El Clasico dunia hubadiri muelekeo

image

Kama kuna vitu ambavyo vinaweza kuifanya dunia ijizungushe kinyume na muelekeo wake wa kawaida kwenye mhimili wake na kulizunguka jua hakuna shaka El Clasico itakuwa moja kati vitu hivyo. Kuna wanaoamini mioyo inayowaambia dunia husimama kupisha dakika tisini zenye ufundi na ladha ya soka. Binafsi moyo wangu umezidi idadi ya mapigo ya kawaida yanayostahili ndani ya dakika moja, si kwamba kunaupande uliopewa nafasi kwenye vyumba vya moyo wangu. La hasha, ila ninachokisubiri ni kuona namna ambavyo kichwa kisichoruhusiwa kuota nywele, tai yenye usmati shingoni, suti kali na viatu vinavyo akisi miyale ya mwanga vya Zinedine Zidane namna vitakavyotenganisha urafiki wake na bosi wake Florentino Perez.

Hii ni siku ambayo shughuli ya kumwagilia bustani huweza kukabidhiwa kwa afisa usalama mbele ya Florentino Perez. Hakuna cha maana mbele ya macho yake kama kumuona Cristiano Ronaldo akikimbilia kibendera cha kona huku akipigapiga kifua chake. Hakuna chenye nafasi kubwa moyoni mwake kama furaha ya alama tatu. Haya ndiyo maisha ambayo sina shaka yanamuweka kwenye sintofahamu Zenadina Zidane mpaka sasa. Kila akiangalia kambini kwake anaweza kuhisi hakuna askari anayeweza kuzilinda kiufasaha njia zake, tena mbele ya majasusi wanaozungumza neno moja tu, kuua kisha hufuata kitendo kilichobeba neno lililotamkwa. Zidane hakutakiwa kuzinyoa nyewe zake zote hasa kuelekea kwenye mchezo kama huu, ambao Pep Guardiola hunyoa kwa mkono wake.

image

Kocha wa Real Madrid, Zinadine Zinade.

Sehemu moja ambayo anatakiwa alale akiiota ni pale anapocheza Sergio Busquests. Kama kuna sehemu ambayo Barcelona wanajivunia kuwa nayo, na hii inahusika. Takwimu zinaonyesha kwenye michezo ambayo Barcelona wamemkosa huyu jamaa, imeonekana kuhangaika sana. Lakini kwenye ubora unaoshuhudiwa na nyama za macho ya dunia nzima, ni pale wanapohusika watatu watakatifu, Lionel Messi, Luis Suarez na Neymar. Mbaya zaidi hawa watatu hupika wenyewe na hula wenyewe. Timu inapokuwa kwenye kiwango chake hawa huwa zaidi ya hatari. Ni bora uugue Malaria ila usikumbane na kadhia itakayokufanya utafute sehemu ya kuuweka uso wako.

Wakati umejisahaulisha na kuvaa akili za kuipa Barcelona ushindi kabla ya dakika tisini, hebu kumbuka jambo kidogo jinsi ambavyo Real Madrid amekuwa mbabe wa Barcelona kwenye michezo 171 ya La Liga waliyocheza. Usisahau kwamba Real Madrid imecheka sana kwenye michezo 71. Barcelona hawapo nyuma sana, wameshinda michezo 68 ambayo si haba kuelekea kwenye michezo 172. Historia ya La Liga imewapendelea Real Madrid na hata rekodi ya upachikaji wa mabao pia imesimama kwa Madrid, ambao wamefunga mabao 278 ya La Liga kwenye michezo hiyo sawa na wastani wa mabao 2 (1.63) kwenye kila mchezo. Barcelona nao hawapo nyuma sana, tofauti ya mabao 6 pekee ndiyo inayowafanya waishi nyuma ya Real Madrid. Wastani wa ufungaji wao nao pia ni mabao 2 (1.59) kwenye kila mchezo. Nionavyo mimi mchezo huu hauwezi kuisha bila bao. Lazima bao lipatikane kwa njia yeyote ile.
image

El Clasico ni jina lililobeba uhalisia wa mchezo wenyewe, yaani mchezo bora. Unaweza kuita ‘Classic’ kama jina lenye maana sawa na hilo. Jina hili awali lilikuwa likihusisha michezo ya Barcelona na Real Madrid pale walipokutana kwenye La Liga pekee, yaani Ligi Kuu ya nchini Hispania. Baadae waliamua kuuita jina hilo kila timu hizo zilipokutana. Uhasama wa Barcelona na Real Madrid unaanzia kwenye siasa, itakumbukwa tangu miaka ya1930 na 1936 ambapo Barca kama ndio walizaliwa upya waishi upya maisha mapya. Mpaka sasa Katalunya haina mapenzi makubwa ya dhati na Hispania. Hii ni sababu nyingine inayochochea ladha ya mchezo huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *