Tshabalala anapoamua kuwa straika Simba

Mohamed_Hussein

Washambuliaji wa Simba wanatia huruma. Wanakosa magoli mengi sana yanayowashangaza wengi. Nadhani Simba ndiyo timu inayoongoza kwa kutengeneza nafasi nyingi za kufunga. Lakini mastraika wao wanawaangusha.

Bado kina Laudit Mavugo, Fredrick Blagnon, Ibrahim Ajibu na hata hawa waliosajiliwa kwenye kipindi cha dirisha dogo, Juma Luzio na Pastory Athanas, hawajaweza kutibu tatizo la ufungaji ndani ya kikosi hicho.

Simba ya sasa ina kipa mzuri, mabeki wazuri na hata viungo, lakini inachokosa ni mastraika sahihi wa kutumia nafasi chache zinazopatikana.

Sijaua tatizo ni nini. Ni viongozi wa klabu hiyo kusajili mastraika wasio sahihi ndani ya klabu hiyo kubwa? Au ni wachezaji wenyewe kushindwa kujua majukumu yao ndani ya klabu hiyo yenye presha kubwa ya mashabiki?


Juma Liuzio

Juma Liuzio


Wiki iliyopita niliandika makala kuhusu mchezaji Okwi anavyoshangiliwa ndani ya kikosi hicho kabla hata haijatakwa kama atatua Simba. Ni kwa sababu ameifanyia makubwa klabu hiyo, huku kwa sasa mastraika wake wakishindwa kufanya kile ambacho kitawafanya wakumbukwe kwa mema walioifanyia klabu hiyo kama Okwi.

Siku chache baada ya makala hiyo, Simba ilikwenda kucheza mechi ya Kombe la Shirikisho la Soka (TFF), maarufu kama Kombe la FA.

Ni kombe ambalo bingwa anaiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF). Wekundu hao wa Msimbazi walicheza na timu ya Polisi Dar es Salaam na kushinda kwa mabao 2-0.

Kama kawaida yao, mastraika wa timu hiyo walikosa magoli mengi ya wazi na kusababisha mashabiki wa timu hiyo kutumia muda mwingi kunung’unika badala ya kushangilia timu yao.

Pamoja na Pastory kufunga bao, lakini bado mashabiki wa timu hiyo walikuwa roho juu muda wote kuwa goli hilo linaweza kurudishwa.

Si kwa sababu mabeki wa timu hiyo walikuwa nyanya, ila ni kwa sababu mastraika walikuwa wanakosa magoli ambayo yangesababisha kutokuwa na wasiwasi tena, hata kama Polisi wangepata bao moja.

Ndipo ilipokuja dakika ambayo beki Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ alipowafundisha mastraika wa Simba jinsi magoli yanavyofungwa. Aliuvunja mtego wa kuotea ambao siku zote mastraika wa Simba huwa hawawezi kufanya hivyo.


Mavugo


Kama utakumbuka hata kwenye Kombe la Mapinduzi Zanzibar kwenye mechi dhidi ya Taifa Jang’ombe, mastraika wa Simba walishindwa kabisa kutegua mtego wa kuotea na mabeki wa timu hiyo, hadi kiungo Muzamir Yassin alipofanya hivyo.

Tshabalala, ambaye ni beki wa kushoto aliuvaa ushambuliaji. Aliuona mpira mrefu uliopigwa kutoka pembeni na kuchomoka nyuma ya mabeki wa Polisi. Akaukimbilia huku akimpigia hesabu kipa alivyokuwa anatoka. Akauwahi na kumpira kanzu.

Kwa straika yoyote wasiwasi angesimama na kuusubiri utinge wavuni. Lakini uligonga mwamba na kurejea uwanjani. Mara nyingi tunaona baadhi ya mastraika wakishika vichwa na kusikitika mpira unapogonga mwamba na kurejea uwanjani.

Tshabalala hakufanya hivyo. Alipoupiga, macho yake yalikuwa yakiusindikiza mpira kama unatinga wavuni au la. Ulipogonga mwamba, aliutazama unarudia wapi na haraka akaukimbilia, kitendo bila kuchelewa akaupigwa kichwa ukatinga wavuni na kumuacha kipa wa Polisi akihangaika kuuokoa bila mafanikio.

Tshabalala anastahili sifa. Kwa jinsi alivyofunga goli lile, aliuvaa ustraika moja kwa moja. Ni goli gumu, kuliko yake wanaokosa mastraika wake. Sina uhakika kama straika yoyote wa Simba pale angeweza kufunga goli la aina hiyo.

Kama wanakosa magoli rahisi zaidi kupata kuliko kukosa, sidhani kama wangefanikiwa kufunga goli kama lile lililoihangaisha zaidi mwili, akili na ujanja wa mfungaji.

Moyoni, nadhani mastraika wa Simba watakuwa wanaona aibu kwa goli hilo. Ingawa si vibaya na si ajabu kwa mabeki kufunga magoli, kwani tunaona hata Ulaya kina Sergio Ramos wanafunga sana magoli, lakini wanafanya hivyo huku safu zao za ushambuliaji zikiwa zinafanya kazi zao kama kawaida.

Lakini kwa Simba hivi sasa imakuwa kama ni mbadala. Kwani awali viungo ndiyo waliokuwa wanafunga, wao wakisuasua, ikidhaniwa kuwa ni kipindi cha mpito.

Sasa imefikia wakati hata mabeki wameshagundua kuwa inabidi na wao waende mbele kutafuta magoli, la sivyo hawawezi kuibuka na ushindi kwani mastraika wao ni matatizo matupu.

Goli lile si habari nzuri kwa mastraika, kwani sasa mashabiki wataamini kuwa wanapata mishahara wa bure na hakuna kitu wanachofanya.

Lakini pia goli la Tshabalala linaweza kuwa somo na ni kengele ya kuifanya safu ya ushambuliaji kushtuka na kujitathmini upya juu ya mchango wao kwenye klabu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *