Danganya toto! Simba, Yanga ‘zalambwa kisogo’ na Mtibwa

 

Katika kile kinachoonekana kwamba raha jipe mwenyewe na usisubiri kusifiwa, klabu ya Mtibwa Sugar imejigamba kwamba msimu huu ina kikosi bora na cha maangamizi.

Timu hiyo imesema kwamba hivi karibuni ilikutana na ratiba ngumu dhidi ya Yanga na Simba lakini kikosi chao kinaweza kufanya makubwa msimu huu.

Afisa Habari wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru alisema hayo na kusisitiza kwamba dhamira yao msimu huu ni kutwaa taji la Ligi Kuu Bara.

“Kiukweli Mtibwa imedhatiti sana msimu huu, ninaamini tunaweza kufanya makubwa sana msimu huu, hapa karibuni tulikutana na ratiba ngumu dhidi ya Yanga ambayo ni timu bora hapa Tanzania na dhidi ya Simba pia ni timu bora kweli kweli” alisema Kifaru.

Katika hatua nyingine mlinzi wa kikosi hicho, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ ameelezea hali ya kikosi chao hicho na matumaini yake msimu huu.

“Kiukweli msimu huu Mtibwa Sugar ina wachezaji wa kiwango cha juu kabisa hivyo kila mchezaji unayekutana naye anakuwa yuko vizuri sana” alisema Issa Rashid.

Pia, Issa Rashid hakuishia hapo aliongeza kuwa msimu huu Mtibwa Sugar ina uwezo mkubwa sana kila idara na imekamilika hivyo ukiweza kuwakabili washambuliaji wa Mtibwa mazoezini kutokana na ubora wanao uonesha basi unaweza kumkabili mshambuliaji yeyote yule kwenye Ligi Kuu Bara.

“Kila mchezaji msimu huu yuko fiti na naweza kusema kila idara imetimia kwa kifupi tuna kikosi kipana na sisi kama mabeki inatujenga maana tunakutana na washambuliaji bora mazoezini hivyo hii inatujenga sisi na baada ya hapo una uwezo wa kumkabili mshambuliaji yeyote katika ligi kwakuwa kilicho bora umekipata mazoezini” aliongeza Rashid.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *