Yanga kucheka tena leo?

Kikosi cha Yanga

Milango ya saa 10:30 katika dimba maridhawa la taifa, mabingwa mara 26 wa ligi kuu Tanzania bara watakuwa wenyeji wa Mbeya City katika mchezo wao wa raundi ya pili kukamilisha mzunguko wa 28 wa ligi hiyo ikielekea ukingoni.

Ni mtanange ambao unabeba hisia za wengi kutokana na ushindani mkali uliopo kati ya Yanga SC na Simba SC kuwania taji la ligi kuu msimu huu . Wawili hao wamekuwa wakifukuzana vilivyo kileleni mwa ligi kutokana na tofauti ndogo ya alama zao huku wanajangwani wakichagizwa na wingi wa magoli yao ya kufunga.

Simba SC wamerudi jana kileleni baada ya kuwabamiza 2-1 Stendi United na kufikisha alama 65 ikiwa ni pungufu ya alama 62 alizonazo Yanga lakini akiwa na michezo mitatu mkononi kuanzia huu wa leo dhidi ya Mbeya City ilihali Simba wakibakiza mchezo mmoja tu.

Licha ya kusaka alama tatu leo ili kujiweka sawa kwenye mbio zake za ubingwa , Yanga SC wanaingia kwenye mchezo huu wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kukubali kichapo cha goli 2-1 katika mzunguko wa kwanza jijini Mbeya . Hivyo kisaikolojia ni mechi ambayo itakuwa na upinzani mkali katika dhana nzima ya kulipa kisasi pia Mbeya wakitaka kulinda heshima yao.

George Lwandamina kocha mkuu wa Yanga SC sanjari na msaidizi wake hivi karibuni wamekuwa vyema kimbinu na kiufundi katika kuandaa timu ya ushindi kwa kusaka matokeo pia soka safi kitu ambacho kitawafanya Mbeya City kuingia uwanjani na tahadhari zote.

Kwa misimu kadhaa mfumo wa ushambuliaji wa Yanga SC ulikuwa ukitegemea sana wings zake kujenga mashambulizi ya hatari na eneo la kiungo cha kati kubaki kama sehemu ya kuziba njia kwa mpinzani lakini sio njia rasmi ya kushambulia kwa klabu hiyo kama central channel ( direct play ) kwa pasi fupi fupi za kazi zinazohama box moja kwenda jingine .

Matumizi ya full backs na mawinga ndio ulikuwa mtaji mkuu wa kushambulia kwa Yanga SC lakini hivi sasa unaiona timu inashambulia pande zote kutokana na kubadilika kimbinu na wachezaji kuimarika katika viwango vyao.

Matumizi ya viungo Thabani Kamusoko na Haruna Niyonzima eneo la kati limeifanya Yanga SC kuwa tishio eneo la kiungo katika kukaba na kuanzisha mashambulizi hususani kwa mfumo wao wa 4-4-2 .

Thabani Kamusoko na Haruna Niyonzima watageuka target kwa Mbeya City leo kutaka kuzima kasi ya mashambulizi ya Yanga SC . Ni dhahiri watataka kutenganisha muunganiko huu endapo Lwandamina atataka kuwatumia wote kikosi cha kwanza ili kupunguza tactical pressing ya Yanga SC kati na kwenye wings zake .

Kwa fununu tu kikosi cha Mbeya City kimepandisha kijana wa kikosi cha pili ambaye huenda leo akasimama eneo la kati dhima kuu ikiwa kusaidiana vyema na wakongwe kina Keny Ally kuvunja ngome ya Yanga SC eneo la kati hususani kutafuta mchezaji ambaye muda wote atakuwa akitembea na Haruna Niyonzima ili kuvunja mfumo wa utoaji pasi za mwisho za Yanga SC kwenye safu ya ushambuliaji.

Ni tahadhari nzuri kimbinu na ni dhahiri Mbeya City watajipanga kucheza ‘ double sic ‘ kwa kuweka viungo wawili kati ambao wana uwezo mzuri kukaba ili kuvunja mipango ya Yanga kati pia kuanzisha mashambulizi ya kasi kwenda mbele ( double pivot ).

Nimekuwa nikifatilia kwa ukaribu mzuri mazoezi ya Mbeya City kuelekea mchezo huu na nikagundua huenda leo Zahoro Pazi na Mrisho Ngasa wakaanzia benchi kwenye safu ya ushambuliaji wa timu hiyo na Nchimbi kuongoza mashambulizi. Huenda hii ni tactical deception plan kwa Yanga SC .

Yaani ukawa ni mpango wa kuwadanganya Yanga SC kutumia muda mwingi kuona watazima vipi kasi ya Zahoro Pasi na Mrisho Ngasa halafu wakaletewa kombinesheni nyingine na wawili hao kusimama kama plan B baadae.

Walinzi wa kati wa Yanga SC watahitajika kuwa makini kuelekea mchezo huu kutokana na mabadiliko yoyote kimfumo kwa Mbeya City. Mchezo uliopita licha kucheza vyema Nadir na Yondani lakini kuna wakati walikuwa wakikosa maelewano mazuri na matumizi makubwa ya nguvu yasiyo na lazima.

Mbeya City ni wajanja sana wanapokaribia lango na wazuri kwenye kujaribu mashuti ya mbali hivyo umakini katika kuufinya uwanja na kuziba njia uwepo kwa walinzi hao.

Geofrey Mwashuiya amekuwa katika kiwango kizuri hivi karibuni na kuingia kikosi cha kwanza kwa klabu ya Yanga . Ana uwezo mzuri wa kukas na mpira , kukokota kwa kasi kwa ajili ya pressing pia kuwapanga wenzake kati kwa ajili ya krosi au pasi nzuri za mwisho lakini bado ana tatizo la kuachia mpira kwa wakati .

Kimbinu na kiufundi dribblers au wakokotaki kwa lugha yetu adhimu ni rahisi sana kuwakaba kwa kuziba njia zao hivyo Mwashuiya kwa muongozo wa benchi la ufundi yampasa kuchukua tahadhari na kuendana vyema na patterns za timu katika kushambulia.

Mbeya City si timu ya kubeza hata kidogo. Wana alama 32 katika msimamo wa ligi kitu ambacho kinawafanya bado kuwa katika hatari ya kushuka daraja. Katika msimamo wa ligi timu ambayo ipo juu ya alama 35 ndio ipo salama mpaka sasa hivyo mchezo wa leo watatoa ushindani mkali kwa wakali hao wa jangwani .

Ikumbukwe mchezo wao wa mwisho watamaliza na Majimaji FC mkoani Ruvuma na wanalizombe hao wapo katika hatari ya kushuka daraja. Mchanganuo huu ni dhahiri MCC leo wapo taifa kiushindani na sio kukamilisha ratiba.

Na Samuel Samuel

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *