Elias Maguli ondoa nadhiri…cheza soka

Maguli

Kwa wale watu wa imani watanielewa katika hili. Kuna baadhi ya mafundisho ya dini yanasema kuna mitihani hutokea katika mfumo wa maisha ya mwanadamu kama andalio la maisha yajayo.

Dhahabu ili iwe safi ni lazima ipitie moto mkali sana . Kuna nahau na maneno kadha wa kadha kuonesha jambo la kheri ama baraka lina njia zake hili litimie katika ubora wake .

Ifike wakati wachezaji wetu mkomae kifikra na kimawazo kutambua mfumo wa soka letu na mustakabali wa maisha yenu kisoka na jinsi ya kutunza utu , kipaji na hadhi yenu.

Nimekuwa mfatiliaji mzuri wa soka la nchi hii hususani vilabu vyetu vikubwa vya Simba na Yanga. Mifumo yao ya usajili, uendeshaji vilabu, utunzaji wa vipaji vya wachezaji na mambo mengine kwa upana sana. Vinashabihana sana.

Kwanza kabisa niwaase wachezaji wetu ndani ya soka letu hapa nchini kuna mfumo batili nyuma ya pazia . Huu ndio mfumo ambao kwa miongo kazaa umeutia kilema ustawi wa soka la nchi hii.

Huu ni mfumo ambao haupo kwa maslahi ya kuendeleza soka la nchi hii bali maslahi binafsi ya watu . Pia ni mfumo ambao ndio kwa miongo kadhaa unatupatia viongozi wa soka ambao hawana A wala B katika elimu juu ya utawala wa soka ( football management) .

Huu ndio mfumo ambao wadau wenye uchungu na soka la nchi hii wameubatiza jina na kuuita ” siasa ya soka”. Wakifananisha matendo ya kisiasa ambayo mengi yao hayana msingi wa kisayansi.

Sasa wachezaji chipukizi ama wenye vipaji vizuri kama Elias Maguli na wengine wanapokubali kuingizwa katika mfumo huo basi siku zao za kucheza soka huhesabika.

Maguli yaliyokukuta Simba SC ndio mtaji wako wa mafanikio leo. Usikubali kwa namna yoyote ile kutumia muda wako wa thamani kuonesha chuki dhidi ya timu hiyo au kula viapo na nadhiri ya kutokuja tena kuichezea timu hiyo.

Waliokunyima nafasi ya kuitumikia Simba ambayo ulionesha mapenzi ya kuitumikia ndio kwa namna moja ama nyingine wamekupa nguvu na kasi ya kuonesha kipaji chako .

Fanya kazi yako. Matokeo chanya ya kazi zako ni kiboko tosha kwa wale walioamini umekwisha au kutokuwa na uwezo wa kuitumikia klabu hiyo.

Simba SC itabaki kuwa Simba SC kwa maana ya chapa-jina ya timu lakini viongozi, wachezaji ama wadau waliokufanya ufikie kauli hiyo ni wanapita sasa kuweka nadhiri ilihali hatujui maisha ya kesho si vyema.

Soka ni maisha yako hivyo ondoa nadhiri katika maisha ya soka . Angalia masilahi na kipaji chako.

Ni ukweli usiopingika pale mtu anaposimama kama kikwazo inaumiza sana lakini mitihani ya maisha tuigeuze chachu ya mafanikio yetu kwa kupata tafsiri chanya.

Simba hii ilimletea mizengwe Samata akagoma kuichezea lakini alipopewa gari lake aliichezea na pia klabu kumpa kibali cha kucheza nje.

Je Samata leo ni adui wa Simba ? La hasha.

Mantiki yangu kubwa ni wachezaji wetu kujitambua pale wanapotoa kauli zao na mustakabali wa maisha yao.

Chezeni mpira siasa za soka waachieni viongozi . Watajifunza tu siku mojanjia bora za kuliendesha soka letu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *