Tujikumbushe: Figo aliporushiwa kichwa cha nguruwe

Figo_kichwa
Tarehe kama ya leo mwaka 2002 Luis Figo alirejea Nou Camp kama mchezaji wa Real Madrid na kukaribishwa kwa balaa la kuzomewa na hadi kufikia kurushiwa kichwa cha nguruwe na mashabiki wa Barcelona.
Kichwa hicho cha nguruwe kilichojaa damu kilirushwa kwa Luis Figo wakati akipiga kona upande wa mashabiki wa Barcelona waliokuwa wakimtuhumu kwa dhambi kubwa ya usaliti wa kuiacha timu yao na kujiunga kwa mahasimu wao wakubwa.
Figo alikuwa kipenzi kikubwa cha mashabiki wa Barcelona, jina lake lilimbwa katika dimba la Nou Camp enzi hizo akiwakosesha usingizi walinzi kwa kasi na chenga. Alichangia ushindi. Alileta ushindi. Alisababisha ushindi na kuleta burudani kwa wapenzi wa Barca.
Aliwavuruga kabisa mashabiki wa Hispania, sio tu Barcelona alipohamia Real Madrid kwa kitita cha pauni milioni 37 ambacho kilivunja rekodi ya dunia kwa wakati huo.
Barcelona walichukulia kama usaliti wa hali ya juu wa mioyo yao. Kwao ulikuwa ni usaliti usiovumilika. Kulipa kisasi kwa aina yoyote ile ikiwemo kumzomea, kumrushia vitu dimbani na hatimaye kumrushia kichwa cha nguruwe ilikuwa ni sawa kabisa.
Hali ilikuwa mbaya kiasi cha mwamuzi kusimamisha pambano kwa dakika 16 kabla ya kuendelea na hatimaye kumalizika kwa sare tasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *