Baada ya kuisimamisha Azam, African Lyon yaigeukia Yanga

Baada ya kuigonga Simba bao 1-0 na kusimamisha Azam wiki iliyopita, African Lyon itashuka dimbani leo kuikakaribisha Yanga katika mechi ya Ligi Kuu Vodacom Tanzania Bara itakayopigwa katika uwanja wa Uhuru.

African Lyon walianza duru la pili kwa kuikomalia Azam na kupata sare tasa katika pambano ambalo kipa wao mahiri Rostand Youthe alifanya kazi ya ziada kuwazuia washambuliaji wa Azam.

Youthe, kipa wa kimatafa wa Cameroon aliumia na kutolewa nje lakini anaweza kusimama langoni leo baada ya kupatiwa matibabu na kuonekana kuwa tayari kwa mikiki ya leo.

Rostand Youthe, kipa mahiri wa African Lyon

Rostand Youthe, kipa mahiri wa African Lyon

Mbali na Youthe, African Lyon itawategemea Hassan Isihaka na Miraj Juma katika safu ya ulinzi huku chipukizi Abdullah Mguhi akitarajiwa kuonesha kiwango kizuri kama alivyofanya dhidi ya Azam.

Katika pambano la duru la kwanza, African Lyon inayoshikilia nafasi ya 11 baada ya kujikusanyia pointi 19 katika michezo 16 walibamizwa mabao 3-0.

Kwa upande wa Yanga wanashuka dimbani wakiwa katika nafasi ya pili na pointi 36,  pointi mbili nyuma ya vinara Simba. Ushindi katika pambano la leo utawarudisha kileleni kwa tofauti ya pointi moja.

Kocha wa Yanga, George Lwandamina atakuwa huru kumtumia Justine Zulu baada ya kushindwa kucheza dhidi ya JKT Ruvu kutokana na awali kukosa kibali cha kufanya kazi nchini.

 

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *