Niliyoyaona Mourinho akifedheheshwa Darajani, United ikifia kwenye miguu ya Kante

Mourinho 3

Conte na umahiri wa mfumo wa 3-4-3

Conte=3-4-3 na 3-4-3=Conte, hayo ni mambo mawili ambayo huwezi kuyaachanisha kwasasa ndani ya klabu ya Chelsea. Mfumo huo ndiyo uliompa Conte vikombe wakati akiifundisha Juventus na kwasasa ndiyo mfumo ambao unaonekana kuing’arisha Chelsea.

Ni mfumo ambao unaifanya Chelsea kuwa bora kwenye ukabaji, na hatari zaidi kwenye kushambulia. Tayari mfumo huo umeipa Chelsea alama 9 na magoli tisa huku pia wakizuia nyavu zao kutikiswa (clean sheet) mara. tatu. 2.

Kante na Matic ni injini za Chelsea

Manchester United walikuwa mahututi dhidi ya Hazard, Pedro na Moses lakini walifia kwenye miguu ya Kante na Matic, hawa ndiyo wachezaji wawili ambao waliifanya Chelsea iweze kukaba na kushambulia kwa urahisi.

Fellaini na Herrera walipotezwa kabisa na umahiri wa viungo hawa wa Chelsea na ndipo dhahama ya magoli ikawakuta United.

Mfumo wa 3-4-3 umemfanya Kante aweze kusogea mbele zaidi na kuweza kushambulia tofauti na hapo mwanzo na leo akaweza kuipatia Chelsea goli.

Luiz na Alonso waing’arisha 3-4-3

Usajili wa Luiz na Alonso umerahisisha mfumo wa 3-4-3 kuchezeka ndani ya Chelsea, ukiangalia kwenye mchezo wa leo Luiz alikuwa na kazi ya kuhakikisha timu inacheza kutokea golini kwenda mbele huku Alonso akiwa na kazi ya kuufanya uwanja kuwa mkubwa kuipa kazi United kukaba. Ndiyo maana hatari ya Lingard na Valencia ilikuwa ndogo sana.

Chelsea na falsafa za Conte

Ukiachana na matokeo ya mchezo wenyewe Chelsea wanaonekana kuanza kuelewa falsafa za Conte kuanzia namna ambavyo wanakaba na kuanzisha mashambulizi unapata picha ya nini hasa kinaendelea pale Cobhan (uwanja wa mazoezi wa Chelsea).

Namna ambavyo walianza mchezo wa leo na kupata goli kwenye sekunde ya 30 tu unaona kabisa kwamba Stamford Bridge panaweza kuwa sehemu hatari kwa wengi.

Victor Moses afufuka

Victor Moses, kijana kutoka Nigeria ni kama amezaliwa upya chini ya Conte, winga ya kulia kwasasa anaimiliki barabara kabisa huku pia akitimiza jukumu la kukaba ipasavyo, dk ya 77 anatoka Hazard na dk ya 78 anatoka Costa anaingia Willian na Batshuayi na hapo ndipo unapojua kwamba Chelsea imebadilika na itazidi kubadilika chini ya Conte.

Kipi bora cha Mourinho ni kipi?

Jose Mourinho ana kazi kubwa ndani ya kikosi cha Manchester United, ukiachana na eneo la De Gea kwingine kote kuna hali ya sintofahamu, eneo la mabeki limehusika moja kwa moja kufungwa kwenye goli la kwanza na la pili huku viungo wakihusika moja kwa moja kwa goli tatu na la nne na hapo ndipo kichwa cha Jose kinapouma kwasababu timu ile ile (ukimtoa Lingard) ndani ya wiki moja imepata matokeo ya sare dhidi ya Liver na leo kuchapwa goli nne.

Viungo wakabaji wa United Mmmh!

Matic alimpa Jose ubingwa na Kante ndiye mchezaji wa kwanza Jose kumtaka baada ya kupewa kazi ya kuifundisha United na leo dhahiri kabisa imeonekana umuhimu wa wachezaji hawa, eneo la katikati la Manchester United lilizidiwa kwa kiasi kikubwa na ni kwasababu kiuhalisia Fellaini na Herrera sio aina ya wachezaji ambao wanafiti kwenye mfumo wa Mourinho hasa wa kukaba na kutawala eneo la katikati.

Dah! Paul Pogba wa pauni milioni 100

Paul Pogba ni tatizo na ni suluhisho ndani ya kikosi cha Manchester United, mpaka sasa Mourinho anatafuta namna ya kumfanya Pogba aweze kung’ara uwanjani anatafuta namna ya kumfanya Pogba aweze kuwa bora na kuiboresha United huku pia Pogba akijaribu kucheza ili kuthibitisha kwamba yeye thamani yake ni pauni milioni 100.

Hapo ndipo timu inapopata wakati mgumu ukiangalia kwa sehemu kubwa ya mchezo wa leo Pogba hakuonekana kabisa hivyo mpaka hapo Mou atakapoweza kufanya hilo ndipo United itaweza kuwa bora na kuogopwa tena.

Ibrahimovic vipi tena?

Zlatan Ibrahimovic, alianza ligi kwa kasi sana na kufunga magoli manne katika michezo ya mwanzoni ila mpaka sasa hajafunga goli lolote katika michezo mitano ya ligi. Zaidi sana akionekana kukosa nafasi nyingi za wazi. Na katika mchezo huu hakuonekana kama ana hatari sana jambo lililofanya United washambulie zaidi kupitia pembeni na kupiga krosi ambazo nyingi hazikuwa na malengo.

Bado Zlatan anatakiwa kufanya kazi zaidi ili kuipa United uhai eneo la mbele ila kwasasa hata akianzia benchi hakuna atakayelalamika.

Wachezaji wa Mourinho ni kina nani?

Kwa namna United walivyoteseka leo hapo ndipo unapojiuliza swali kwamba hivi kweli Manchester ina wachezaji wa aina ya Mourinho, nani ni Matic, nani ni Terry, nani ni Fabregas, nani ni Willian ndani ya Manchester. Ukiangalia kwa jicho la tatu ni kama vile United imejaa wachezaji ambao wanapenda kushambulia zaidi yaani “offensive players” kuliko kukaba yaani “defensive player” na sio tu namna wanavyocheza bali hata akilini mwao (mind set) na hapo ndipo falsafa za Mourinho zinapopata kazi kuingia vichwani mwao kwasababu kocha huyo asili yake ni kuzuia kwanza na kushambulia ni baadaye.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *