Niliyoyaona Anfield, Mourinho akisaka matokeo salama

Full time

Liverpool 0-0 Manchester United
1. Liverpool bado wana timu ila kwa zaidi ya dakika 50 ni kama huu mchezo ulikuwa mkubwa kuliko wachezaji wenyewe. Ule ubora wa “movements” za kina Mane na Firmino haukuonekana kabisa huku wakipiga pasi nyingi mbovu kwa sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza hasa katikati ya uwanja.
2.  Umahiri wa Coutinho

Coutinho ni mchezaji mahiri, huyu ndiye alikuwa kiini cha mengi mazuri ya Liver na kama sio umahiri wa De Gea basi lile shuti lingewapa alama klabu ya Liver, kwa sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza alikuwa anacheza chini sana na hivyo kumchukua muda mrefu kulifikia lango la United.
3. Hendo na pasi za pembeni

Henderson ni kiungo mzuri ingawa kama anataka kufikia kule ambako Alonso na Gerrard waliweza kuifikisha Liver basi anatakiwa kulifanyia kazi swala la kuifanya timu ichezee kutokea chini, Hendo anatakiwa kuwa bora katika upigaji wa pasi za kuelekea mbele na hivyo kuwapunguzia majukumu viungo washambuliaji wa Liverpol hasa Coutinho.
4.  Wengi watanyanyasika Anfield

Matokeo ya sare waliyoyapata ya Liverpool yanaweza kukudanganya katika kujua umahiri wa timu hii ila dakika 15 za mwishoni zilitosha kuona kitu gani hasa ambacho Klopp anakijenga ndani ya Anfield, nafikiri bado vilabu vingi ndani ya Ligi Kuu Uingereza vitateseka vitakapocheza na Liverpool hasa Anfield.
5. Karius bado anahitajika kuonyesha utulivu kama anataka kumpoteza kabisa Mignolet leo ni kama hii dabi ilikuwa kubwa kwake na kumfanya akose utulivu, Emre Can sio Georginio Wijnaldum, Can ni mzuri ktk mchezo wa kuzuia zaidi (defensive game) tofauti kabisa na namna Liver wanavyocheza (offensive game) na hivyo kuifanya timu ikose “flow” nzuri kutokea eneo la nyuma.
6. Mourinho na matokeo salama

Jose Mourinho alijua udhaifu wa timu yake na alijua kwamba kama akipishana na Liverpool basi dhahama inaweza kumkuta ikabidi awape Liverpool mpira yeye akabaki na mbinu zake. kwa kifupi unaweza kusema Mou anajua namna ya kutafuta matokeo salama kwake. Suluhu aliyoipata itamfanya afarijike kuelekea EUROPA.
7. Ander Herrera mchezaji bora wa mechi

Ander Herrera, mi napenda kumwita bastola ya Mourinho yenye kiwambo cha sauti, bonge ya kiungo mkabaji, mpigaji pasi yeye, mkabaji yeye, mwelekezaji yeye na kwa mchezo wa leo binafsi nampa tuzo ya mchezaji bora wa pambano. Huyu ndiye mchezaji ambaye analeta UWIANO mkubwa ndani ya United. Kazi yake akishirikiana na Fellaini iliwafanya United wawe salama huku wakizima mashambulizi ya kina Mane, Firmino na Sturridge.
8. Antonio Valencia, mtumishi mwaminifu wa Mourinho

Antonio Valencia, ama kama una mahaba mazito zaidi unaweza kumwita “mtumishi mwaminifu wa Jose”. Mshikaji ndani yake kuna wachezaji wawili mmoja winga na wingine beki wa kulia, kwa anavyocheza unaweza kusema ana mapafu manne, usiku wa leo alifanya karibu kila kitu kwa ufanisi na ile “tackling” dhidi ya Firmino ilikamilisha umahiri wake ndani ya Anfield.
9. Mourinho na changamoto ya kusaka kikosi Bora

Ndiyo matokeo haya ya sare ni faraja kwa Mourinho kwasababu ni matokeo aliyoyatafuta ila ni dhahiri kwamba kocha huyu bado anakitafuta kikosi chake bora, bado anatafuta namna ya kumfanya Pogba ang’are na kufanania zile pauni 100 lakini pia bado anatamani kuona United ikiogopwa kwa namna ya mchezo wake.
10. Tutasikia mengi kuhusu Rooney

Dakika ya 77 anatoka Rashford anaingia Rooney, ni dhahiri kwamba kwasasa ana miaka 30 lakini pia akili na mwili wake vinashindana katika kufanya maamuzi. Mara ya mwisho Rooney kuanzia benchi kwenye michezo mitatu mfululizo ya ligi ni mwaka 2003 akiwa anaichezea Everton. Mpaka huu msimu utakapokwisha mengi tutayasikia dhidi yake, nani hawajui Waingereza?

NK: Ila kwa kifupi huu ulikuwa mchezo MBOVU wa mahasimu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *