Jjuuko Murshid, mpigie simu Novaty Lufunga

Kuna mwanaume mmoja kutoka kwenye chuo cha Victoria nchini Uganda amejengeka sana kimwili. Ukimuona sifa yake kubwa ni kucheza kwa nguvu wakati wote. Kuna wakati hulaumiwa sana lakini hio ndio aina yake ya uchezaji.

Mwanaume huyu anaitwa Jjuuko Murshid, alisajiliwa na Simba na sasa anaishi kwenye kikosi cha Simba, alitengeneza ukuta wake na Method Mwanjale katika pambano la watani wa jadi, Simba na Yanga, hapana ilikua ni Yanga dhidi ya Simba, mazoea yana taabu jamani!

Huyu ni beki mgumu pekee aliyesalia kwenye kikosi cha Simba, hakuna mwingine ukimuondoa Mwanjale, aina yake ya uchezaji ni ile ya mpira upite wewe ubaki au kinyume chake.

Jjuuko ni moja kati ya walinzi wachache wenye maamuzi magumu sana, huwa hajali chochote zaidi ya kuhakikisha timu yake inabaki salama wakati wote. Huwa hana masihara ya kitoto, ameshapevuka kimchezo muda mrefu tu na ule uvulana ulishamtoka siku nyingi tu.

Huu ni msimu mwingine ambao unamwathili kutopata mechi nyingi kutokana na upana wa kikosi cha Simba, kwenye kikosi cha Simba yupo, Mwanjale, Mbonde, James Kotei ambaye huwa anacheza kama mlinzi wa kati na kiungo wa ulinzi, ameathiriwa sana na upana wa kikosi.

Ilisemekana mfumo wa Omog hauwezi, lakini tumeshuhudia dakika zake dhidi ya Yanga licha ya kuruhusu kufungwa bao lililotokea katikati ambapo yeye na Mwanjale ndio waliokua mabosi wa sehemu hio.

Usipoupenda mpira, utampenda Jjuuko kwa aina yake ya uchezaji, amini huyu ni mlinzi mwenye kariba ya walinzi wagumu duniani, huhakikisha mpira unatoka nje ya chaki kwenye vita ya wawili tu pindi mnapowania mpira, lakini huwa mstari wa mbele kuhakikisha anapandisha mashambulizi ya timu. Wakati wa kona, hupanda kuhakikisha anapiga vichwa vya faida kwa timu yake.

Loh! Kuna wakati mchezo wa soka huongea misamiati migumu sana na huzungumza lugha tata sana, yaani lugha isiyo na maana moja kiasi kwamba huupelekea ubongo wa mtu kuhitaji maana zote ili hali ya utata isiendelee kuutesa ubongo. Hebu ngoja tukumbushane kidogo safari ya Jjuuko,  ni lugha hii ambayo huzaa maswali magumu pia. Lakini maswali haya yanakosa majibu sahihi na huishia kupata majibu mepesi yasiyo na uzito sawa kwenye mzani mmoja.

Swali ambalo niliwahi kujiuliza kila nilipoiona miguu ya Novaty Lufunga msimu uliopita ni yupo wapi Jjuuko Murshid kwenye miguu ya Novaty Lufunga? Binafsi bado namtafuta mpaka leo! Simba, msimu wa 2015/16 licha ya matatizo yote lakini Jjuuko Murshid alisimama kama nguzo imara ya ulinzi kwa watu wanne waliosimama kuunda safu ya ulinzi ya Simba.

Ni Jjuuko Murshid aliyeilinda ngome ya Simba kwa miguu yake, ni Jjuuko Murshid aliyeitwa ‘muhuni’ kwa mchezo wake wa kibabe ili kuhakikisha ngome ya Simba inabaki salama. Ni Jjuuko huyohuyo aliyehakikisha anatengeneza ugumu uliwapa shida baadhi ya washambuliaji kuifunga Simba pale walipokabiliana nayo.

Mwisho wa siku Tanzania iliimba majina ya watu wanne wagumu kutokana na aina yao ya uchezaji, majina yenyewe ni Pascal Wawa kutoka Azam, Nadir Haroub wa Yanga, Jjuuko Murshid kwenye kikosi cha Simba na Andrew Vincent wakati yupo Mtibwa.

Sifa kubwa ya watu hawa ilikua ni kucheza kwa moyo na kupambana kuhakikisha ndoto za wapinzani wao hazigeuki uhalisia mbele yao, ndipo hapo masikio yetu yakasikia juu ya ugumu wa Wawa, Cannavaro, Jjuuko na Dante akaibuka katikati yao. Simba ililamba dume! Jjuuko ni kiongozi mzuri uwanjani kwa wenzake na hawezi kuruhusu uzembe mbele ya macho yake.

Tangu msimu huo umalizike, mwanzoni mwa msimu uliofuata wa 2016/17 ulimshuhudi Jjuuko Murshid akipoteza imani kwenye kikosi cha Simba. Alikua ni Method Mwanjali na Novaty Lufunga, waliokabidhiwa majukumu ya ulinzi kwenye ngome ya Simba.

Tangu wacheze pamoja waliruhusu mabao mawili kwenye michezo minne ya mwanzo. Ubingwa hutegemea pia idadi ya mabao unayofungwa, kipindi hicho Yanga haikua imeruhusu mpira kuingia kwenye nyavu zake, yaani haikua imefungwa, suala si kuruhusu tu mabao je, walinzi ulionao wanaweza kumaliza msimu kwa kuruhusu idadi chache ya mabao?

Hapa ndipo nilioanza kumfikiria Jjuuko Murshid  na miguuni yake. Sikuuona uwezo wa Novaty Lufunga ukiziba njia zote za waharifu kuifikia ngome ya Simba, sikuuona mwili wake ukiahidi anachokifanya Jjuuko uwanjani.

Jjuuko yupo mmoja tu kwenye kikosi cha Simba kuanzia aliposajiwa hadi hivi sasa, lakini Novaty Lufunga alikuwepo zaidi ya mmoja kwenye kikosi hicho hicho cha Simba. Shughuli ya Lufunga iliweza kufanywa na watu wengi Tanzania ila shughuli ya Jjuuko ni ngumu kufanywa na watu wengi Afrika Mashariki.

Iweje tegemeo la aliyekua kocha wa Uganda, Micho kwenye kikosi cha Uganda aliyeweza kucheza na moja kati ya timu ya bora Afrika asiingie kwenye mfumo wa timu ya Simba inayocheza na Ndanda yenye Omary Mponda, Ruvu Shooting?

Hivi nilijiuliza msimu uliopita na nikawaza kwa sauti, iliwezekana mfumo wa Simba ukawa na wivu kwa Jjuuko Murshid lakini si kweli kwamba hakuweza kuingia kwenye mfumo huo. Jjuuko amezaliwa kulinda ndiyo maana licha ya kuwekwa benchi aliingia moja kwa moja kwenye kikosi cha Uganda. Hakuna aliyejali kwamba alikosa utimamu wa kimwili kwa kutocheza muda mrefu, walipomuamini hakuwa na sababu ya kutojiamini na kutimiza majukumu yake.

Ilifika wakati thamani yake ilionekana.  Huku kwa kina JKT Ruvu (wameshuka daraja), Ruvu Shooting, Ndanda na African Lyon (wameshuka daraja) miguu ya vidole vya miguu ya Lufunga vilishirikiana bila matatizo kuilinda Simba kwa mfumo huo uliomkubali, lakini muda ulitufikisha kwa kina Azam, Yanga na wale wabishi wa Mbeya City, tukakiri kwa mioyo yetu kuwa thamani ya miguu miwili ya Jjuuko ilikua kubwa mno kuliko tulivyodhani. Hio ndio misimu miwili ya Jjuuko ilivyokua.

Jjuuko ataishi kama mchezaji wa kulipwa aliyetengenezewa misingi toka Victoria University alipoonekana na jicho la Simba.  Huyu ndie anayepaswa kucheza na Mwanjale kwani licha ya kua kiongozi mzuri uwanjani hawezi kucheza kwa dakika tisini na pumzi ileile hasa kwenye michezo migumu.

Lakini umri wa Mwanjale haumruhusu kuendelea kua kwenye kiwango kile kile kwa misimu mitatu ijayo, kwa wakati huu Simba ingemtengeneza Jjuuko ili awe kiongozi baada ya Mwanjale hasa kwenye michuano ya kimataifa ambayo Simba inashiriki msimu huu.

Simba itaendeshwa kikampuni, hilo ndilo tarajio letu hivyo basi, tunategemea kuona haya mambo ya kuachana na wachezaji kila baada ya msimu yatapungua, Jjuuko bado ni Jjuuko na hatakua mchezaji mwingine yeyote, ni mlinzi mgumu mwenye kila sababu ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza cha Simba. Halidi Abdulrahman.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *