Makala: Bado Lwandamina ni muhimili sahihi wa Yanga

George Lwandamina akifuatilia mchezo wa dhidi ya MCA ( Picha/ Soka360)

Kujenga timu bora ya ushindani sio kazi ya siku moja , sio kazi rahisi ambayo utaiona kwenye mechi mbili au tatu. Hii ni taaluma kama taaluma nyingine hivyo ina misingi yake na taratibu zake za kufuata pia inahitaji muda.

Papara zetu watanzania juu ya waalimu wanaokuja kufundisha vikosi vyetu, kwa muda sasa imetufanya tubaki tulipo kwa kuanza moja kila uchao.

Bado kwa maoni yangu Lwandamina ni nguzo sahihi kwenye benchi la ufundi la Yanga SC. Msimu uliopita alikuta kikosi cha Hans Van Pluijm na kuchechemea nacho mpaka kulinda ubingwa wa ligi . Nasema kuchechemea nacho kwa maana aliikuta klabu kwenye kipindi kigumu kuliko mtangulizi wake . Aliikuta klabu inayoshindwa kulipa mishahara kwa wakati kitu ambacho kilikuwa kinavunja ari na moyo wa kupambana wa wachezaji lakini kwa uwezo wake kisaikolojia na wasaidizi wake waliweza kuwajenga vyema kimbinu na kisaikolojia wachezaji hao na kuibuka mabingwa wa ligi kuu.

Aliikuta Yanga yenye lundo la majeruhi tena wachezaji tegemeo kama Donald Ngoma , Kamusoko na wengineo lakini alijenga fighting spirit kwa vijana waliobaki hata wale ambao walikuwa hawapati nafasi sana ya kucheza kama Mwashiuya , Mhilu na Mahadhi ilimradi jahazi lisonge mbele.

Aliikuta Yanga yenye migomo ya wachezaji kama Bossou na Chirwa ambao kwa nyakati tofauti waligoma kucheza kwa masilahi yao lakini falsafa ya mzambia huyu kufanya kazi na mchezaji aliyepo kwenye timu ilimfikisha kwenye Canaan ya ligi yetu. Wengi walifumba macho mechi ya mzunguko wa pili ligi kuu dhidi ya Azam FC ambayo kama Yanga angepoteza basi ni dhahiri ilikuwa njia nyeupe kwa Simba kubeba ubingwa lakini si wote mnakumbuka alivyoicheza ile mechi?

Mechi tatu tu za ligi kuu akiwa na alama 5 mkononi akishinda moja na kutoka sare mbili tayari watu wameanza kuongea. Wameanza kumnyooshea kidole hafai. Sababu kubwa wakisema timu inacheza bila muunganiko mzuri.

Ngoja tuwekane sawa ndugu zangu; tukiachana na usajili mwepesi ambao ambao kwa mara ya kwanza Yanga imeufanya katika kipindi cha miaka mitano iliyopita bado kuna sababu nyingi za kiufundi za kupelekea haya kuliko kumnyooshea kidole Lwandamina. Usajili remarkable wa Yanga SC msimu huu ni ujio wa kiungo mkabaji Pappy Tshishimbi, kiungo mshambuliaji Ibrahimu Ajibu na kipa Youthe Rostand na kwa hakika mpaka sasa wanaibeba timu kwa uwezo wao.

Timu imetoka kwenye kipindi cha maandalizi , bado miili haijanyumbuka sawasawa kutokana na mazoezi magumu ya preseason, pia kukosa mechi ngumu za kutosha za majaribio kipindi hicho. Tazameni wenzetu Ulaya kipindi cha preseason wana ligi fupi fupi nyingi ambazo zinawandaa vyema kabla ya misimu ya ligi kufunguliwa lakini hapa nyumbani ni ngumu kuziona Simba na Yanga kwenye tornaments kama hizo kabla ya ligi.

Mfano Simba SC au Azam FC tumeanza kuona breakthrough yao kimbinu na kiufundi mwanzoni tu mwa ligi kutokana na kupata mechi za kutosha kipindi cha preseason. Simba wamecheza na Bidvest, Orlando pirates na Rayons Sports. Ni timu nzuri na kipimo sahihi kwa ligi yetu. Tazama mechi alizocheza Azam FC hapa nchini kabla ya kwenda kuweka kambi ya siku kumi Uganda. Alicheza na Lipuli, Mbeya City na Ndanda na kule Uganda akacheza na timu ya taifa ya Uganda na timu nguli zaidi ya tano za ligi kuu nchini humo. Si kwamba Yanga hawakupata mechi za kirafiki lakini mechi zao huwezi kulinganisha na wapinzani wake hao wakuu, mechi dhidi ya Singida United, Ruvu Shooting, Mlandege na Jamhuri ya Pemba. Lakini bado kocha amepambana na timu yake ambayo kwa jana licha ya sare ya 1-1 na Majimaji kwa mbali tulianza kuona timu inafunguka sasa . Alama mbili ugenini si haba.

Si mpigii chapuo Lwandamina lakini nataka tufunguane katika hili ili tukinyoosha vidole tuvinyooshe tukiwa na uhakika na kile ambacho tunakifanya.

By Samuel Samuel

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *