Niliyoyaona Nou Camp Guardiola akinyanyaswa na kinyago alichokichonga mwenyewe

FB_IMG_1476946147070

Barcelona 4-0 Manchester City

1. Tofauti kati ya Barcelona na Manchester City ilikuwa ni LIONEL MESSI, huyu ndiye aliyeleta dhahama yote kwa City magoli matatu na pasi ya goli la nne ndivyo vinavyomtenganisha yeye na wachezaji wengine 21 waliokuwa uwanjani. “Hat-trick” ya 41 kwake huku pia akifikisha magoli 50 ndani ya Nou Camp (hakuna mchezaji mwingine aliyewahi kufikisha zaidi ya magoli 46 ndani ya kiwanja kimoja kwenye UCL).

2. Andre Iniesta, almaarufu “El Cerebro” ama kwa lugha yetu ni “ubongo” na kama tunavyojua kazi ya ubongo kwenye mwili wa mwanadamu basi ndivyo ilivyo kwa huyu jamaa, fundi, mkali, mjuaji, mtaalam na majina mengine kama hayo. Nyuma ya umahiri wa Barcelona na MSN ni huyu mjuzi wa soka.

3. Barcelona ni mahiri katika kushambulia lakini pia wanafungika, kama ambavyo ni ngumu kupewa kila kitu maishani basi ndivyo klabu hii ya Catalunya ilivyo, bado beki ya Barca ni mbovu ingawa unahitaji kuwa bora ili kuwafunga. Na ubovu wao ulidhihirishwa na kadi nyekundu ya kijinga kabisa aliyoonyeshwa Jeremy Mathieu

4. Ter Stegen, huyu dogo nimemwelewa sana, leo ni kama alikuwa anamwonyesha Bravo kwamba ni kweli alistahili kuuzwa kwa sababu angebaki kusugua benchi tu pale Barcelona. Bonge ya kipa tena katika umri mdogo wa miaka 24. Inaoenekana dhahiri Ujerumani ni kiwanda kizuri cha makipa.

5. Anatoka Andres anaingia Andre, katika umri wa miaka 23 kijana Andre Gomez anaonekana kuifanya kesho ya Barcelona ing’are. Ukimtazama alivyocheza leo ni kama kusema mashabiki walikuwa wanamtazama Iniesta mwingine lakini mrefu zaidi.

6. Pep Guardiola pole sana, najua ulikuwa unajua kuhusu Messi, miaka kadha wa kadha ulimtumia huyu kuwaumiza wengine hebu na wewe endelea kupata maumivu yale yale uliyowasababishia wengine. Pep alijua tu namna ya kumfanya Messi awe bora lakini nafikiri hajawahi kufahamu namna ya kumzuia.

7. Manchester City inaelekea kuzuri, ukiachana na matokeo ya mchezo wenyewe City walionyesha uhai kwa sehemu kubwa ya mchezo kabla ya Bravo kuonyesha kadi nyekundu na hata mpaka kuwazidi Barcelona kumiliki mpira (possesions) wakati mwingine kitu ambacho sio cha kawaida ukicheza dhidi ya Barca. Kesho ya Guardiola na City itakuwa na ladha tamu sana, MUDA UTATUAMBIA.

8. Raheem Sterling, huyu ndiye Messi wa Guardiola ambaye bado yuko darasani. Kiungo huyu wa pembeni ndani ya miaka ambayo Pep atakaa City basi ataweza kuja kuwa mmoja wa viungo mahiri kabisa wa Uingereza na hasa kama akiendelea na kasi aliyonayo kwasasa. Ingawa bado anahitajika kujifunza zaidi kutafuta magoli.

9. Silva na Fernandinho hawa ndiyo wachezaji ambao wataendelea kumpa Guardiola kiburi dhidi ya timu yoyote ile anayokutana, unaweza kusema hawa ndiyo injini ya gari la City ktk safari yoyote ile na kwenye barabara yoyote ile.

10. Ile sentensi ya kwamba “mpira ni mchezo wa makosa” imedhihirishwa na karibu magoli yote ambayo City wamefungwa leo. Makosa ambayo City waliyafanya yanaonyesha wazi kwamba bado falsafa ya Pep ndani ya klabu hiyo itachukua muda zaidi kuweza kueleweka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *