Tathmini ya makundi Kombe la Dunia 2018

Makundi ya Kombe la Dunia yamepangwa nchini Urusi ambapo mataifa 32 yaliyofuzu yamegawanywa katika makundi 8 yenye timu nne kila moja.

Kundi A

Kundi hili ndipo alipo mwenyeji wa mashindano haya nchi ya Urusi akiwa sambamba na Saudi Arabia , Misri na Uruguay. Katika kundi hili Urusi ndio nchi pekee iliyo chini kisoka katika viwango vya FIFA ikishika nafasi ya 65 wakifuata Saudi Arabia nafasi ya 63, Misri wanashika nafasi ya 31 na Uruguay wakiongoza kundi hili kwakuwa nafasi ya 21 katika ubora wa viwango vya soka duniani. Urusi ana kazi ya ziada kupenya kundi hili kama nchi mwenyeji kitakwimu ingawa ubora wa FIFA si kigezo sana katika maandalizi kimbinu na kiufundi kwa maana nzima ya muda mrefu wa kujiandaa mpaka mwezi juni mwakani. Mechi ya ufunguzi Urusi atakutana na Saudi Arabia ndio mechi pekee ambayo ana asilimia 50/50 kushinda ukiangalia ubora wa vikosi vya Uruguay ikiwa na kina Cavan na Suarez huku Mohamedi Salah akizidi kuonesha ubora wake na Liverpool hivyo kuingia katika uga wa wachezaji hatari watarajiwao katika fainali za kombe la dunia nchini Urusi mwakani na kikosi cha mafarao.

Kundi B

Kundi hili ndipo alipo mfalme wa soka kwa sasa duniani Christiano Ronaldo akiwa na kikosi cha Ureno kitakachofungua mechi za makundi na Uhispania. Ni fainali za mwisho kwa Ronaldo kutokana na umri wake na uwezo uwanjani kwa mtazamo wa miaka minne ijayo hivyo inatarajiwa kuwa makini sana kudhihirishia dunia ubora wake akiwa na kikosi cha Ureno . Uhispania hawakuwa bora michuano ya mwaka 2014 nchini Brazil hali iliyowafanya kushindwa kuvuka hatua ya makundi hivyo inaleta changamoto kwa Ureno , Morocco na Iran . Morocco anahitajika kuwa makini zaidi ikiwa mara yake ya kwanza kuingia katika michuano hiyo tangu fainali za mwaka 1998 nchini Ufaransa ili asijegeuka ngazi ya wenzake kusoka mbele.

Kundi C

Ufaransa anapewa nafasi kubwa kupenya kundi hili akiwa na wachezaji makini na wenye viwango vizuri kama kiungo wa Manchester United Paul Pogba , Giroud toka Arsenal na Griezman . Wengine kwenye kundi hili ni Australia, Peru na Denmark. Peru amerudi kwenye michuano hii baada ya kutoshiriki kwa miaka 38 akipitia njia ya mtoano. Endapo Ufaransa akizichanga vyema karata zake kuna uwezekano mkubwa wa kuingia hatua ya 16 bora!.

Kundi D

Kama ilivyo kwa kundi B , pia kundi hili lina mfalme mwingine wa soka Lionel Messi akiwa na kikosi cha Argentina sambamba na nchi za Croatia, Iceland na Nigeria. Kwa mtazamo wa karibu unaweza kusema Argentina wakiongozwa na Lionel Messi wanaweza kupita kwa urahisi lakini Iceland katika kumbukumbu fainali za Euro mwaka 2016 waliweza kumng’oa England licha ya udogo wao pia hakuna asiyekumbuka maajabu ya Croatia 1998 nchini Ufaransa. Ni kundi gumu kwa maana nzima ya Argentina hivi karibu kutokuwa na maendeleo mazuri kisoka ngazi ya ushindani. Nigeria hivi karibuni alicheza mechi ya kirafiki na Argentina na kumfunga 4-2 hivyo licha ya kupewa nafasi finyu kupenya lakini anaweza kusonga mbele katika kundi hili pia.

Kundi E

Mabingwa mara tano wa kombe la dunia ‘ the selecao ‘ Brazil yupo kundi hili akipewa nafasi kubwa kusonga mbele. Serbia , Costa Rica na Uswisi wana kazi ya ziada kumzuia Brazil kuingia hatua ya 16 bora kutoka kundi hili. Brazil ndio ilikuwa nchi ya kwanza kufuzu michuano hii na hivi karibuni chini ya kocha mzawa Tite wamekuwa na kiwango bora sana . Neymar Jr alishindwa kuipa kikombe Brazil mwaka 2014 hivi sasa anatarajiwa kuifanyia makubwa nchi hiyo kama key player ili aweze kuwa katika mizani ya watangulizi wake kama Rivaldo, Cafu, Gaucho , De Lima na wengineo.

Kundi F

Hili linahesabika kama kundi la kifo likiwa na bingwa mtetezi, Ujerumani ambaye ameingia hatua hii kwa kishindo baada ya kushinda mechi zote za kufuzu . Ujerumani yupo na wakali wengine kama Mexico, Sweden na Korea Kusini. Ni nchi ambazo soka lao linakuwa kwa kasi na wamekuwa na maandalizi mazuri kuelekea fainali hizi. Ni dhahiri Ujerumani wanapewa nafasi kupenya kundi hili lakini Mexico sio wakuwabeza waliweza kupenya hatua ya makundi fainali za mwaka 2014 nchini Brazil, pia Sweden ambao wamemzuia Italia kushiriki fainali hizi ikiwa ni mara ya kwanza tangia mwaka 1956!.

Kundi G

Kundi hili linajumuisha nchi za Ubelgiji, watoto wa malikia Elizabeth II England, Panama na Tunisia. Ubelgiji ndio vinara kisoka katika viwango vya FIFA katika kundi hili wakishika nafasi ya 5 wakifuatiwa na England waliopo nafasi ya 15. Tunisia mwakilishi toka Afrika wapo nafasi ya 27 na Panama nafasi ya 56. Kundi hili licha ya Ubelgiji kuwa bora kitakwimu lakini England wanapewa nafasi kubwa kusonga mbele. Wamekuwa na maandalizi mazuri kisoka kuliko fainali nyingi zilizopita wakitengeneza kizazi kipya cha soka cha akina Harry Kane . Meneja wa England wa hivi sasa Southgate fainali za mwaka 1998 alikuwa mlinzi wa kati wa England wakiwaadhibu Tunisia hivyo atajipanga vyema kulinda legacy yake na taifa hilo kwa ujumla.

Kundi H

Lewandowsky akiwa na timu yake ya Poland atakuwa anajaribu kupenya mbele ya timu zenye uchu wa kufika mbali kisoka katika michuano hiyo. Senegal walioweza kufika hatua ya robo fainali mwaka 2002 Cisse akiwa mchezaji na sasa nahodha tayari ameanza kuwapa waafrika matumaini ya kupenya kundi hilo kwa kiwango kizuri cha timu yake . Colombia na Japan pia ni mwiba mwingine kwa Poland. Ni kundi ambalo kila timu ina uwezo wa kuvuka hatua ya makundi endapo itakuwa na maandalizi mazuri.

Imeandaliwa na Samuel Samuel
0624006257

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *