Dida alishikishwa mzigo na waarabu na mambo mengine matatu Yanga na MCA

Dida

Deogratius Munishi ‘Dida’ ( Picha/ Soka360)


Hakuna shaka kuwa Deogratius Munishi ‘Dida’ ni kipa namba moja wa Yanga na Jumamosi usiku alisimama langoni dhidi ya MC Alger katika mchezo wa marudiano wa kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kwa mara nyingine tena, Dida alirudia makosa yale yale ambayo kwa namna moja yanamfanya kuhusika katika mabao mawili kati ya manne waliyoruhusu Yanga.

Katika bao la pili licha ya kuwa Nadir Haroub ndiye aliyeanza kutengeneza kosa, Dida hawezi kukosa lawama kwa kushindwa kuupanga ukuta wake na pia kukaa vibaya na hatimaye kujarbu kudaka mpira wa faulo ya Derrardja utadhani anachota maji kwa karai.

Alihusika tena katika bao la nne pamoja na kuwa tunaweza kumkingia kifua kwa kushindwa kulindwa na ngome yake kiasi cha kubaki ana kwa ana na mfungaji. Utemaji wake wa mpira katika miguu ya mfungaji ni jambo linalomfanya kuwa mmoja wa ‘ wapishi’ wa bao la Zerdab lililoikata maini Yanga.

Kama Dida anayeshikilia rekodi ya kipekee ya kuvichezea vilabu vigogo watatu wa Ligi Kuu, Azam, Yanga na Simba pamoja na kuitumikia timu ya Taifa ya Tanzania kwa muda anaruhusu mabao ya aina ile inakuwaje tunafunga akili zetu na kuanza kumshutumu kipa wa Mbao, Eric Ngwengwe kuruhusu mabao ya ‘miamala’?

Tunatoa wapi ujasiri wa kumtuhumu Ngwengwe kuwa alipewa kit kidogo wakati inaezekana kabisa ni udhaifu, kukosa umakini na uwezo wa makipa wetu? Katika mechi kati ya Simba na Mbao, mabao matatu kati ya matano yaliyofungwa yalihusisha udhaifu wa makipa wa pande zote mbili.

Hakuna aliyesikika akimshutumu Manyika kwa kuhongwa na Mbao, na sitashangaa nisiposikia Dida akituhumiwa kula pesa za waarabu kwa sababu tunaujua ukweli.

Ukweli ni kuwa hawa ndio makipa wetu ndio maana hata wale tunaona ndio bora zaidi bado ni ngumu kupenya katika soko la nje hata barani Afrika.  Soka ni mchezo wa makosa lakini kwetu tumegeuza mchezo wa makosa kuwa soka letu.

2. Fitna za waarabu

Ni msamiati mwingine wa kijinga katika soka letu. Cha kushangaza karibu wadau wote wanaendelea kuukuza. Utasikia blah blah blah nyingi kuhusu ‘fitna za waarabu’ lakini mwishowe tunafungwa kwa makosa yetu wenyewe.

Soka haujawahi kuwa mchezo wa waungwana japo ni mchezo wa kiungwana. Daima unaongozwa na watu wenye aina fulani ya ‘uhuni’ wasioona haya kusaka ushindi kwa njia zisizo za kistaarabu. Tulikubali hili na kuacha kulialia na kupiga mayowe kila mara tunapopangwa na timu za Uarabuni. Kuendekeza kulialia ni kuzidi kudhihirisha uchanga na udhaifu wetu katika soka la kimataifa.

Inakuwaje tunaendelea kulia kilio kile kile kwa miaka zaidi ya 40? Muda wote huo hatujajifunza tu jinsi ya kukabiliana na ‘watukutu’ zaidi kuwazuia wasichukue video za mechi katika ulimwengu wa kisasa ambao naweza kukaa sehemu yoyote uwanjani na kurekodi video kwa simu?

Mwaka jana Azam waliwazuia Esperance kutochukua video pale Chamazi lakini matokeo yake wakapigwa 3-0, Yanga nao walifanya hivyo hivyo mwaka huu kwa ‘makomandoo’ wao kuwazuia waandishi wa Algeria kuchukua video bado haikuwasaidia katika kipigo cha mabao 4-0.

Hata bila kuongelea mambo ya nje ya uwanja, ni wazi kuwa tatizo kubwa ni umakini wa kutumia nafasi tunazopata. Azam alipata nafasi nyingi dhidi ya Esperance lakini akaibuka na ushindi finyu wa mabao 2-1 nyumbani kabla ya kupigwa 3-0 katika marudiano.

Yanga nao hivyo hivyo, walipata nafasi nyimgi kipindi cha kwanza dhidi ya MCA uwanja wa Taifa lakini hawakufunga hata bao moja. Bao pekee la Thaban Kamusoko kipindi cha pili likawapa ushindi finyu wa roho juu kuelekea mechi ya marudiano.

Ni kweli mambo ya nje ya uwanja yapo lakini tusiyape kipaumbele kiasi cha kufunika uwezo halisi wa timu zetu na kikubwa zaidi tunawajengea hofu wachezaji wetu ambao wengi ni watanzania wasiokuwa na utamaduni wa kushikamana wanaposhikwa zaidi ya kusinyaa na kusubiri ‘viongozi, mashabiki na wadau tulie kuonewa’.


George Lwandamina akifuatilia mchezo wa dhidi ya MCA ( Picha/ Soka360)

George Lwandamina akifuatilia mchezo wa dhidi ya MCA ( Picha/ Soka360)


4. Kwa Lwandamina Yanga iliacha bunduki ikachukua rungu?

Kwa mara ya pili ndani ya muda fupi tangu achukue mikoba ya Hans Van Der Pluijm, kocha Lwandamina ameshuhudia kikosi chake kikipokea kipigo cha mabao 4-0. Haikuwahi kumtokea Hans licha ya kukutana na timu kubwa zaidi.

Pamoja na udhaifu wake si sawa kumbebesha mzigo wa lawama Lwandamina wakati ameingia Yanga na kukumbana na kipindi kigumu cha mpito ndani na nje ya uwanja.

Hatujui kama amelipwa mshahara. Anafundisha wachezaji ambao hawajalipwa huku akikabiliana na janga la majeruhi kwa wachezaji tegemeo.

Aliwakosa Donald Ngoma na Amissi Tambwe katika pambano dhidi ya Zanaco na katika mechi dhidi ya MCA aliwakosa Vincent Bossou, Obrey Chirwa pamoja na Tambwe na Ngoma waliolazimika kutokea benchi licha ya kutokuwa fiti.

4. Tutafia Uwanjani

Tunautumia vibaya huu msemo na matokeo yake tunajiongezea presha bure na kufungwa kwa makosa yetu sisi wenyewe.

Huwa napata mashaka kila nikiusikia huu msemo, mara nyingi wachezaji wetu huwa wanajifia uwanjani kabisa. Hatujazoea presha, tunauwezo mdogo wa kukabiliana nazo hivyo si busara kuendelea na kujipa presha za bure.

Kabla ya mechi tunaambiwa ‘Tutafia uwanjani’ mwishowe mashabiki wa Tanzania kuziona timu zao zikicheza pungufu hata kabla ya kupewa kadi nyekundu maana kuna wachezaji huwa wameshakufa hata kabla ya kipenga cha kwanza.

Jumamosi usiku sikuona wachezaji wa Yanga wakijaribu kufa kwa ajili ya jezi kama tulivyoahidiwa. Shambulizi pekee la maana nililiona kutoka kwa Yanga ni lile la Kelvin Yondani kumtemea mate mpinzani wake.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *