Ibrahim Ajib, zunguka, kila kukicha mambo mapya

Usajili ni kamari! Usajili ni sawa na kucheza kamari! Yanga ilicheza kamari kwa Ibrahim Ajib, sasa inalipa. Wamelamba dume na Ibrahim Ajib amelamba dume. Usajili wake uliibua shangwe nyingi sana, usingeweza kujua kwa haraka kwanini kelele zile ziliibuka mithili ya mlipuko, tena kwa sauti kubwa kumbe wenyewe walijua walifanyalo.

Kwenye usajili wake kulikuwa na sajili nyingine zilizoambana na usajili huo, kulikuwa na Haruna Niyonzima kwenda Simba, hebu acha kidogo tumuangalie Ajib. Kwenye mchezo wa ligi kuu uliochezwa Jumamosi dhidi ya Kagera Sugar, Ajib alifanikiwa kufunga, siyo kufunga tu, bali alifunga kwenye mchezo ambao Yanga ilishinda kisha kujiongezea pointi tatu kwenye akiba yake ya pointi.

Ni kama vile nyota njema huanza kuonekana majira ya asubuhi, ndivyo ilivyokuwa kwenye mchezo huo, alitoa pasi ya mwisho ya bao la kwanza la Yanga, alimpikia vizuri Obrey Chirwa bila ajizi, Chirwa aliiandikia Yanga bao la kuongoza. Kwahiyo licha tu ya kufunga lakini alitoa pasi ya mwisho ya bao la kwanza la Yanga, kwa kifupi tunasema hivi, alihusika kwenye mabao yote mawili ya timu yake hiyo jana.

Mchezo ukamalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, Ibrahim Ajib aliifungia bao muhimu pia timu yake kwenye mchezo dhidi ya Njombe Mji. Ndiyo, lilikuwa ni bao muhimu sana siku hiyo, alifunga kwa kutokana na mpira uliokufa, alifunga kwa mkwaju wa adhabu ndogo, mpira ulielea hewani hatimaye ukatumbukia nyavuni na kutulia tuli.

Kwenye mchezo huo pia, Yanga iliondoka na pointi tatu, yaani ilishinda kwa bao hilo moja la Ajib. Na Ibrahim Ajib alifanikiwa kufunga kwenye mchezo mwingine ambao Yanga ilifanikiwa kuondoka na pointi tatu uwanjani. Hapa tunaweza kusema aliisaidia Yanga kuondoka na pointi tatu, alifunga bao muhimu sana kwenye mchezo muhimu na mazingira muhimu pia.

Unahitaji kuendelea kuifuatilia simulizi hii tamu na ya kusisimua ya Ibrahim Ajib? Sina shaka jibu ni ndiyo! Mchezo mwingine aliofunga bao muhimu lililoipa Yanga ushindi na kuifanya kuchukua pointi zote tatu ulikuwa ni ule dhidi ya Ndanda, alifunga bao kwenye mchezo mwingine ambao Yanga ishinda na kufanikiwa kuzichukua pointi zote tatu. Nadhani unaanza kumuelewa sasa Ajib ni nani!

Kama nitahitajika kumuelezea Ibrahim Ajib hivi sasa, nitamuelezea kwa njia hii, huyu ni mshambuliaji mwenye mabao matatu ambaye amefunga kwenye mechi tatu ambazo timu yake ya Yanga imefanikiwa kuondoka na pointi zote tatu uwanjani. Unaweza kusema kila anapofunga bao basi ni lazima, Yanga ipate pointi tatu, ndiyo namba hazidanganyi bwana.

Kwa sasa Yanga agizeni soka bariidi hapo dukani kwa Mangi, kisha yaruhusuni mafunda mawili, matatu yateremke taratiibu kwenye koo zenu kujipongeza kufanya usajili muhimu sana msimu huu, usajili uliootesha mizizi kwa haraka, usajili uliokomaza matawi yake haraka na usajili ulipevusha maua yake haraka pia, matunda yameshazaa, yamekomaa, yameiva na sasa yanaliwa kwa raha mustarehe.

Soma pia: Ajib aendelea kurudisha chenji Yanga

Yaani hivi, usajili wake umelipa kwenye klabu ya Yanga, pointi tisa kati ya 13 za Yanga mpaka sasa zimechangiwa pia kwa msaada mkubwa wa mabao ya Ajib. Kama ambavyo usajili huu ulilipusha bomu la kelele nyingi, ndivyo ambavyo usajili wa Haruna Niyonzima ulikuwa, sajili mbili kwenye wakati mmoja lakini mmoja umeshaanza kulipa, ule wa Niyonzima bado unasubiri kidogo muda kisha uanze kulipa.

Si kwamba Niyonzima ni mchezaji asiyeweza kuilipa Simba, hapana nimelinganisha wakati na mafanikio yao kwa wakati uliopo. Tunasema hivi matumizi ya wakati kwenye usajili wenye maneno mengi kama huu, ilikuwa ni lazima Ajib awahakikishie Yanga kwamba hawakukosea kumsajili, hawakukosea kumuamini na ndicho anachokifanya hivi sasa. Hataki mambo mengi, nipe, nikupe, tupeane!

Licha ya kunufaika na usajili wake kwa maana ya mabao, lakini pia Yanga inanufaika na aina ya uchezaji wake uwanjani, mara kwa mara tumekuwa tukishhudia nyota wenye viwango vya dunia wakitumia mipira ya faulo kuzibeba timu zao mabegani mwao, hiki pia kilionekana kwa Ajib kwenye mchezo dhidi ya Njombe Mji. Hii inamaanisha kwamba, kuna kitu kipya kinaanza kukomaa kwenye akili ya Ajib na miguu yake.

Kwasasa atakuwa anawaza hivi, ili niwe mchezaji wa kulipwa nje ya nchi ni lazima niwe na uwezo pia wa kuisaidia timu kwenye mazingira magumu ikiwemo kufunga mabao kutokana na mipira iliyokufa. Huyu ndiye Ajib anayeanza kuzaliwa upya kuelekea kwenye kilele cha mafanikio.

Kitu kingine ambacho Yanga itanufaika nacho kutoka kwa Ajib ni namna anavyoweza kuwa mtoa pasi za mwisho, yaani kuwasetia wenzake kisha wakafunga, Obrey Chirwa kwenye mchezo wa jana aliitumia pasi ya Ajib kama ngazi ya kufunga bao la kwanza la Yanga. Kwa sasa uwezo huu wa kufunga kwa njia zaidi ya moja na kuweza kutoa pasi za mwisho za mabao, acha nimwambie Ajib hivi.

Kila kukicha mambo ni mapya, tumeona upya msimu huu, umefunga kwenye michezo muhimu sana ambayo usingefunga Yanga isingepata pointi tatu, naamini unalifahamu hili ndiyo maana umeamua kuwa mpya, maisha ni mzunguko, jana Simba, leo Yanga kesho TP Mazembe, kila siku ni lazima uwe na kitu tofauti, aidha kizuri au kibaya. Hivyo ni lazima uyakabili kwa namna yatakavyokuja. Mimi Halidi Abdulrahman sijawahi kukikataa kipaji chako, sijawahi kuwa kipofu juu ya kipaji chako, unaweza kuwa mpya zaidi na kucheza zaidi ya hapo ulipo.

Soma pia: Ngassa, kisichong’olewa hakikauki

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *