Mnaandika lakini? Ajib tisa , Okwi saba

Mchakachaka wa Ligi Kuu Tanzania Bara unazidi kukolea baada ya timu kutoana jasho kuwania pointi tatu katika raundi sita mpaka sasa, lakini utamu zaidi upo kwa nyota Ibrahim Ajib wa Yanga na Emmanuel Okwi wa Simba.

Macho yote ya wadau wa soka yapo kwa mastaa hawa kwa jinsi walivyo mstari wa mbele kuzifungia mabao timu zao.

Ajibu aliyejiunga na Yanga msimu akitokea kwa mahasimu wao, ndiye kinara wa ufungaji ndani ya kikosi hicho cha Wanajangwani akiwa na mabao matatu.

Okwi pia anaongoza msimamo wa upachikaji mabao  baada ya kuwafungia Wekundu hao wa Msimbazi mabao saba hadi sasa.

Ukiachilia mbali ufungaji mabao, mvutano wa nyota  upo kwenye kuchangia pointi kwa timu zao, hapo sasa Ajib ndo anaibuka kinara baada ya mabao yake matatu  kuisadia Yanga kuvuna pointi tisa, huku Okwi akichangia pointi saba kwa mabao yake saba.

Ajib amefunga mabao yake katika michezo dhidi ya Njombe Mji ambapo Yanga ilibuka na ushindi bao 1-0, akafunga tena bao wakati Yanga ikiichapa Ndanda bao 1-0, kabla ya kufunga bao la pili lililoihakikishia kuvuna pointi katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar, ambao uliisha kwa Yanga kushinda mabao 2-1.

Yanga kwa sasa ina pointi 12, ambapo ukitoa mabao ya Ajib, Wanajangwani hao wanabaki na pointi tatu.

Okwi amefunga mabao yake katika michezo ifuatayo, alifunga mabao manne wakati Simba ikiibuka na ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting, akafunga mabao mawili, Simba ilipoibuka na ushindi wa mabao 3-0, kabla ya kufunga bao ambalo liliiokoa Simba na kipigo kutoka kwa Mtibwa Sugar, mchezo huo uliisha kwa sare bao 1-1.

Simba ina pointi 12, ambapo ukitoa mabao yote yaliyofungwa na Okwi, Wekundu hao wa Msimabzi wanasalia na pointi tano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *