Waliohamia timu mpya waanza kuleta balaa Ligi Kuu

Wale wachezaji waliotolewa kwa mkopo na waliozihama timu zao kwenye kipindi cha dirisha dogo, wameanza kuzitumikia timu zao mpya katika mzunguko wa lala salama wa Ligi Kuu Vodacom Tanzania Bara.
Baadhi ya walioanza maisha mapya ni Juma Kaseja ambaye awali alikuwa Mbeya City na akapumzika kidogo kucheza soka, lakini kwa sasa amejiunga na Kagera Sugar. Ameanza kukaa golini kwa takribani mechi mbili sasa, hadi raundi hii ya 18.
Pastroy Athanas, straika wa zamani wa Stand United, yeye ameanza maisha mapya kwenye klabu ya Simba na kwa bahati nzuri ameonekana kuwa chaguo kwenye kikosi cha kwanza.
Emmanuel Martin, straika kutoka JKU ya Zanzibar naye ameanza kuitumikia klabu ya Yanga na kwa bahati nzuri, amekuwa akipata namba ya kucheza.
Kati ya hao, wapo ambao wamejiunga klabu mpya na kuanza kufunga magoli kiasi cha kuanza kuzikumbusha klabu zao za zamani kuwa hawakuwa sahihi kuwaacha, kuwauza au kuwatoa kwa mkopo.

1. Awadh Juma-Mwadui

Amejiunga na Mwadui kwa mkopo akitokea klabu ya Simba. Tayari amepachika mabao mawili katika mechi tatu alizocheza mara tu baada ya kujiunga na klabu hiyo mpya na kupata namba.
Msimu huu hakupata kabisa nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha Simba, chini ya Mcameroon, Joseph Omog hivyo kufikia uamuzi wa kutolewa kwa mkopo.


Awadhi_Juma


Desemba 31 mwaka jana, alifunga goli ambalo liliifanya timu yake hiyo kuondoka uwanjani na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar.
Hadi anakopeshwa, alikuwa hajafunga goli lolote na klabu ya Simba kutokana na kutocheza.

2. Venance Ludovic-Lyon

Ingawa amekatiwa rufaa na klabu yake ya Mbao kuwa hakuhamishwa kihalali, lakini tayari ameshaanza kuleta balaa kwenye Ligi Kuu, kwa kuifungia African Lyon goli moja.
Goli hilo alilifunga Desemba 23 mwaka jana, Yanga ikilazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Lyon. Goli hilo linamfanya kutimiza magoli matano kwenye orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
Magoli manne aliyafunga akiwa na klabu yake ya zamani Mbao FC, kabla ya kuhama kutokana na kile ambacho mwenye anadai kuwa timu yake hiyo haijamlipa mishahara wake wa zaidi ya miezi miezi mitatu, hivyo kwa mujibu wa mkataba wao ni kwamba umeshavunjika.

3. Tito Okello-Mbeya City

Amejiunga na Mbeya City kwenye kipindi hiki cha dirisha dogo akitokea African Lyon.  Tayari pia ameshaifungia timu yake hiyo mpya bao moja.
Goli hilo alilifunga Desemba 31 mwaka jana, Mbeya City ikiichapa Mbao mabao 3-1. Alifunga kwa mkwaju wa penalti baada ya yeye mwenyewe kuangushwa ndani ya eneo la hatari.
Amefikisha idadi ya magoli manne ya kufunga, matatu akiyafunga msimu huu kwenye nusu ya kwanza ya ligi akiwa na timu yake ya African Lyon.


Tito Okello_action_Mbeya


Ikumbukwe kuwa Okello alijiunga na Mbeya City kwa mbinde, baada ya Lyon kumuwekea kauzibe kwa kudai kuwa ni mchezaji wao. Hata hivyo, ilidaiwa kuwa mchezaji huyo raia ya Uganda na wenzaake wawili, Hood Mayanja na Otong William waliichezea Lyon bila mikataba kama wachezaji wa ridhaa, hivyo walikuwa huru kuingia mkataba na timu hiyo mpya.

4. Zahoro Pazi-Mbeya City

Ni mchezaji wa zamani wa klabu za Simba na JKT Ruvu. Muda mrefu alikuwa hapa nchini baada ya dili lake la kwenda kucheza soka la kulipwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kushindikana.
Ili kucheza alihitaji uhamisho wa kimataifa (ITC), kutokana na kwamba tayari Shirikisho la Soka Nchini (TFF) lilishautuma, hivyo haingewezekana kucheza soka nchini bila kibali hicho. Ilibidi rais wa TFF, Jamal Malinzi atumie juhudi za makusudi kumsaidia kijana huyo na hatimaye mambo yakanyooka.


Zahoro Pazi akiwajibika uwanjani katika timu yake ya Mbeya City. ( Picha/ Mbeya City )

Zahoro Pazi akiwajibika uwanjani katika timu yake ya Mbeya City. ( Picha/ Mbeya City )


Na katika kuthibitisha kuwa alikuwa na hasira, mechi yake ya kwanza tu akiwa na timu ya Mbeya City, alifunga bao kali kwa shuti la mbali lililokwenda moja kwa moja hadi wavuni kwenye dakika ya 80, likiwa ni la tatu kwenye mechi hiyo. Ilikuwa ni mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Mbao FC, Mbeya City, ikishinda mabao 3-1.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *