Tathmini ya Azam dhidi ya Simba

Simba_squad

Ni saa chache kabla ya kukutana kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi na Azam kufanikiwa kuifunga Simba kwenye mchezo huo.

Simba ikiwa kileleni mwa msimamo wa ligi kuu Bara kwa pointi 45 ilitoka sare ya bila kufungana na Mtibwa Sugar siku ya Jumatano jioni huku Azam ikilazimishwa sare kama hiyo na Mbeya City siku hiyohiyo usiku.

Simba ndiyo timu iliyofungwa mabao machache kuliko timu zote za ligi kuu ikiwa imefungwa mabao 6 tu huku ikiwa timu ya pili kwa kufunga mabao mengi nyuma ya Yanga iliyofunga mabao 40 huku wenyewe wakifunga mabao 30.

Azam wametoa sare ya tano msimu huu ikiwa imeruhusu mabao 15 na kufunga mabao 23 tu huku straika wake John Bocco akichangia mabao sita peke yake.

FALSAFA YA AZAM NA MBINU ZA IDD CHECHE.

Tangu aiongoze timu hiyo imeonekana kuimarika mno kwenye eneo la ulinzi kwani haijaruhusu bao kwenye michezo sita iliyocheza mpaka sasa. Kwenye makaratasi wanaonekana kutumia 4-4-2 wakati mwingine 3-5-2.

Mara kwa mara huanza mpira kwa taratibu kuanzia kwenye eneo lao la ulinzi na wanapofika kwenye kiungo kasi huongezeka, mbinu hii hutumiwa na mdudu aina ya nyoka kumjeruhi adui yake.

Wanahitajika kutumia mfumo wa 3-5-2 au 4-4-2 ‘diamond’ ili kuwa na viungo wengi wa kati ambao watawazidi viungo wa Simba na kusababisha giza kati yao hali itakayowapelekea kutoonana kirahisi.

Hii itafuatia baada ya Gadiel Michael, Yahya Mohammed, Aggrey Morris na Shomari Kapombe kuanzia kwa lile umbo lao walilokuwa wakilitengeneza dhidi ya Mbeya City, yaani umbo la Trapeza litakalowaweka washambuliaji wa Simba, Mavugo na Juma Liuzio katikati yao.

Hali hii itawafanya kutotembea au kukimbia na mpira kwa faida katikati yao hapo watakuwa wamewafanya kuzurura pasipo na malengo uwanjani.

Ni lazima wahakikishe wanakuwa na mawasiliano kati ya John Bocco na straika mwenzake nambari mbili kwani kwenye mchezo dhidi ya Mbeya City walionekana kufanya majukumu wote kwa pamoja bila kuachiana nafasi.

Ni muhimu mno kuhakikisha ule mpira unaodondoka baada ya walinzi wa kati wa Simba, Abdi Banda na Method Mwanjali wanauwahi wao ili kujipatia mabao badala ya kuondoshwa na walinzi hao.

SIMBA NA MBINU ZAO.

Wanatumia 4-4-2 siku hizi lakini wana utajiri mno wa viungo.

Mbinu niliyoitaja hapo juu kwa Azam ni hiyohiyo inayoweza kutumika kwa Simba kwa kuwa mpira wao unafanana fanana. Wana Mohammed Hussein, huku Azam wana Shomari Kapombe.

Tatizo lao ni lilelile la kutotumia straika wa kati kujipatia mabao, ni lazima wahakikishe eneo la kati la uwanja linakuwa kwenye umiliki wao ili kushinda mchezo kwa kuwa asilimia kubwa ya mabao yao yamezalishwa na viungo.

Atakayepashinda katikati mwa uwanja, atashinda mechi yenyewe!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *