Busungu, jiandae na ule wakati wa kuyameza maneno yako

Busungu

Mwaka 1990 dunia ilishuhudia uzazi wa binaadamu mtukutu sana ndani na nje ya uwanja. Binaadamu huyu aliyepatina baada ya mbegu za kiume za mzazi mwenye asili ya Ghana kurutibasha yai la kike la mama wa kiumbe hiki kilichopewa jina la Mario Balotelli, dunia ilimfahamu hasa kama mtukutu.

Licha ya dunia kumfahamu hivyo, Balotelli aliyekulia kwenye vituo vya watoto wa kulelea wakimbizi nchini Italia, hakuwahi kuthubutu kukifanya kipaji chake kupotezwa na utukutu wake. Hakuwahi hata siku moja na kuna wakati huwa anaamini yeye ni bora zaidi ya yeyote kwenye ulimwengu huu.

Mario Balotell akishangilia bao lake katika moja ya mechi za ligi kuu Italia.  ( Picha Claudio Villa/Getty Images)

Mario Balotell akishangilia bao lake katika moja ya mechi za ligi kuu Italia. ( Picha Claudio Villa/Getty Images)

Balotelli, dunia ilianza kumfahamu kwa sababu ya kucheza mpira, utukutu ulifuata baada ya kujulikana lakini sifa kubwa ya kiumbe hiki, hahitaji kukipoteza kipaji chake kirahisi, ndiyo maana leo hii ni malaika kwenye klabu ya Nice.

Malimi Busungu ni mshambuliaji wa Kitanzania aliyefanya makubwa mno na Mgambo Shooting kabla ya kushuka daraja. Ni yeye aliyesajiliwa na Yanga kwa kusudi la kuongeza upana wa kikosi na mwanzo wake kikosini hapo haukuwa wenye urafiki na ubaya.

Busungu ni moja kati ya wachezaji wenye uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja kwenye eneo la ushambuliaji. Unaweza kumtumia kama winga au mshambuliaji nambari moja na akakupa ulichokihitaji pindi akiwa kwenye ubora wake.

Sifa ya kucheza mipira ya hewani ni moja kati ya rafiki wema wa kipaji chake. Lakini tunavyozungumza benchi ndiye rafiki yake mwema kwa sasa. Kwanini? Kiwango kimepungua miguuni mwake? Si yule tena?

Majibu ya maswali yote haya anayeweza kuyajibu kwa usahihi ni Busungu mwenyewe. Huenda umbali kutoka, Kabuku, Handeni mkoani Tanga ambako starehe zake ni chache mno kulinganisha na jiji la Dar es salaam analoishi hivi sasa umeondoka na nidhamu yake aliyokuwa nayo.

Busungu aliwahi kuyatoa maneno juu ya Hans van Pluijm, akahusisha na chuki dhidi yake na kuifanya kuwa sababu kuu ya kutopangwa kikosi cha kwanza. Hapo nilikuwa nakukumbusha tu. Hivi sasa Pluijm hayupo kwenye benchi la ufundi.

Kocha wake mpya ni George Lwandamina ambaye amecheza mechi mbili za Ligi na hatujamuona Malimi Busungu kwenye kikosi cha kwanza, hayupo fiti? Busungu alianzishwa kwenye mechi dhidi ya JKU ambayo Yanga ilifungwa mabao 2-0. Busungu alikuwepo jioni ya siku ile.

Lakini Lwandamina ameonekana kumwamini mchezaji mwenzake, Said Juma Makapu kwenye eneo la kiungo wa chini au kiungo wa ulinzi. Unapata picha gani hapa? Ni kwamba Lwandamina ukimshawishi na kumuahidi kumtekelezea majukumu yake, atakuamini na kukupa nafasi.

Kwani Lwandamina hajamuona Busungu? Kwanini amwamini Haruna Niyonzima kucheza nyuma ya mshambuliaji? Nina maswali mengi hapo! Ninachokiamini ni kwamba, ule wakati wa Busungu kuyameza maneno yake unawadia taratiibu. Utafika tu endapo ataendelea na muendeleza huu wa sasa.

Kitu ambacho Busungu amekikosa kwenye ubongo wake ni ubongo wa Balotelli. Balotelli hawezi kuruhusu kipaji chake kipotee kirahisi, Busungu hatakiwi kuruhusu kipaji chake kipotelee benchi. Cha kufanya anakijua na kama hakijui ni bora astaafu tu soka.

Nani hakumbuki utukutu wa Athumani Idd Chuji? Lakini hakuruhusu utukutu wake uyeyushe kipaji alichozaliwa nacho, ni wakati sasa wa Busungu kutuonesha kwamba anastahili kupangwa na Lwandamina kwenye kikosi chake baada ya Pluijm kuwa mkurugenzi wa ufundi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *