Mbaraka Yusuph Mechi moja Azam, goli moja

AMEANZA vitu vyake. Mechi yake ya kwanza tu kucheza, tayari  ametupia kambani. Amefunga goli la kwanza kwenye timu yake  mpya ya Azam FC dhidi ya timu yake ya zamani, Kagera Sugar.
Mbaraka Yusuph, alifunga bao hilo dakika ya 43 akimalizia pasi ya  safi aliyopenyezewa na Yahya Zayd.
Na hii ni mara ya kwanza mchezaji huyo kuicheza Azam kwenye  mechi ya Ligi Kuu, baada ya kushindwa kufanya hivyo kwenye  mechi mbili zilizopita kutokana na kuwa majeruhi.
Aliumia akiwa na timu ya taifa, Taifa Stars kwenye michuano ya  COSAFA iliyochezwa Julai mwaka huu.
Goli hilo ni kengele ya hatari kwa mastraika wengine wa Ligi Kuu  Tanzania Bara kwenye kinyang’anyiro cha kuwania kiatu cha  dhahabu.
Alishika nafasi ya pili msimu uliopita akifunga magoli 13, akizidiwa  goli moja tu na vinara waliogawana zawadi ya ufungaji bora msimu  huo, Simon Msuva wa Yanga na Abdulrahman Mussa wa Ruvu  Shooting waliofunga magoli 14 kila mmoja.

Zao la Simba

Mbaraka ni zao kutoka klabu ya Simba na kabla ya kujiunga na  klabu yake ya sasa ya Azam alitokea Kagera Sugar.
Anakumbukwa kuwa ni mmoja wa makinda wa kikosi cha pili cha  Simba waliounda timu kali ya vijana akiwa na kina Ramadhani  Singano ‘Messi’, Abdalah Seseme, Wiliam Lucian,  Ibrahim Ajibu,   Said Ndemla, Hassan Isihaka, Haruna Chanongo na wengine chini  ya kocha Selemani Matola na kufanikiwa kutwaa Kombe la Banc  ABC, Uhai Cup na Kinesi.
Licha ya kuwa na mwanzo mzuri kwenye timu ya vijana ya  Mnyama, Mbaraka Yusuph hakufanikiwa kupenya kwenye timu ya  kikosi cha kwanza cha Wekundu wa Msimbazi.
Wakati kina Singano, Ishaka, Ndemla, Chanongo na wengine  wakipenya, yeye alipelekwa Kagera Sugar kwa mkopo.

Ang’ara Kagera Sugar

Msimu wa kwanza tu ndani ya Kagera alifanya vizuri kwa kufunga  magoli mengi zaidi kufanya Simba kutaka kumrudisha tena baada  ya kiwango kizuri kipindi cha mkopo.
Hata hivyo, aligomaa kurudi akidai kuwa hana mkataba Simba,  huku wao wakidai kuwa Yusuph amebakiza mwaka mmoja kwenye  mkataba wake
Mgogoro huo uliamuliwa na Shirikisho la Soka Nchini (TFF) na  Mbaraka na klabu yake ya Kagera Sugar walishinda kesi.

Kesi juu ya kesi

Mbaraka aliingiza tena mgogoro timu yake ya Kagera Sugar  kwenye mgogoro mwingine wa kimkataba na Azam FC.
Aliingia mkataba na Azam, huku timu yake ya zamani ikidai kuwa  bado wana mkataba naye.
Ilidaiwa kuwa TFF ilikuwa na mikataba miwili, mmoja ukisema  kuwa alibakisha mkataba wa mwaka mmoja Kagera Sugar ambayo  uliokuwa unamalizika, na mwingine ulionyesha ana mkataba wa  miaka mitatu, hivyo imebaki miwili.
Wakati mashabiki wa soka wakisubiri kujua, upi mkataba halali  kati ya hiyo miwili na nani alifoji mkataba mmoja kati ya huo, Azam  na Kagera Sugar walikaa chini na kukubaliana kuwa Mbaraka  aichezee Lambalamba.

Ndoto yake

Kwa mujibu wake mwenye, lengo lake ni kufuata nyayo za  mshambuliaji wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ambaye anakipa  Ubelgiji kwenye klabu ya KRC Genk
“Navutiwa zaidi na timu za Hispania, yaani Barcelona na Real  Madrid, lakini pia napenda kuichezea Tp Mazembe ya DR Congo ili  niweze kupata ujuzi na nina imani ndoto zangu zitatimia” alisema  kinda huyo ambaye pia huichezea timu ya taifa, Taifa Stars.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *