Singida United sio mbeleko ya Kariakoo

Kwanini mnakuwa na mtizamo hasi juu ya Singida United kugeuka mbeleko ya Yanga SC ligi kuu msimu ujao kisa uwepo wa mheshimiwa Mwigulu Nchemba?!

Ngoja niwakumbushe ujio wa Azam FC ligi kuu na mitazamo waliyokuwa wakipewa na hawa hawa wadau wa soka nchini wenye mtazamo hasi juu ya timu mpya ligi ambazo kwa sehemu zinaonesha unasaba na vigogo wa Kariakoo.

Ilipoingia ligi kuu Azam FC msimu wa 2008-9 wengi walisema ni tawi la Simba SC kutokana na wengi wa viongozi wake kuwa mashabiki wa Simba na baadhi kuwemo katika lile kundi maarufu la Friends of Simba SC.

Propaganda hizi za wafalme wa Kariakoo hazikufua dafu kwa uongozi wa Azam FC . Waliingia kwenye ligi kwa dhamira ya ushindani kwa kila timu mbele yao .

Katika miaka 9 ya Azam FC ligi kuu , imekuwa mwiba mkali kwa Simba SC ambao walinadiwa kuwa ni tawi lao . Ujio wao umewatoa Simba kwenye harakati za kuchukua ubingwa wa ligi kuu pia kucheza michezo ya kimataifa kwa kujipenyeza katikati yao na mahasimu wao wakubwa Yanga SC .

Katika miaka 5 ya Simba kupotea kimataifa kuna miaka 9 ya Azam katika ujio wao ligi kuu wakiwa na kombe la ligi kuu 2013-14 , Kagame Cup na mapinduzi Cup.

Hii ina maana timu ikijipanga inaweza kukaa mbali na hizi propaganda za kugeuka tawi na kufanya vyema kwenye ligi.

Wanakazana kusema Singida United itapotea kwa kugeuka tawi la Yanga mie nadhani wachukue mfano wa Azam FC katika hili. Singida United wanawekeza pesa nyingi na nguvu kubwa katika timu yao kwa kuyataka mafaniko ya ligi na kisoka kiujumla sio kugeuka nguzo ya mtu mwingine kufanikiwa .

Binafsi niseme wazi Singida United wamejipanga vyema kuwa timu ya ushindani kwa timu zote ligi kuu pia kulikamata soko la soka nchini kwa taratibu za chini ya kapeti ambazo wanaziandaa kuuza bidhaa zao.

 

By Samuel Samuel

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *