Lazima tukubali Yanga ndie bingwa halali

Mashabiki na wachezaji wa Yanga wakati wa sherehe za ubingwa ( Picha /Hisani )

Msimu wa VPL 2016/17 umemalizika kwa timu ya Yanga kuchukua ubingwa. Naamini, pamoja na ushindani uliokuwepo, Yanga walistahili kuwa mabingwa ndio sababu wakawa.

Hongereni sana timu ya Yanga, wachezaji, viongozi, wapenzi, washabiki na wadau wote kwa umoja wenu kufanikisha timu yenu kuchukua Ubingwa msimu huu, kubwa zaidi ubingwa huu ukiwawezesha kutwaa kombe mara tatu mfululizo.

Niwaombe sasa, muandae kikosi imara, madhubuti, chenye uwezo mkubwa wa kupambana na kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.

Ushiriki wenu katika mashindano ya Kimataifa, pamoja na kwamba mnakwenda kama timu, kwa namna fulani mnaiwakilisha nchi. Wapo watakaopingana na kauli yangu hii laini ukweli ndio huo. Mnapocheza nje huko, lazima iwe isiwe neno Tanzania litatajwa tu, linapotajwa kupitia ninyi ni sawa na kuiwakilisha na kuitangaza nchi yetu.

Ushiriki wenu huko, ukaitangaze Tanzania kwa mema na mafanikio, mkifanya vizuri ninyi ni sifa kwenu na taifa pia.

Msiende huko kunusa tu kama ajuza na kikebe cha ugolo, mchezo mmoja tu ukawaondosha mashindanoni, yaani kutolewa hatua za awali ni aibu kwenu na Taifa. Hii mtaiepuka kwa kufanya maandalizi mapema ikiwa ni Pamoja na kufanya usajili mzuri na makini.

Naamini, Charles Boniface Mkwasa, kwa weledi wake katika soka, mkimpa ushirikiano atawafikisha kileleni kwa mshindo mkubwa!

Sisi Ruvu Shooting, msimu huu tumekubali changamoto zimetuweka hapo zilipotuweka lakini naamini, nanyi naamini mnaamini ninavyoamini mimi kwamba, Ruvu Shooting ni bora kuliko, changamoto tu zimetunyima ubingwa!

Tunajipanga msimu wa 2017/18 tufanye makubwa katika ligi ili tupate fursa ya kushiriki mashindano ya kimataifa tukateme cheche zetu huko! Inawezekana, ni maandalizi tu!

Yanga, “Mbele daima” iwe mbele kweli, mbele msiigeuze ikawa nyuma kwani kwakufanya hivyo itakuwa aibu kubwa! Nyuma hakufai, mbele ndiko haswaaaa kwenyewe! Ukiona mtu anapenda nyuma huyo ni tatizo, yaani anafurahia kushuka daraja, hafai! Msiwe ninyi, Kitaifa na Kimataifa.

 

imeandika na Masau Bwire

Msemaji wa Ruvu Shooting

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *