Nenda tu Julio, tuache na waamuzi wetu

Kocha wa Mwadui, Jamhuri Kihwelo ' Julio'

Kocha wa Mwadui, Jamhuri Kihwelo ‘ Julio’


Mwandishi na mhandisi, Glen McQuirk aliwahi kuuuliza ulimwengu kwamba “Hivi hiki ndicho bora hasa unachoweza kukifanya?” Hakutoa majibu baada ya hapo.

Aliamua kuuacha ulimwengu kwenye swali hilo, hajaamua kutoa jibu lolote mpaka sasa, kitu kizuri ni kwamba, bado anapumua na swali lake hilo lipo kwenye kitabu chake, analiona na analikumbuka kwa kuwa ni moja kati ya nukuu zake.

Natamani siku moja afungue mdomo wake kutupatia majibu sahihi ambayo yataambatana na maelezo sahihi pia juu ya kile alichokimaanisha mbele ya ulimwengu kwenye swali hilo. Hivi hiki ndicho bora hasa unachoweza kukifanya?

Ninaamini kwamba alitamani kila mmoja wetu ajaze mtihani huo kwa majibu anayoyaamini kuwa ni sahihi kisha ajisahihishie mwenyewe na ajigawie maksi mwenyewe. Hapo kitakachofuata ni juu ya mtu mwenyewe, yeye hatakuwa na deni, hahusiki ndiyo maana hajatoa majibu.

Ningependa pia binaadamu mmoja mwenye ushawishi kwenye vyombo vya habari, anayetajwa kuwa na maneno mengi sana, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ajiulize swali hili, hivi hiki ndicho sahihi hasa ninachoweza kukifanya?

Nani anahitaji kusimuliwa juu ya Julio na hatma yake ya soka? Ameshatishia sana kujiuzulu kufundisha mchezo huo kisa kikiwa ni kile alichokiita kutokuwa ‘fair’ kwa waamuzi wetu. Hatimaye amesikika akitangaza kuachana na mchezo huo.

Lakini hiki anachokifanya Julio ndicho sahihi kinachotakiwa kufanywa? Nawaza sana hapa, natamani Glen McQuirk aje mbele yetu kutuambia alikuwa na maana gani kutuuliza swali hili ninalomuuliza Julio muda huu.

Siwezi kukuacha kama ambavyo McQuirk alivyouacha ulimwengu, ngoja nikuambie, Julio hakufanya kitendo sahihi na hatafanya kitendo sahihi kuuacha mpira wetu kisa waamuzi kutokuwa waungwana kama alivyosema, hii ni kama sababu aliyoisema ndiyo yenye uhalisia.

Anatakiwa kuacha kufundisha soka kutokana na mwenendo wake mbovu ndani ya Mwadui, kuifanya kwake Mwadui kuwa katika timu za chini kwenye msimamo na upepo mbaya wa kutopata matokeo ya ushindi ndicho kinachopaswa kuwa sababu ya kuachana na soka na si waamuzi kutokuwa waungwana.

Siwezi kuingia kwenye makosa ya kukataa kukosa uungwana kwa baadhi ya waamuzi wetu, hawalitendei haki soka letu hata kidogo.

Lazima tufanye kitu sahihi kwenye sehemu sahihi na wakati sahihi. Lazima lijulikane tatizo linalopelekea waamuzi kufanya maamuzi ya kipuuzi dimbani.

Chanzo ni kipi? Hawana mafunzo ya kutosha? Wanafanya makusudi? Wanachukua rushwa? Najiuliza maswali mengi sana, sina wa kunipatia majibu.

Bodi ya Ligi haipaswi kuwafungia hadharani, wanachotakiwa kukifanya ni kuwaondoa kwenye orodha ya waamuzi watakaochezesha michezo yetu kimya kimya pasipo wenyewe kujua mpaka watakapoonekana kurudisha viwango vyao.

Nafikiri huu unaweza kuwa mwarobaini sahihi kwenye hili gonjwa la waamuzi linalolimaliza soka letu taratibu!

Julio tuachie soka letu na waamuzi wetu ingawa kukimbia tatizo si njua sahihi ya kutatua matatizo, nenda tu, hawa ndio waamuzi tulionao na ukisubiri wazaliwe wengine huenda ukafa bila kuliona hili likitokea.

Julio kisingizio hiki hakipaswi kuwa cha kwanza, kilistahili kuwa cha pili baada ya matokeo yako mabovu msimu huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *