Barcelona kama paka aliyestaarabika mbele ya Valencia La Liga

image

La liga

Haina haja ya kutumia nguvu nyingi kuipiga jeki pikipiki ili uone  uvunguni kwake. Mkono pekee unatosha.

Ni dakika nyingine ngumu kwa upande wa Valencia ambayo sioni kama ina nguzo imara za ulinzi wa kuweza kuwazuia watakatifu ambao wamevaa kiremba cha ukatili wanapokuwa mbele ya lango.

Hakuna shaka la tone kwamba Valencia wanahitaji kuwa na paa la bati lisilo na tundu hata moja ili kuzuia mvua ya mawe na upepo wa kimbunga kutoka kwa Barcelona.

Wanatakiwa kuimarisha nguvu kwenye kutupa mashambulizi mara kadha wa kadhaa kwani kule nyuma kwa Barcelona kunavujisha mabao ukikata mirija ya mbele yao na kuwafanya wazurure bila malengo.

Ni ngumu kuziishi dakika tisini za maigizo mbele ya Lionel Messi, Luis Suarez na Neymar.

Wakati Valencia wakipanga njia za kuifikia ikulu ya Craudio Bravo, huku Luois Enrique ni kama paka aliyejifanya amestaafu kukamata panya. Atakuwa anaamua tu ni panya yupi anastahili kumeng’enywa na ncha za meno yake.

Kwangu huu mchezo utaamuliwa na ubora wa safu mbili. Kwanza ubora wa ngome ya ulinzi ya Valencia pale watakapopambana na majambazi sugu. Messi, Suarez na Neymar.

Na safu ya kiungo sanjari na ushambuliaji ya Barcelona ambayo ni ngumu kuapa kwamba wanaweza kumaliza dakika tisini bila bao.

Hakuna namna ambayo mchezo huu utakwisha kwa sare au bila bao.

Kama si uwepo wa dakika tisini, ningethubutu kusema Valencia wanakwenda kukoga mvua ya mabao lakini siku zote mpira ni dakika tisini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *