Tshishimbi nakuita kwa maudhi itikia kwa miguu

Ni majina mapya ya wachezaji wanane pekee yaliyopata bahati ya kusajiliwa na kikosi cha Yanga msimu huu. Kati ya majina hayo, majina mawili yalitembea sana vichwani vya watu wengi. jina moja lilikuwa maarufu lakini jina jingine lilikuwa linavutia kulitamka zaidi ya lile jina maarufu na majina mengine yote yaliyosalia.

Jina lililokuwa maarufu lilikuwa ni la Ibrahim Ajib na jina lililovutia lilikuwa ni la Pappy Kabamba Tshishimbi. Hili lilikuwa linavutia sana kulitamka kama lilivyokuwa linavutia jina la Vincent Boussou. Majina haya yalipendwa zaidi na mdomo kuliko macho. Yalivutiwa zaidi na ndimi za watu kuliko mboni zao. Ndiyo mana ilikuwa rahisi kuwafananisha na wale wana muziki wa Kikongomani wanaoimba Bolingo kuliko kuwafikiria uwezo wao uwanjani. Tuwaombe radhi.

Nilikuwa nayaangalia majina haya mawili kwenye mchezo wa ligi kuu siku ya Jumamosi dhidi ya Ndanda kwenye Uwanja wa Uhuru. Mambo mawili yaliwahusu kwa ukaribu sana. Pappy atavaa uhusika wa kina Youthe Rostand, Obrey Chirwa, Donald Ngoma, Amissi Tambwe na wachezaji wote wa kigeni kwenye Ligi kuu. Kwanza tuwaombe radhi, wakati ukipigwa na butwaa naomba nimbebeshe Ajib mzigo huu kisha nitaomba autue kabla safari haijafika mwisho.

Ajib atavaa uhusika wa kina Gadiel Michael, Abdallah Shaibu, Pius Buswita na wachezaji wote waliozaliwa ndani ya nchi ya nchi inayoongozwa na Rais Magufuli. Huyu alifunga bao kwenye mchezo ule lakini hakumaliza dakika tisini. Obrey Chirwa alimaliza dakika tisini. Hivi umewahi kujiuliza thamani ya miguu ya Ajib?

Ibrahim Ajib akipiga hesabu za kumtoka William Lucian ‘ Gallas’ wa Ndanda

Mwenyewe anaijua thamani ya miguu yake? Huyu ni moja kati ya wachezaji wenye vijaji sana, anaweza kukokota mpira na kuufanya atakavyo mithili ya ufalme wa mkaanga samaki mbele ya kikaango. Angeweza kutulisha samaki wenye ladha tofauti tofauti na kujitengenezea ufalme wake.

Yupo, bado yupo tu. Nidhamu ya upambanaji kwa upande wake sijui tuipe asilimia ngapi. Wakati huohuo vitazame viatu vya Obrey Chirwa vinavyoaibika kuifunika miguu isiyoweza kuutawala mpira kwa kiwango cha juu kama ilivyo kwa Ajib. Kinachovifanya viendelee kuishika ngozi yake ni kwamba havijawahi kumuangusha linapokuja suala la nidhamu ya upambanaji. Haviangushi viatu vyake hata mara moja ndiyo maana alisaliwa Yanga na alicheza dakika tisini kwenye mchezo ule. Unadhani Ajib alimaliza kazi yake au Lwandamina alitaka kufanya mzunguko wa kikosi kwa kumuingiza Mwashiuya? Hapana.

Obrey Chirwa akiwania mpira na William Gallas

Hawa wachezaji wa kigeni tunawabeza sana, hatuwapi heshima zao kama inavyostahili. Tunapaswa kuwaomba radhi, nasisitiza wanastahili kuombwa radhi. Tunawaita majina yasiyofaa,  Pappy Tshishimbi atakuwa mfano mzuri sana, tulimwita Shishi baby, wenye hekima wakamwita Shishi boy. Bila hawa tutakuwa na ligi yenye uhaba wa wapamanaji, isiyo na changamoto.

Nakuita Tshishimbi kwa sauti na lugha yenye maudhi, naomba usifungue mdomo wako kuitikia, utapoteza sauti yako, niitikie kwa miguu yako, mpelekee salam hizi na Obrey Chirwa.

Kupata odds bora zaidi 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *