dirisha Dogo – Yanga

Dirisha Dogo la usajili nchini Tanzania linafunguliwa Jumatano Novemba 15 na litafungwa Disemba 15, 2017.

Vilabu hutumia kipindi hicho kidogo cha usajili kuongeza wachezaji katika kuimarosha vikosi vyao kuelekea raundi ya pili ya lala salama.

Soka 360 imefanya uchambuzi ya Timu za Ligi Kuu na mahitaji yake ya wachezaji katika kipindi cha dirisha dogo.

Yanga SC

Hawa ni mabingwa watetezi wa ligi kuu Tanzania bara kwa mara tatu mfululizo wakifanya hivyo 2014-15, 2015-16 na 2016-17 lakini pia wakisimama kama mabingwa wa kihistoria wa ligi hiyo kwa mara 27 toka kuanzishwa kwake mwaka 1965 .

Kwa misimu kadhaa Yanga SC wamekuwa vyema katika usajili kwa maana ya kuandaa timu nzuri katika mapambano ya ligi hii ndio maana kwa sehemu kubwa wameweza kuitawala ligi kwa muda mrefu ingawa changamoto kubwa ni michuano ya kimataifa .

Msimu huu wa 2017-18 ni moja ya msimu ambao mabingwa hawa hawakufanya usajili wa kutisha kama ilivyo ada zaidi ya kurekebisha mikataba ya wachezaji waliopo , kuziba mapengo muhimu yenye ulazima mkubwa mfano eneo la kiungo walipowanasa Pappy Tshishimbi toka Congo, Rafael Daudi wa Mbeya City, Piusi Buswita wa Mbao FC na kiungo huru Buruan Yahya.

Sambamba na hilo ni kuimarisha safu ya ulinzi kwa kumsajili Shaibu ‘ Ninja ‘ toka Jang’ombe boys Zanzibar , kipa Youthe Rostand na kinda Ramadhani Kabwili baada ya kipa wao namba moja Deogratius Munish kutimkia Afrika Kusini. Gadiel Michael mlinzi wa kushoto pia wamemsajili kipindi hiki kama back up kubwa kwa Haji Mwinyi kwenye ulinzi wa kushoto.

Kwenye safu ya ushambuliaji ni ujio wa Ibrahim Ajibu ndio badiliko kubwa toka Simba SC ambaye mpaka sasa wamelamba dume .

Lakini pia kwa mara ya kwanza walitoa nafasi kubwa kwa vijana wa kikosi cha pili kujiunga na timu kubwa kama kuwapa nafasi ya kujifunza kwa wakubwa wao kwa ajili ya Yanga ya kesho , vijana kama Maka Edward, Saidi Mussa na golikipa Ramadhani Kabwili

Lengo limetimia ?

DIRISHA DOGO

Safu ya ulinzi

Tukianzia langoni; Youthe Rostand, Beno Kakolanya na Ramadhani Kabwili ni kombinesheni nzuri na hapa Yanga hawahitaji kusajili kipa mwingine au kumwacha yoyote. Rostand ni kipa kiongozi katika muunganiko huo lakini Juma Pondamali anatakiwa kumsuka vyema kwenye punch zake.

Kwenye michuano ya klabu bingwa atakutana na washambuliaji matured wenye uwezo mkubwa kuzitumia hizo rebounds na kufunga . Hili ni tatizo lake kubwa ! . Kakolanya amekuwa majeruhi wa muda mrefu anahitaji match fitness ili kumjenga zaidi . Ni wakati wa kuangalia uwiano wa ugawanaji wa mechi ili makipa wote wawe sawa. Si mbaya Kabwili wakianza kumpa majukumu mechi za Mapinduzi Cup mwezi ujao ili kufikia January timu itapokuwa ‘ busy ‘ kwenye mashindano mengi kuwe na depth nzuri kiufundi eneo hilo.

Tukija kwa walinzi wa pembeni Juma Abdul na Hassani Kessy kulia hakuna shida ya kuongeza mlinzi mwingine . Wote ni wapambanaji , Juma Abdul licha ya kiwango chake kupanda na kushuka lakini bado imara kwa michuano ya ndani na nje ni kiasi cha kumuandaa zaidi Kessy kuwa bora kwa kumpa mechi za kutosha .

Kushoto kwa Gadiel Michael na Haji Mwinyi napo kupo imara . Haji Mwinyi licha ya kukosa mechi kadhaa kwa ujio wa Gadiel bado ana uzoefu mkubwa kimataifa. Ni mlinzi ambaye amechangia upatikanaji wa vikombe vitatu mfululizo vya ligi kuu pia kuifikisha timu hatua ya makundi kombe la Shirikisho 2016. Anahitaji match fitness ili kumwandaa ( readiness ) wakati wowote kumpa back Gadiel ambaye anasimama kama chaguo la kwanza kwa sasa.

Nafasi ya walinzi wa kati kwa Yanga kuna changamoto kubwa kwa sasa. Toka kuondoka kwa Vincent Bossou bado benchi la ufundi halijapata mbadala sahihi wa mlinzi huyo . Ni dhahiri kombinesheni ya Kelvin Yondani na Vincent Andrew ndio tegemeo kwa sasa lakini wasaidizi wao nahodha Nadir Haroub na Shahibu ‘ Ninja ‘ wanakinzana sana kwa ubora na viwango kwa uwiano na muunganiko wa Kelvin Yondani na Andrew Vincent.

Nadir ni dhahiri umri umekwenda , uwezo anao lakini kasi na nguvu ya kupambana umepungua. Ni wakati sasa wa kupumzika ili Yanga ipate mlinzi mwingine bora zaidi ya Yondani na Dante ili asimame kama mlinzi kiongozi kwenye michuano ya ndani na nje .

Shaibu ataendelea kuwa understudy chini ya Dante , Yondani na mlinzi huyo ambaye watamsajili huku Nadir akijiandaa kustaafu kwa heshima au kupangia majukumu mengine klabuni.

Nafasi ya kiungo

Hili ni eneo nyeti sana kwa klabu yoyote ile kimbinu na kiufundi . Ndio sehemu inayosimamia mifumo yote miwili ya kushambulia na kujilinda .

Kabla ya msimu huu wa 2017-18, Yanga walikuwa na tatizo kubwa la kiungo cha chini licha ya kubeba ubingwa mara tatu mfululizo!. Lakini tatizo hilo lilikuwa halionekani sana kuithiri timu kutokana na ubora wa viungo wa pembeni na safu ya ushambuliaji.

2015-17 , misimu yote miwili udhaifu huo ulifichwa na viungo kama Saimoni Msuva upande wa kulia , huyu mbali ya kucheza kama winga primarily kutengeneza krosi na kusaidia attacking patterns lakini pia kasi yake iliwafanya wapinzani kucheza kwa tahadhari sana tofauti na sasa .

Hii kimbinu ilisaidia pia mfumo wa kujilinda kwa kumsogeza adui mbali. Upande wa kushoto, Deusi Kaseke alisaidia kwenye marking, blocking, disrupting eneo la kati pia agility ( kasi ) kwenye wing ilileta uwiano na winga ya kulia kuifanya timu kuruka vyema katika mabawa yake pande zote .

Haruna Niyonzima, ubora Kamusoko ( sio huyu wa majeruhi ya mara kwa mara ) pia Donald Ngoma aliyekuwa anakuja chini kama deep playmaker eneo la kiungo liliifanya Yanga kuziba madhaifu ya kiungo wa chini .

Msimu huu Yanga imeondoa tatizo hilo kwa kumpata Tshishimbi amabaye analeta balansi nzuri eneo la kati kama kiungo mkabaji, mchezeshaji pia mshambuliaji ( to some extent) lakini benchi la ufundi na kamati ya usajili lilijikuta linapoteza balansi ya timu kwenye wings .

Piusi Buswita huu ni usajili mpya msimu huu. Dhumuni kuu la usajili wake ni ‘ ukiraka wake ‘ eneo la kiungo pia umri mdogo kwa maana ya kudumu muda mrefu kikosini . Buswita ana uwezo kucheza kama kiungo pia nafasi za ulinzi wa pembeni lakini kiufundi bado ni ‘ average’ player anayehitaji muda mrefu kufikia kiwango cha brand ya Yanga kwenye mechi za kimataifa .

Hana kasi , nguvu na uwezo wa kuachia mpira kwa wakati timu inafanya ‘ build up ‘ ya shambulizi pembeni . Huyu kwa sasa ni tegemeo kikosi cha kwanza wing ya kulia hapo utaona dirisha dogo la usajili Yanga inahitaji matured player kiwango juu ya Saimoni Msuva ili waweze kuwa bora katika wing hiyo pia kuleta uwiano mzuri na uwepo wa Tshishimbi eneo la kati . Wakati huo Buswita atakuwa anasahihisha makosa yake .

Wing hii pia ina kiungo Juma Mahadhi , huyu wengi tulitarajia kurithi mikoba ya Saimoni Msuva lakini ni mchezaji ambaye ameshindwa kwa kiasi kikubwa kuitendea haki nafasi hiyo pia kama kiungo wa kati ( juu ) . Huyu kamati ya usajili na benchi la ufundi wasisite kumtoa kwa mkopo ili akaimarishe kipaji chake.

Upande wa Buruani Yahya, Yusufu Mhilu, Maka Edward na Saidi Mussa bado ni vijana wadogo ni kiasi cha mwalimu kuendelea kuwaamini na kuwapa nafasi ili waongeze kujiamini. Yusufu Mhilu ana uwezo mzuri kama kiungo wa kati na pembeni kinachomwangusha ni kasi. Lwandamina ni muumini mzuri wa viungo wenye kasi, nguvu na uhakika wa vitendo .

Rafael Daudi ni mapema sana kumkatia tamaa kutokana na kukosa ile kasi aliyokuwa nayo Mbeya City . Lwandamina ameijenga njia ya kati juu ya mgongo wa Tshishimbi anachotakiwa Rafael kukifanya ni kuitazama kasi ya kiungo huyo na kutafuta njia ya kuendana nae ili kuleta uwiano mzuri na washambuliaji wa mbele kama Ajibu .

SAFU YA USHAMBULIAJI

Usajili wa Ibrahim Ajibu bado ni mzuri lakini ili kujiweka sawa Yanga wanahitaji kusajili pacha wake mwenye kasi na uwezo mzuri kumalizia kazi ya kiungo huyu mshambuliaji ( playmaker ) . Obrey Chirwa amesimama vyema lakini shida ni nafasi hii kukosa depth kimbinu kwa maana wengi wa wachezaji eneo hilo ni pancha tupu! .Ngoma bado ni majeruhi na fighting spirit yake imepungua sana sambamba na pacha wake Amisi Tambwe .

Kama mfuko wa usajili unaruhusu si mbaya kuwafungulia milango washambuliaji hao na kupata walio bora zaidi yao hususani Amisi Tambwe ambaye ameshindwa kuitumikia klabu hata kwa mechi moja toka aongeze mkataba wa mwaka mmoja ambao unakwenda ukingoni.

Antony Mateo licha ya kumuongezea mkataba wa miaka miwili msimu huu bado hajaonesha kama ni msaada kwa timu hiyo katika safu ya ushambuliaji, atolewe kwa mkopo kutoa nafasi ya kusajili vijana wenye ubora na uchu wa mafanikio.

By SAMUEL SAMUEL

Itaendelea sehemu ya tatu kwa Azam FC …..

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *