Niyonzima, ahsante kwa kuzifungua kurasa ngumu za kitabu cha ‘Mchawi Mweusi’

Niyonzima_o2

Ili uishi marefu ni lazima ufuate miiko ya maisha. Haruna Niyonzima ni moja kati ya wachezaji wa kulipwa wanaozitendea haki shilingi za kitanzania hapa nchini.

Ulishuhudia alichokifanya? Alipotolewa Amissi Tambwe kwenye eneo la ushambuliaji, aliingia Said Juma Makapu ambaye ni kiungo asilia wa ulinzi.

Kilichofuata ni Haruna Niyonzima kupanda juu kucheza kama mshambuliaji namba mbili mwenye majukumu ya kumlisha Ngoma, Msuva na Kaseke waliokuwa wakitokea pembeni na kuitanua idara ya ulinzi ya JKT Ruvu.

Kwa kuwa Niyonzima ni mzuri sana wa kupiga pasi za mwisho zenye madhara, haikuwa ngumu kwa George Lwandamina kufanya mabadiliko hayo na kumruhusu Niyonzima kuufungua ukurasa wa Mchawi Mweusi.

Ni nani huyu Mchawi Mweusi? Huyu ni Bakari Shime kocha wa JKT Ruvu ambaye aliingia kwa kukaba mno hasa kwenye idara yake ya ulinzi iliyokuwa na nidhamu mno ya ukabaji kwenye kipindi cha kwanza.

Tulishuhudia sana Msuva na Kaseke wakitumika katika kupandisha mashambulizi. Nidhamu kubwa ya Michael Aidan, Edward Charles na wenziwe ilianza kushuka mara tu baada ya Niyonzima kusogea juu na sekunde chache tu Msuva akapata bao.

Niyonzima ndiye aliyekuwa ‘Playmaker’ wa Yanga siku ya leo.

Licha ya kutocheza vizuri kipindi cha kwanza, Yanga walistahili ushindi kwenye mchezo wa leo.

Ndiyo maana baada ya mchezo kocha Lwandamina aliandika kwenye akaunti yake juu ya vijana wa Yanga kushinda.

Lwandamina alisema “Vijana walistahili ushindi” ni kweli. JKT Ruvu hawakuonekana kuwa na mipango hasilia ya kutafuta ushindi ikiwemo kushindwa kuutumia uwazi katikati ya Vincent Bossou na Kelvin Yondani ambao mara kwa mara walikuwa wakiacha uwazi katikati yao.

Donald Ngoma hakuwa kwenye kiwango cha juu, Ngoma tuliyemzoea si yule tuliyemuona, hakuwa mzuri kwenye makadirio wala umakini ndiyo maana ilikuwa rahisi mno kwake kutoipatia Yanga mabao.

Hata hivyo ubora wa Bakari Shime kwenye kuitengeneza safu yake ya ulinzi ndicho chanzo kingine cha kutokuwa na ubora kwa Ngoma, ulipotua mpira walikuwepo kina Aidan na wenzie, walikaba na kucheza kwenye nafasi na kutoruhusu Yanga kutembea na mipira kuelekea kwenye eneo lao la ulinzi.

Ndiyo maana ninasema, ahsante sana Haruna Niyonzima kwa kukifungua kitabu cha ‘Mchawi Mweusi’ Bakari Shime. Hata kama huupendi mpira na huipendi Yanga, lazima utazipenda tu pasi za Niyonzima, mijongeo yake na namna anavyofungua kurasa ngumu kusomeka na kuzilainisha. Niyonzima utaishi maisha marefu ya mpira, sijawahi kuwa mtabiri ila acha tuamini kwamba ukifuata miiko ya maisha, utaishi maisha marefu yenye starehe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *